Sunday, June 15, 2025
spot_img

WITO WATOLEWA KULINDA MIUNDOMBINU YA ANWANI ZA MAKAZI

RIPOTA WHMTH

Arusha

WANANCHI wameombwa kuilinda miundombinu ya Anuani za Makazi kwa kutumia ulinzi shirikishi kwa sababu imetengenezwa kwa gharama kubwa.

Wito huo umetolewa Agosti 14, 2024 jijini Arusha na Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mkoa, David Lyamong katika hafla ya ufunguzi wa uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi mkoani humo.           

Lyamong amesema katika baadhi ya maeneo zipo taarifa za miundombinu ya mfumo wa Anwani za Makazi ambayo ni nguzo za majina ya barabara na vibao vya namba za nyumba kuanza kuharibiwa.

 “Natambua katika baadhi ya maeneo, watu wameanza kuharibu nguzo za majina ya barabara na wengine wanaenda kuuza kama chuma chakavu. Serikali haitakubali hujuma dhidi ya miundombinu hii na  niwaombe wananchi kutoa taarifa za uharibifu na kuilinda,” amesema.

Lyamong amesema ni muhimu kutunza na kulinda miundombinu hiyo kutokana na umuhimu wake kwani kupitia programu yumishi ya mfumo huo,,, mtumiaji anaweza kuona huduma mbalimbali na kuzifikia ikiwemo hoteli, migahawa, hospitali, maduka na hata vivutio vya utalii.           

“Iwapo tutahakikisha taarifa za Anwani za Makazi ndani ya Mkoa wa Arusha ziko sahihi na zinahuishwa kila wakati, sio tu tutachochea kasi ya matumizi ya Mfumo wa NaPA kwa watalii bali tutaiwezesha nchi yetu kunufaika na fursa za uchumi wa kidijitali,” amesema Lyamong.  

Amekumbusha kuwa “wengi wetu tuliamini kuwa zoezi la Anwani za Makazi liliisha baada ya kufanya Sensa ya Watu na Makazi mwezi Agosti, 2022, lakini hapana, kila Mtanzania anatakiwa kufahamu kuwa utekelezaji wa zoezi hili ni endelevu.”  

Ufunguzi wa uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi katika Mkoa wa Arusha umefanyika kwa mara ya kwanza, ukitarajiwa kufanyika katika halmashauri sita za mkoa huo ambazo ni Arusha Jiji, Wilaya ya Arusha, Ngorongoro, Monduli, Karatu na Longido.

Lyamong amesema uamuzi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kufanya hafla ya uzindizi wa Anuani za Makazi kwenye halmashauri sita za mkoa huo kwa mara moja ni heshima kubwa kwa kutambua mchango wa Mkoa wa Arusha katika uchumi wa nchi.

Amesema kuwa uhakiki wa Anwani za Makazi unaambatana na mafunzo kwa wenyeviti na watendaji wa kata na mitaa wa halmashauri zote utakakofanyika uhakiki wa taarifa hivyo ni muhimu viongozi hao wakazingatia mafunzo hayo ili wakawasaidie wakazi wa maeneo yao.

“Endapo kila jengo litasajiliwa na kuonekana na kufikika kupitia mfumo wa Anwani za Makazi basi tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kuimarisha usalama ndani ya mkoa wetu wa Arusha na nchi kwa ujumla,” amesisitiza Katibu Tawala huyo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya