MAKALA YA MTANGAZAJI
NIMEKUTANA na kufanya mahojiano ya ana kwa ana na Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Athuman Mrisha kuhusu mwenendo wa shughuli za Bandari hiyo kwa sasa baada ya kufanyiwa maboresho makubwa na Serikali.
Pamoja na mambo mengine katika mahojiano hayo, nilimuhoji Mrisha kuhusu mipango ya sasa na ijayo ya uendelezaji wa bandari hiyo na matarajio yaliyopo kuhusu ufanisi wake kulingana na mipango ya Serikali ya uimarishaji na uendelezaji Bandari za Tanzania.
Nilikwenda Tanga kuona maboresho ya Bandari hiyo yaliyofanywa na Serikali chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), ili kuutangazia umma wa Watanzania na ulimwengu wote mabadiliko makubwa ya kiutendaji na pia uwezo wa vifaa na mitambo iliyopo sasa kwenye Bandari hiyo; kama ilivyoahidiwa na Serikali na sasa mawio yanachomoza bandarini hapo.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Athuman Mrisha
Nilipoingia ofisini kwa Mrisha kwa ajili ya mahojiano nilikuwa nimefumbata maswali nane ya kumuuliza lakini nilimuuliza maswali saba, moja nilibaki nalo kibindoni hadi mwaka 2025/26 wakati Bandari ya Tanga itakapokuwa ikihudumia shehena ya tani milioni tatu hadi tano kwa mwaka baada ya maboresho mengine yanayotarajiwa kufanyika mwaka huu, ndipo jibu la swali hilo litapatikana na kukata kiu ya Watanzania kuhusu Taifa letu kusonga mbele katika utoaji huduma bora za Bandari.
Nilimuuliza kwanza Mrisha kuhusu hali ya uboreshaji Bandari ya Tanga kivifaa, mitambo na upanuzi wa magati ipoje? naye anajibu;
‘Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), iliwekeza mradi wa kimkakati wa awamu mbili kwa jumla ya Shilingi bilioni 429.1 kwa miradi ya awamu mbili.
‘Tukianza na mradi wa awamu ya kwanza, ulianza tarehe 3 Agosti, 2019. Ulikuwa mradi wa mwaka mmoja ambapo TPA iliingia mkataba na Kampuni ya M/S China Harbour Engeneering Company Limited (CHEC) kwa maana ya maboresho ya Bandari ya Tanga.
‘Mradi huu ulikuwa wa mwaka mmoja na ulihusisha kuongeza kina cha maji katika Mlango Bahari, meli zinapoingia na zinapotoka. Kuongeza kina cha maji kutoka mita 3 mpaka 13. Zamani kina cha maji kilikuwa kimefikia mita 3, sasa kimetoka mita 3 hadi 13. Pia kuongeza upana wa Mlango Bahari kufikia mita 135.
‘Jambo jingine katika hiyo awamu ya kwanza ilikuwa kuongeza kina cha maji katika sehemu ya kugeuzi meli ili kuwa na kipenyo cha mita 800. Vile vile awamu ya kwanza ilijumuisha ununuzi wa vifaa au mitambo ya bandarini 16.

Moja ya meli kubwa ikiwa imetia nanga katika Bandari ya Tanga baada ya maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa kuongeza kina cha maji kutoka mita 3 hadi mita 13.
‘Nayo ni mitambo miwili inayofahamika kama diesel electrical operated mobile habour crane zenye uwezo wa kubeba tani 100 kila moja, forklift moja ya tani 16, forklift moja ya tani tano, bale clamp (folklift) mbili za tani tatu na front loader moja ya tani 50.
‘Pia empty conteiner handler moja ya tani 16, terminal tractor (TT) mbili, grab moja yenye uwezo wa kubeba tani 15 kwa wakati mmoja, rubber tyred gantry (RTG) moja ya tani 45, spreader mbili za futi 40 na spreader mbili za futi 20 kwa ajili ya kubebea kontena. Jumla ya mitambo hiyo ni 16. Thamani ya mradi wa awamu ya kwanza ilikuwa Shilingi bilioni 172.3.

Moja ya mtambo mpya wa kubeba makasha ulionunuliwa na Serikali kwa ajili ya kuboresha shughuli za upakuaji na upakiaji shehena ya mizigo katika Bandari ya Tanga.
‘Awamu ya pili ilihusisha kuboresha magati mawili yenye urefu wa mita 450. Magati hayo mawili, la kwanza lilijengwa mwaka 1914 lilikuwa na urefu wa mita 221 na gati la pili lilijengwa mwaka 1954 likiwa na urefu wa mita 229. Magati yote yalikuwa na urefu wa mita 450.
‘Lakini ukiangalia hapo awali, picha ya awali ilikuwa inaonekana kwamba hayako straight kwa hiyo upande wa Mashariki kuingia kwenye maji tulijenga kuingia ndani mita 50 na upande wa Magharibi kuingia kwenye maji tuliongeza mita 92 ili kuwa na gati lililonyooka. Meli zikifika ziweze kufunga mbili zenye urefu wa mita 220 kila moja.
‘Pia mkandarasi wa awamu ya pili alikuwa M/S China Harbour Engeneering Company Limited akisaidiwa na wahandisi washauri Kampuni ya NIRAS ya Dermark na mwingine mzawa Kampuni ya ANOVA.
‘Mradi huu wa awamu ya pili nao uligharimu Shilingi bilioni 256.8, hivyo jumla ya gharama ya miradi yote miwili ambayo Serikali imewekeza ni Shilingi bilioni 429.1. Hayo ndiyo maboresho ya awamu ya kwanza na ya pili yaliyofanyika kwenye Bandari ya Tanga na fedha zote zimetolewa na Serikali.’
Baada ya majibu hayo namuuliza Meneja Mrisho kuhusu mwenendo wa upokeaji na usafirishaji mizigo katika Bandari ya Tanga upoje baada ya kufanyiwa maboresho.
Anajibu kuwa mwenendo wa upokeaji wa mzigo kwa shehena kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia 2019/20 hadi 2023/24, kwanza ulikuwa ukikua taratibu lakini baada ya maboresho umekuwa kwa kasi.

Meli kubwa yenye makasha ikiwa nangani katika Bandari ya Tanga.
Hapo anaanza kutoa takwimu kwa kueleza kuwa ukuaji wa shehena umekuwa ukiongeza kwa asilimia 27.1 ambapo mwaka 2019/20 Bandari ya Tanga ilihudumia shehena, metric tone’s (MT) 470,611, mwaka uliofuata 2020/21 metric tone’s 637,182, mwaka 2021/22 metric tone’s 888,130, mwaka 2022/23 metric tone’s 890,901 na mwaka jana, ulioishia juni 30, 2024 metric tone’s 1,191,480.

Makasha yaliyokwishapakuliwa kutoka kwenye meli katika Bandari ya Tanga
Kwa maneno yake mwenyewe, anasema; ‘utaona ukuaji huo wote ni ukuaji wa asilimia 27.1. Ukiangalia mwaka 2019/20 na 2023/24 imekwenda juu mara tatu, mwaka 2019/20 tulipata 470,661 lakini mwaka jana ni 1,191,480. Hiyo ni mara tatu zaidi, kwa hiyo mwenendo wa upokeaji wa mizigo umekuwa wa kiwango kikubwa sana, mafanikio ni makubwa sana.’
Namuuliza pia Mrisha kuwa; Takwimu zikoje katika uhudumiaji wa makasha kwa muda wa miaka mitatu, naye anajibu kuwa; ili kutoa taarifa sahihi kwa umma atatoa takwimu za uhudumiaji makasha kwa miaka mitano, kuanzia 2019/20 hadi 2023/24.
Anasema; ‘Kuhusu kiwango cha makasha tulichohudumia katika Bandari ya Tanga, nitoe takwimu za miaka mitano ili kuelimisha jamii na watumiaji wa Bandari ya Tanga wajue mwenendo wa bandari yao. Ukuaji wake ni asilimia 0.8.
‘Hakikuwa kiwango kikubwa sana. Mwaka 2019/20 tulihudumia makasha (TEUs) 7,631 lakini mwaka jana 2023/24 tumehudumia makasha 7,817 kiwango hicho ni ukuaji wa asilimia 0.8.
‘Lakini nitoe mfano mzuri, mwezi julai, huu ambao tumeanza mwaka huu 2024/25 kuna makampuni sasa yamejitokeza. Kampuni ya MAERSK imeanza kuelekeza meli zake Bandari ya Tanga. Kuna meli yao moja kubwa, CONTSHIP ambayo sasa inaleta mzigo katika Bandari ya Tanga.
‘Mwezi huo mmoja tu, lengo ilikuwa kuhudumia makasha 577 lakini tumehudumia zaidi ya makasha 1300. Hii inaonyesha kwamba sasa tumeanza upya na huu ni mwelekeo mzuri katika upande wa kuhudumia makasha. Hiyo ni ishara nzuri, kama mwezi wa saba tu tumeweza kwenda mara mbili ya lengo tulilopangiwa katika kuhudumia makasha, maana yake tumevuka malengo mara mbili zaidi, zaidi asilimia 100.’
Anamalizia jibu lake huku akimwaga tabasamu la haja nami hapo hapo namuuliza swali la nne kuwa; maboresho yaliyofanyika yameipa uwezo gani Bandari ya Tanga wa kupokea meli kubwa.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Athuman Mrisha akitabasamu wakati wa mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog.
Anajibu; ‘Kabla ya maboresho haya, Bandari ya Tanga tulikuwa tunahudumia mzigo, kupakua na kupakia kilomita 1.7 kutoka gatini. Kwanini ilikuwa hivyo, ni kwa sababu ya kina kifupi, kama nilivyosema kina cha maji, kilikuwa ni mita tatu tu.
‘Kwa hiyo meli kubwa tulikuwa hatuwezi kuzihudumia, zilikuwa zinakaa kule kwenye kina kirefu tunatumia matishari kwa maana ya mzigo unapakuliwa kutoka kwenye meli unawekwa kwenye matishari, unakokotwa mpaka kwenye gati ndiyo unapakuliwa. Hiyo yote ilikuwa ni double handling. Unafanya kazi mara mbili mbili.
‘Ilikuwa inaongeza gharama kwa mteja na ilikuwa inaongeza gharama kwa mlaji pia kwa sababu kulikuwa na Dolla 1.3 ambayo inakwenda kwa mlaji kutokana na kufanya kazi mara mbili mbili. Na ilikuwa inatukosesha sisi kuhudumia meli kubwa.
‘Ukiangalia sasa, kwa mfano mwaka 2019/20 tulihudumia meli 118, mwaka 2020/21 tulihudumia meli 113, mwaka 2021/22 tulihudumia meli 198, mwaka 2022/23 tulihudumia meli 197, lakini mwaka jana baada ya maboresho haya kukamilika tumehudumia meli 307,’ hapo anatabasamu tena kisha anaendelea kujibu.
‘Kutoka mwaka juzi tumehudumia meli 197 lakini mwaka jana tukahudumia meli 307. Maana yake kuna ongezeko la meli 110, kwa hiyo kuna ongezeko kubwa la kuhudumia meli kubwa.

Meli kubwa ya mizigo ikiwa katika Bandari ya Tanga.
‘Katika hizo meli 307, meli 126 ni meli za deep sea, zinazotoka mataifa ya nje na meli 181 tulizohudumia ni za ndani ya Tanzania kwa maana ya majahazi yanayotoka hapa kwenda Zanzibar, Comoro na sehemu za karibu. Baada ya maboresho kufanyika tumeweza kuhudumia meli kubwa ambazo zamani zilikuwa haziwezi kuja hapa nangani.

Majahazi yanayohudumiwa katika Bandari ya Tanga
‘Vile vile, kwanini tumeweza kuhudumia meli kubwa, maana yake ni kwamba watu wamepata taarifa kwamba sasa mteja, mzigo wako unaweza kuhudumiwa moja kwa moja gatini. Ile mizigo ambayo watu walikuwa wanaogopa kuhudumiwa kule, wakiogopa labda kwamba wakati wa kupakia au kupakua ni risk, ile hatari imeondoka, ina maana sasa watu wameamua kuleta meli kubwa moja kwa moja zije zifanye kazi katika bandari yetu ya Tanga.
‘Kuna kampuni kama Sea Front sasa tunaihudumia hapa wakati hapo awali walikuwa hawawezi kuleta meli zao hapa na hawa Sea front wanaleta mizigo mchanganyiko wakati awali hatukuwa na meli za aina hiyo.
‘Maboresho haya yameleta manufaa makubwa katika bandari yetu. Kuna baadhi ya bidhaa zilikuwa hazijawahi kuhudumiwa katika Bandari ya Tanga, Copper kwa ajili ya export ilikuwa haijawahi kupita hapa kabla ya maboresho.
‘Sulphur, baada ya kufanyika maboresho tumehudumia meli 36 zilizobeba metric tone’s 330.173.61. Maboresho yameongeza shehena na mapato katika bandari yetu.’

Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Athuman Mrisha (aliyeketi kwenye kiti) waliosimama nyuma ni Mkuu wa Idara ya Masoko, Rose Tandika, Afisa Uhusiano, Bashiru Athuman, Afisa Habari Msaidizi, Fatuma Mwalimu na Mkuu wa Kitengo cha Mipango na Uwekezaji, Tumgonze Kabigumila
Swali lililofuata namuuliza hivi; ‘Mipango ya muda mrefu ya uboreshaji Bandari ya Tanga ni ipi?
Naye anaendelea kujibu; ‘Sasa mipango ya muda mrefu. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari wana mipango miwili au mitatu ya muda mrefu mikubwa katika mwaka huu wa 2024/25.
‘Kwanza kuongeza gati upande wa Mashariki mita 300, gati hili litakuwa ni container terminal, mahususi kwa ajili ya mzigo wa makasha tu.
‘Upande wa Magharibi tutaongeza mita 50 kwa ajili ya abiria, litakuwa gati la abiria. Kwa hiyo ukichukua zile 350 na zile 450 tutakuwa na gati linalofikia mita 800. Hapo mzigo utaongezeka.
‘Mwaka jana tumehudumia metric tone’s 1,191,480 lakini kwa maboresho yatayokuja tutaweza kufikia lengo la milioni tatu na hata milioni tano, tunaweza kufika huko baadaye.
‘Lakini vile vile kwenye huo ujenzi wa mita 300 wa container terminal utaendana na kununua mitambo maalumu kwa ajili ya kuhudumia makasha (SSG) itakuwa mitatu. Hizo SSG zina uwezo wa kuhudumia makasha 30 mpaka 36 kwa saa moja wakati hizi tulizonazo sasa, mobile habour crane kwa saa moja zinaweza kuhudumia makasha 15.
‘Kwa hiyo, mitambo mipya itakapokuja itaweza kwenda mara mbili na zaidi kwa saa moja tu, ni mitambo ya kisasa ambayo itahudumia shehena ya makasha.
‘Pia kuna ujenzi wa gati la mafuta kule eneo la Raskazone. Litajengwa kipindi hiki cha mwaka 2024/25. Miradi yote hiyo ya kimkakati kwa mwaka huu itakapokamilika tutaongeza shenena mpaka kufikia milioni tatu mpaka tano.’

Mwonekano wa Bandari ya Tanga miaka 1800
Majibu haya ya Mrisha yananifanya kuliweka kibindoni swali langu la sita mpaka mwaka 2025/26, namuuliza swali la mwisho; Meneja, Historia ya Bandari ya Tanga ipoje? Naomba wapitishe kidogo Watanzania na walimwengu kwenye historia ya Bandari ya Tanga.
‘Bandari ya Tanga ni Bandari kongwe Afrika Mashariki. Ilianza kujengwa na wakoloni wa kijerumani mwaka 1888 ikakamilika mwaka 1891, ilijengwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Wakati huo ilikuwa inajulikana kwa jina la marine jet.
‘Gati la kwanza lilijengwa 1914 likiwa na urefu wa mita 221 na gati la pili lenye urefu wa mita 229 lilijengwa mwaka 1954.
‘Bandari ya Tanga ilianzishwa kwa ajili ya kusafirisha bidhaa zinazotoka upande huu wa Mashariki kupeleka Nchi za Ulaya kwa ajili ya biashara zilizokuwa zikifanywa na wakoloni.
‘Ukubwa wa Bandari ya Tanga ni ekari 17 lakini tunayo maeneo mengine ambayo tunayamiliki, yako chini ya Bandari ya Tanga. Eneo la Mwambani liko umbali wa kilomita 6 kutoka hapa tulipo katika bandari yetu, lina ukubwa wa ekari 174 lakini tuna eneo Chongoleani, ni umbali wa kilomita 28 kutoka hapa tulipo, ni kule kwenye mradi wa Bomba la Mafuta, eneo hili lina ukubwa wa ekari 207.
‘Wenzetu wa East African Crude Oil Pipeline (EACOP)tumewapa ekari 76 katika eneo letu la Chongoleani kwa ajili ya mradi wa Bomba la Mafuta ambao ni mradi wa kitaifa. Kwa hiyo katika zile ekari 207, tumetoa ekari 76 kwa ajili ya mradi huo.
‘Tunazo pia andari ndogo ndogo ambazo zipo chini ya Bandari ya Tanga. Tunayo Bandari ya Pangani, Bandari ya Kipumbwi, Bandari ya Mkwaja na Bandari ya Sahare.
‘Bandari ya Pangani ilirasimishwa siku za nyuma lakini hizi tatu; Mei 6, 2022 ndiyo zilirasimishwa rasmi kuwa Bandari za kisheria zinazotumika katika Bandari ya Tanga.
‘Mazao na bidhaa tunayosafirisha ni pamoja na mkonge, kahawa, macadamia, copper, mazao ya misitu. Mazao na bidhaa tunayopokea ni pamoja na sulphur, mafuta ya petrol, dizel na mafuta ya ndege tumeanza kupokea hivi karibuni na malighafi kwa ajili ya utengezaji wa saruji na malighafi za viwandani.