Monday, December 23, 2024
spot_img

MAENDELEO YA WATU, HUJUMA NA UHALIFU, UHABA WA DOLA MWIBA KWA MALENGO YA WIZARA YA NISHATI 2023/24

MAKALA MAALUMU

UZALISHAJI wa umeme na gesi asilia kwa mwaka 2023/24 haukuendana na mahitaji yaliyopo nchini kwa sababu ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii pamoja na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme.

Sambamba na hilo, changamoto nyingine iliyosababisha kutofikiwa kwa malengo ya uzalishaji umeme na gesi asilia kwa mwaka huo ni vitendo vya hujuma na uhalifu kwenye miundombinu ya umeme.

Na aidha; uhaba wa Dola za Marekani ambazo hutumika kulipia mafuta yanayoagizwa nje ya nchi ni changamoto nyingine iliyokwamisha kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa kwani wafanyabiashara walipunguza kiasi cha mafuta walichokuwa wakiagiza.

Hizi ndizo changamoto tatu kubwa zilizobainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko kuikabili wazira yake katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka 2023/24, alipokuwa akiwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/25.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Dotto Biteko akiwasilisha hotuba ya wizara yake bungen.

Dk. Biteko anasema katika hotuba yake hiyo kuwa; Serikali ilikabiliana na changamoto hizo zote, kwanza kwa kuwachukulia hatua za kisheria waliobainika kutekeleza vitendo vya kihalifu na uharibifu kwenye miundombinu ya umeme.

Pili ni kuharakisha utekelezaji wa miradi ya uzalishaji wa umeme pamoja na kukarabati na kufanya matengenezo ya miundombinu ya umeme.

Na hapo alionya kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kufanya vitendo vya hujuma na au uhalifu katika miundombinu ya umeme, kunakosababisha hasara na usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa umeme.

Tatizo la uhaba wa Dola za Marekani nalo lilishughulikiwa na Serikali na hapa Dk. Biteko anasema Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wadau wengine walishirikiana kufanya mapitio ya mikataba ya kuagiza mafuta na kuruhusu kutumika kwa fedha ya Uingereza (British Pound), Umoja wa Ulaya (Euro) na Umoja wa Nchi za Uarabuni (Dirham).

Aidha, Wizara ya Nishati kupitia EWURA iliimarisha ukaguzi katika vituo vya mafuta ili kuhakikisha mafuta yanapatikana wakati wote katika maeneo yote nchini.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akihutubia mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya TabniaNchi (COP 28)

Nje ya changamoto hizo, Dk Biteko anasema kwenye hotuba yake kuwa kutokana na athari za matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia hususan uharibifu wa mazingira, kiuchumi na kijamii na za kiafya, Serikali iliendelea kutekeleza mikakati mahususi ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Anasema Serikali iliidhinisha mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024 – 2034, unaolenga angalau asilimia 80 ya Watanzania kuwa wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Dk. Biteko anasema malengo ya mkakati huu ambao unabainisha majukumu ya wadau ni pamoja na kupunguza gharama za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia; kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uhakika ya nishati safi ya kupikia, kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi ya kupikia na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kwamba kwa kushirikiana na wadau, wizara iliratibu na kushiriki mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) uliofanyika Dubai mwezi Novemba hadi Disemba, 2023.

“Kwenye mkutano huo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alizindua programu ya nishati safi ya kupikia itakayowawezesha wanawake barani Afrika (African Women Clean Cooking Support Programme-AWCCSP) kutumia nishati safi ya kupikia,” anasema.

Anaeleza pia kuhusu mkutano wa wakuu wa nchi kuhusu nishati safi ya kupikia barani Afrika uliofanyika Mei, 2024 jijini Paris, Ufaransa ambapo Rais Dk. Samia alikuwa Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo kwa kushirikiana na Waziri Mkuu wa Norway, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Nishati Duniani (International Energy Agency-IEA) na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Rais Samia Suluhu Hassan akipokelewa na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alipokwenda nchini humo kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi kuhusu nishati safi ya kupikia barani Afrika.

Dl. Biteko anasema mkutano huo pamoja na mambo mengine ulijadili na kuweka mikakati ya namna ya kuimarisha sera, ugharamiaji na ushirikiano katika kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika.

“Hatua nyingine zilizochukuliwa na wizara kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ni kusambaza mitungi ya gesi ya LPG, gesi asilia na majiko bunifu, kutekeleza program mbalimbali za kuhamisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na kuendesha kongamano la wanawake la nishati safi ya kupikia lililofanyika mkoani Dodoma Machi 9, 2024.

“Pia kushirikiana na Jeshi la Magereza ili kuwezesha jeshi hilo, kambi za makazi ya watumishi, ofisi, vyuo, shule na hospitali kutumia nishati safi ya kupikia,” anasema Dk. Biteko.

Sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nayo ilikuwa sehemu ya hotuba ya Dk. Biteko anayoieleza kuwa mwaka 2023/24, Serikali iliendelea kuchukua hatua za kuendeleza sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia katika maeneo ya utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta na gesi.

Anasema utekelezaji wa hatua hizo ulizingatia majadiliano ya mikataba ya utekelezaji wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) ili kuboresha rasimu za awali za mikataba hiyo kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na wadau ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi nyingine za Serikali.

Anasema shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya kimkakati vya Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi – Wembere, Songo Songo Magharibi na vitalu namba 4/1B na 4/1C ziliendelea.

Aidha, Serikali iliridhia kutolewa kwa leseni ya uendelezaji wa gesi asilia iliyogunduliwa katika eneo la Ntorya katika kitalu cha Ruvuma kwa TPDC kwa niaba ya mwekezaji ambaye ni Kampuni ya ARA Petroleum.

“Uendelezaji wa gesi iliyogunduliwa Ntorya unatarajiwa kuiwezesha nchi kupata gesi ya takribani futi za ujazo milioni 60 kwa siku katika kipindi cha awali cha miaka miwili na kuongezeka hadi kufikia uzalishaji wa futi za ujazo milioni 140 kwa siku baada ya kipindi hicho na hivyo kuimarisha upatikanaji wa gesi asilia nchini,” alisema.

Katika mlolongo wa hatua hizo, pia kuna ununuzi wa asilimia 20 ya hisa za Kampuni ya Wentworth kwenye mkataba wa uendeshaji wa kitalu cha uzalishaji gesi asilia cha Mnazi Bay kilichopo Mtwara. Hisa hizo zilinunuliwa na TPDC.

“Miradi ya usambazaji wa gesi asilia viwandani, taasisi na majumbani iliendelea kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.

“Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kujenga bomba la gesi asilia lenye urefu wa kilometa 12.4 kutoka Mwenge hadi Mbezi Beach Dar es Salaam lililounganishwa kwa miundombinu ya gesi asilia kwenye viwanda na hoteli mbalimbali na kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka BVS kuelekea Kata za Mnazi Mmoja na Mingoyo mkoani Lindi lenye urefu wa kilomita 10.04 lililounganisha nyumba 209 na gesi asilia.

Mitambo ya uzalishaji gesi iliyopo Mtwara

“Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kukamilisha taratibu za kumpata mkandarasi wa kujenga miundombinu ya kuunganisha nyumba 451 mkoani Lindi katika Kata za Mnazi Mmoja na Mingoyo na nyumba 529 mkoani Pwani eneo la Mkuranga,” alisema.

Anaendelea kwa kueleza kuwa ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia (Compressed Natural Gas-CNG) katika magari uliendelea kwa kushirikisha pia sekta ninafsi.

Kwamba TPDC na GPSA ziliendelea na taratibu za kumpata mshauri mwelekezi wa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa michoro ya kihandisi na yathmini ya athari ya mazingira na jamii ili kuwezesha GPSA kujenga vituo vya CNG katika Bohari za Dar es Salaam na Dodoma ili vyombo vya moto vinavyomilikiwa na Serikali kutumia CNG vitumike.

Dk. Biteko anasema sekta binafsi iliendelea kutumia fursa ya matumizi ya CNG katika vyombo vya moto kwa kujenga vituo vya CNG katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, pamoja na karakana nane za kubadilisha mifumo ya matumizi ya CNG kwenye magari ambayo ni nyenzo muhimu ya kuchochea matumizi ya CNG katika magari.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya