Monday, December 23, 2024
spot_img

BARAZA LA WATOTO LAOMBA KUSHIRIKISHWA KUTUNGA SHERIA, KANUNI

RIPOTA PANORAMA

Arusha

BARAZA la Watoto la Taifa limeiomba  Serikali kuona umuhimu wa kuwashirikisha watoto katika kutunga sheria zitakazosaidia kuwabana watakaobainika kufanya vitendo vya ukatili dhidi yao.

Akizungumza kwenye mdahalo ulioandaliwa na Shirika la Save the Children, katika maadhimisho ya wiki ya AZAKI Jijini hapa, Mjumbe wa Kamati ya Baraza la Taifa la Watoto, Sabrina Salum (pichani juu) amesema vitendo vya ukatili dhidi ya watoto nchini vinaongezeka kwa sababu hakuna sheria kali za kuwaadhibu wanaowatendea watoto ukatili.

“Imefikia wakati watoto tunaogopa kwenda viwanjani kucheza, tunaogopa kwenda kwenye nyumba za ibada na maeneo mengine ya kutufanya tufurahie maisha, Serikali na Taasisi angalieni mambo haya kwa upekee, kama leo hali ni hii je 2050 itakuwaje? Watoto watakuwepo. Naomba haya yazingatiwe na haki ya kuishi kwetu watoto ni ya msingi,” amesema Sabrina.

Mtoto Yasin kutoka Dar es Salaam alitaka mamlaka zinazohusika kuweka utaratibu utakaosaidia wanafunzi wa Dar es Salaam na miji mingine mikubwa nchini kuepuka kero kubwa ya usafiri wanapokwenda shule na kurudi nyumbani.

“Ikiwezekana, zitungwe sheria au kanuni zitakazolazimisha kila daladala katika miji hiyo mikubwa kubeba wanafunzi wasiopungua kumi ili kupunguza taabu na mateso wanayopata wanafunzi,” amesisitiza.

Aidha, amependekeza magari ya Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama yatumike pia kuwachukua wanafunzi wanaorundikana vituoni ili kupunguza au kuondoka kero ya usafiri kwa wanafunzi.

Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE Shinyanga linalookoa, kulea na kumuendeleza mtoto wa kike, John Miyola ameyataka Mashirika ya Plan International na Save the Children kuruhusu mtu yeyote kupeleka malalamiko mahakamani badala ya dhamana hiyo kupewa wanasheria tu kwa sababu ya vitendo vya  rushwa vinavyoonekana kukithiri.

“Natamani suala hili liangaliwe kwa ukubwa ili kuwasaidia watoto wanaofanyiwa vitendo viovu na kuepuka kupotea kwa ushahidi kwa sababu ya matumizi  ya rushwa kwa waliotenda vitendo voovu,” amependekeza Miyola.

Sambamba na hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Wanawake na Watoto CWCD, Hindu Mbwego ameshauri sheria iangaliwe upya kuwabana wazazi kuwa na malezi ya heshima kwa watoto wao.

Ameongeza kuwa jukumu la kuea na kumuangalia mtoto yasiachiwe mashirika na taasisi tu bali sheria ichukue mkondo wake pale mzazi au mlezi atakapoonekana kutozingatia malezi ya mwanae.

“Zamani wazazi wetu walitufundisha utamaduni, walitenga muda kutufundisha desturi na historia ya maisha yetu lakini leo mzazi hana muda wa kuongea na kumfundisha mwanae, mtoto hajui lugha ya mama wala baba, suala la malezi lizingatiwe ili kukomesha ukatili kwa mtoto,” ameeleza Hindu.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya