RIPOTA WA WHMTH
Arusha
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, yameanza kutoa Anwani za Makazi katika kambi, makazi, hoteli na vivutio vya utalii katika Hifadhi za Taifa.
Utoaji anuani huo utafanyika kwa awamu sambamba na kusajili taarifa za Anwani za Makazi katika mfumo wa kidigitali unaojulikana kwa jina la NaPA ili kuboresha shughuli za utalii katika hifadhi hizo.
Haya yanafanyika sasa baada ya mazungumzo na makubaliano baina ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambayo ni mratibu wa utekelezaji na matumizi ya mfumo, Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA.
Taarifa ya kuanza kutoa na kusajili Anwani za Makazi katika Hifadhi za Taifa ilitolewa Agosti 27, 2024 na Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Kamishna Massana Mwishawa jijini Arusha.
Alisema lengo ni kurahisisha shughuli za utalii na hasa kuwawezesha watalii kufika maeneo mbalimbali ya utalii kwa urahisi.
Kamishna Mwishawa ambaye alimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Juma Kuji alisema utoaji na usajili wa Anwani za Makazi utaanza Agosti 28, 2024 katika hifadhi na mbuga tatu zilizo ndani ya Mikoa ya Arusha na Manyara ambazo ni Hifadhi ya Taifa Arusha, Hifadhi ya Taifa Tarangire na Hifadhi ya Taifa Manyara.
Mratibu wa Anwani za Makazi Taifa, kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Jampyon Mbugi aliipongeza TANAPA kwa utayari wao wa kutumia mfumo huo ili kuboresha huduma za utalii.
Alisema mfumo wa Anwani za Makazi ni mfumo wa utambuzi ambao pamoja na mambo mengine utachochea jitihada za Serikali kutangaza utalii na utatumiwa na sekta zote za kijamii na kiuchumi zikiwemo za utalii, biashara, ulinzi, usalama na uokoaji.
Awali wakiwasilisha mada kuhusu mfumo huo unavyotumika na faida zake mbele ya Menejimenti ya TANAPA, wataalamu wa mfumo huo kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, waliainisha faida ambazo TANAPA itazipata kwa hifadhi zake kutambuliwa na mfumo.