PANORAMA RIPOTA
Arusha
SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Save the Children, limetoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wafanyabiashara wa Soko la Tengeru, lililoko wilayani Arumeru mkoani hapa, kwa ajili ya kupambana na utumikishwaji wa watoto kwenye masoko badala ya kwenda shule kusoma.
Akizungumza na wafanyabiashara katika soko hilo wakati akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia, meneja miradi wa shirika hilo Mkoa wa Dodoma, Mariam Mwita amesema wamefika eneo hilo kutoa elimu hiyo ikiwa ni mwendelezo wa shughuli za wiki ya Azaki zinazofanyika jijini hapa kwa siku tano.
Amasema wamekwenda kwenye soko hilo kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kwa kuwa wengi wao ni wazazi na walezi wa watoto.
“Tumetoa elimu ya ajira kwa watoto, lishe, kaya na familia lengo likiwa kuwagusa watoto ili wazazi wafanye biashara lakini kipato wanachokipata wakitumie kuboresha lishe za watoto, kuwanunulia mahitaji muhimu ikiwamo mahitaji ya shule, malazi na mavazi ili wakae katika mazingira mazuri yatakayowafanya kukua vizuri badala ya kutumia kipato hicho kunywea pombe,” anasisitiza.
Hata hivyo, amesema elimu hiyo imegusa maeneo ya utumikishwaji wa watoto masokoni na kilimo hai kwa kuwa kwa sasa kuna changamoto ya kilimo cha kutumia dawa na kinaathiri watoto ambao ndiyo wahanga wakubwa.
“Pia tumetoa elimu ya usafi wa mazingira, kunawa mikono, maandalizi ya chakula na mikopo kwa kuwaunganisha wafanyabiashara hao na taasisi za kifedha ikiwamo mabenki ili waweze kukopesheka kwa ajili ya kuongeza mtaji na kukuza vipato vyao,” amesema.
Maofisa wa Shirika lisilo la kiserikali la Save the Children wakiangalia bidhaa katika Soko la Tengeru, wilayani Arumeru ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Azaki yanayofanyioka jijini Arusha.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Meru wilayani Arumeru, Martha Mzava amesema wamekwenda soko hapo kwa ajili ya shughuli ya utoaji elimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali hususani masuala ya ajira kwa watoto, afya, kilimo na uwezeshaji wa kundi hilo kiuchumi.
“Uchumi wa wananchi ukiimarika watoto wataondokana na ukatili wa kijinsia kwa kuwa watapata mahitaji yao ya msingi ikiwamo chakula, mavazi na malazi.
Vilevile amesema wazazi na walezi watakuwa na akili kuweza kukaa na watoto wao na kuwasikiliza ili kuwakinga na vitendo vya ukatili.
Ameongeza kuwa katika hatua ya kukabiliana na matukio hayo, wanatoa elimu ngazi za kata, kwenye mikutano ya vijiji, pia wameunda Kamati za Kupambana na Kupinga Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA).
“Kamati hizi ziko kwenye kata zote kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Meru kwenye vijiji 60 kwa kuwa mpango mkakati wetu ni kupinga na kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto,” aliongeza.