MAKALA YA MTANGAZAJI
TANAPA Investiment Limited (TIL) ni jina geni kwenye orodha ya kampuni za uwekezaji na uzalishaji mali zinazomilikiwa na Mashirika ya Umma ambayo imefungua milango ya kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa gharama nafuu.
TIL pia imekuja kutoa huduma nje ya Shirika la TANAPA kwa kutekeleza miradi ya nje ya shirika hilo kibiashara na sasa inatazamwa kama moja ya vyombo muhimu vya utekelezaji wa miradi mikubwa ya Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma pamoja na Sekta Binafsi, ikizingatia thamani ya fedha ya miradi hiyo.
KUANZISHWA KWAKE
Kampuni hii ilianzishwa kwa agizo la Serikali ambayo iliiagiza TANAPA kuanzisha kampuni yake ya uwekezaji baada ya kuridhika kuwepo kwa vigezo vyote muhimu ndani ya Shirika wakiwemo watendaji wabobezi, wenye elimu ya juu na uwezo mkubwa wa kutekeleza kazi za kihandisi, mitambo ya kutosha na vilevile uwezo wa kifedha.
Serikali ilizingatia kuwepo kwa watumishi ndani ya TANAPA wenye uwezo na ujuzi mkubwa usiokuwa wa kutiliwa shaka kiuhandisi na waliosajiliwa na Bodi ya Wahandisi; ndipo Disemba 31, 2019 ilielekeza Shirika hilo kuanzisha kampuni tanzu ya uwekezaji kwa ajili ya kutekeleza miradi yake ya maendeleo ndani na nje ya Shirika.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mhandisi Mshauri, Dkt. Richard John Matolo.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mhandisi Mshauri, Dkt. Richard John Matolo alishiriki kwa kiasi kikubwa kwenye uanzishaji wa kampuni hiyo tanzu ambapo TANAPA lilikamilisha usajili wake mwishoni mwa mwaka 2023 na kuanza rasmi kufanya kazi zake mwanzoni mwa mwaka huu wa 2024.
Akielezea mwenendo wa kampuni hiyo, Dkt. Matolo anasema ilianza kutekeleza majukumu yake ikizingatia maelekezo ya Serikali kuwa badala ya kuendelea kutumia wakandarasi na washauri majenzi wa nje ya Shirika ambao kwa muda wa takribani miaka 65 wamekuwa wakitumiwa na TANAPA, jukumu hilo sasa libebwe na TIL.
Dkt. Matolo anasema msingi wa maelekezo hayo ya Serikali ni kuwepo kwa changamoto nyingi katika utekelezaji wa miradi ya shirika kwa muda mrefu na anataja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na gharama kubwa za majenzi zinazotozwa na wakandarasi, kutokamilisha kazi kwa wakati, kukosa umakini na weledi unaotakiwa kwa baadhi ya wakandarasi na pia kukosa umakini kwenye utunzaji wa mazingira ndani ya maeneo ya hifadhi.
Anasema kutokamilisha kazi kwa wakati kumesababisha kuwepo kwa migogoro ambayo imekuwa ikiilazimu TANAPA kusitisha baadhi ya mikataba ya wakandarasi na hivyo Shirika kuchukua jukumu la kukakamilisha miradi inayoachwa na wakandarsi hao kwa kutumia nyenzo na rasilimali zake za ndani.
Dkt. Matolo anasema Serikali ilizingatia mambo mengi baada ya kubainika kuwa; kwa muda mrefu Shirika lilikuwa halipati thamani ya fedha iliyokusudiwa kwenye utekelezaji wa miradi yake na ndipo ilielekeza TANAPA kubadili mwelekeo na kukabiliana na changanoto hizo kwa kutumia chombo chake ambacho ni TIL.
Greda la Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lililo chini ya Kampuni ya TANAPA Investiment Limited (TIL) likisafisha eneo la kuchonga barabara.
Na kwamba, kwa kutumia kampuni yake ya TIL, Serikali iliielekeza TANAPA itekeleze miradi yake yenyewe na kwa gharama nafuu kuliko ilivyokuwa ikitekelezwa na wakandarasi wa nje ya Shirika, kuikamilisha kwa wakati, kuzingatia athari za mazingira vizuri zaidi na kupata thamani bora zaidi ya shilingi katika utekelezaji wa miradi ya Shirika.
Agizo jingine la Serikali lilikuwa ni kwa TANAPA kutumia kampuni yake ya TIL kama kitega uchumi kwa kutekeleza miradi ya nje ya Shirika kama inavyofanywa na Kampuni ya Uzalishaji Mali ya Jeshi la Kujenga Taifa, (SUMA JKT).
Msingi wa agizo hilo la Serikali ni kulifanya TANAPA kuwa na njia mbadala ya kupata mapato badala ya kuendelea kutegemea utalii peke yake ambao ulionyesha changamoto kubwa sana wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19.
Dkt. Matolo anasema wakati wa mlipuko wa UVIKO 19 hakukuwa na mgeni wa nje hata mmoja kwenye Hifadhi za Taifa hivyo hakukuwa na fedha zozote za kigeni zilizokuwa zinaingia. Kuanzishwa kwa TIL kulionekana kama njia mbadala ya kulisaidia Shirika kuingiza fedha inapotokea mtikisiko na changamoto kwenye biashara ya utalii kama ilivyokuwa wakati wa UVIKO-19.
UWEZO, MTAJI WA TIL
Dkt. Matolo anasema wadau wakubwa wa TIL ni Serikali, Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s), Taasisi na Mashirika ya Umma, Taasisi za Kidini, Sekta binafsi n.k.
Baadhi ya vifaa vya kisasa vya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) vinavyotumiwa na Kampuni ya TANAPA Investiment Limited (TIL) kwa shughuli za majenzi.
Kwamba, TANAPA likiwa na watumishi wabobezi na wenye elimu ya juu na ujuzi usiokuwa wa kutiliwa shaka kiuhandisi, lilikidhi vigezo vyote vya kusajiliwa na kupewa cheti cha usajili daraja la kwanza kwenye eneo la ujenzi wa miundombinu ya majengo (Building category), barabara (Civil category) na ushauri majenzi (Consultancy category).
Anasema hisa zote za TIL ni za TANAPA. Mtaji wa TIL utatokana na bajeti ya miradi ya maendeleo ya kila hifadhi kwa mwaka wa fedha husika na iliyoidhinishwa na Serikali na inatekelezwa kwa kutumia mikataba nafuu ya ndani ya Shirika.
UTEKELEZAJI MIRADI
Dkt. Matolo anasema tangu TIL ilipoanza kufanya kazi imekwishateleza miradi ya ndani ya Shirika na ya nje kwa ufanisi mkubwa kama ilivyoelekezwa na Serikali.
Anaitaja miradi hiyo akianza na mradi wa ndani ya Shirika ambao ni ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 16 katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha inayounganisha Lango la Ngongongare hadi Lango la Nasula.
Greda la Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) linalotumiwa na Kampuni ya TANAPA Investiment Limited (TIL) kufanya shughuli za majenzi likichonga barabara.
Kwa upande wa miradi ya nje ya shirika, Dkt. Matolo anasema TIL imeishatekeleza ujenzi wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) zenye urefu wa takriban kilomita 23 zilizopo katika Jiji la Arusha.
Dkt. Matolo anazitaja barabara hizo kuwa ni pamoja na ile inayoanzia Mateves – Olmoti yenye urefu wa kilomita 9.0 na barabara nyinginezo katika eneo la Mateves zenye urefu wa kilomita 1.7.
Anataja pia barabara zinazoanzia Kibanda cha Maziwa hadi Shamsi yenye urefu wa kilomita 1.7, Barabara ya Dk. Msemo yenye urefu wa kilomita 2.0, Barabara ya Kijenga Juu hadi Ngulelo yenye urefu wa kilomita 1.2, Barabara ya Bomasiara hadi Redio Wave Junction yenye urefu wa kilomita 1.7, Barabara ya Moshono hadi kwa Mrefu yenye urefu wa kilomita 2.3 na ile ya Relini hadi Kambi ya Chupa yenye urefu wa kilomita 3.5.
Dkt. Matolo anasema utekelezaji mzuri wa miradi hiyo umeifanya TARURA kuiongozea TIL kazi mbili za dharura ambazo zipo mbioni kuanza utekelezaji wake na kwamba, TIL ina wataalamu wa kutosha, wabobezi na wenye ujuzi wa hali ya juu wa kihandisi na pia; inayo mitambo ya kisasa na uwezo wa kutekeleza mradi wowote mkubwa wa ujenzi kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha.