Saturday, April 19, 2025
spot_img

DK. BITEKO ASHUKURU WAFADHILI MRADI WA TAZA

TERESIA MHAGAMA

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko amewashukuru wafadhili wa mradi wa ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme wa msongo wa kilovoti 400 wa TAZA.

Wafadhili hao ni Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Ufaransa
(AFD) na Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) ambao wametoa zaidi ya
Shilingi trilioni moja za kutekeleza mradi huo unaohusisha ujenzi wa vituo vitano vya kupoza umeme.

Shukrani hizo alizitoa mwishoni mwa mwezi uliopita alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo huko Sumbawanga mkoani Rukwa.

Alisema Serikali inawajali wafadhili wanaosaidia ujenzi wa miradi ya aina hiyo ambayo inawezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

Dk. Biteko alisema Serikali itaendelea kuipa kipaumbele ajenda hiyo na tayari imeshaanzisha kitengo cha kushughulikia nishati safi ya kupikia ndani ya Wizara ya Nishati.

Dk. Biteko alisema Benki ya Dunia imeahidi kuiwezesha Serikali kutekeleza ajenda hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere ambaye alihudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi wa ujenzi wa mradi za TAZA alisema utakapokamilika, mkoa huo utapata umeme wa uhakika.

Alisema tayari vijiji 308 vina umeme katika mkoa huo na 31 vilivyobaki kazi inaendelea.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema mradi wa TAZA ni wa kipekee kwa sababu utawezesha Afrika kuunganishwa na umeme kutoka Afrika Kusini hadi Ethiopia.

Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mathew Mkingule aliipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa umeme wa TAZA.

Alisema mradi huo utatoa uhakika wa  usalama wa nishati katika nchi za Kusini mwa Afrika, kukuza uchumi Mkoa wa Rukwa, kuwezesha biashara ya umeme,
fursa ya ajira na kulinda mazingira kwani nishati ya umeme inawezesha
wananchi kutumia nishati hiyo kupikia.

Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete aliyezungumza kwa niaba ya wawekezaji wa mradi alimpongeza Dk. Biteko na Serikali kwa miongozo iliyowezesha mradi wa TAZA kuanza kutekelezwa.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alisema mradi wa TAZA ni sehemu ya maazimio yaliyofanyika
Disemba 15, 2014 baina ya Nchi za Tanzania, Kenya na Zambia ya
kuunganisha gridi za nchi hizo tatu.

Katika utekelezaji wa makubaliano hayo, alisema Tanzania ilianza kujenga laini ya umeme ya kV 400 ya km 670 kutoka Dodoma hadi Shinyanga ambayo ilishakamilika na baadaye  kujenga laini ya kV 400 kutoka Singida hadi Namanga kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya ambao umekamilika kwa asilimia 99.8 na kipande cha tatu ni  cha mradi wa
TAZA ambacho kinatekelezwa sasa ili kuunganisha gridi ya Tanzania na
Zambia.

Alisema mradi umeshaanza na umefikia asilimia 29.8 huku ukitarajiwa kukamilika Mei, 2026.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio, wenyeviti na makamu wenyeviti wa kamati mbalimbali za Bunge, Mwakilishi wa AU, AFD, Katibu Mtendaji wa EAPP, Bodi na Wakurugenzi wa taasisi chini ya wizara, Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na watendaji kutoka Shirika la Umeme la Zambia (ZESCO).



Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya