Monday, December 23, 2024
spot_img

E-MAIL YA KIGWANGALLA NA RASIMU YA MKATABA WA KIBALI CHA TANI 25,000 ZA SUKARI

RIPOTA PANORAMA

KUNA sintofahamu kuhusu uhusika wa Mbunge wa Nzega Vijijini, Hamisi Kigwangalla kwenye mipango ya kuwatafutia wafanyabiashara vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi kutoka Bodi ya Sukari kwa makubaliano ya kimkataba ya kulipwa mabilioni ya fedha.

Sintofahamu hii inatokana na kupatikana kwa rasimu ya mkataba wa kutafuta bila kukosa kibali cha kuagiza nje ya nchi, tani 25,000 za sukari kutoka Bodi ya Sukari; rasimu ambayo iliandaliwa na mwanasheria (jina lake kapuni) kisha akamtumia Kigwangalla kwa barua pepe.

Rasimu ya mkataba wa kusaka kibali cha kuagiza sukari nje ya nchi kutoka Bodi ya Sukari iliyotumwa kwenye chemba ya barua pepe ya Kigwangalla ina vipengele 10.

Rasimu hiyo ilitumwa kwa Kigwangalla Julai 31, 2023 saa 1.46 jioni  ikiwa imeambatanishwa na maneno yanayosomeka hivi; ‘Hello Dr/ Comrade/ Mheshimiwa, please kindly receive a draft of service Agreement as per earlier communique for your perusal and comment.’

Siku hiyo hiyo, majira ya saa 3 usiku, Kigwangalla anaonekana kujibu barua pepe hiyo kwa kuandika; ‘well received, thanks. Nakutumia details ili uprint.’

Sukari.

Kigwangalla ameulizwa na Tanzania PANORAMA Blog na kukiri kuwa barua pepe iliyotumika kwa mawasiliano hayo ni ya kwake lakini alikataa kuitambua rasimu ya mkataba wa kusaka kibali hicho kabla hajaiona ili ajiridhishe.

Rasimu ya mkataba wa kusaka kibali cha kuagiza sukari nje iliyo kwenye mawasiliano ya barua pepe ya Kigwangalla inawataja wahusika kama mtoa huduma na mshauri elekezi pasipo kutaja majina yao wala kampuni inayotafutiwa kibali hicho.

Kigwangalla ameonyeshwa rasimu ya mkataba huo aliyotumiwa Julai 31, 2023 na kuulizwa maswali matano ambayo hadi sasa ameshindwa kuyajibu na aidha, licha ya kuonyeshwa rasimu hiyo kama alivyotaka ili kujiridhisha kabla ya kujibu, hadi sasa ameshindwa kukiri wala kukanusha kuifahamu.

Baadhi ya maswali ambayo Tanzania PANORAMA Blog imemuuliza Kigwangalla ni kazi ya kutafutia wafanyabiashara vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi ameifanya kwa muda gani na hadi kuonwa kwa rasimu ya mkataba wa kutafutia wafanyabiashara kibali cha kuagiza sukari ikiwa kwenye mawasiliano yake, ameishawatafutia wangapi vibali hivyo kutoka Bodi ya Sukari.

Ameulizwa pia malipo ya mabilioni ya fedha yanayolipwa kwa kazi hiyo kama yanakatwa kodi na iwapo kazi ya kutafutia wafanyabiashra vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi haikinzani na sheria na maadili ya viongozi wa umma. Maswali haya, Kigwangalla ameshindwa kuyajibu hadi sasa.

Rasimu ya mkataba imeandikwa kwa Lugha ya Kiingereza; kwa tafsiri isiyo rasmi ya Lugha ya Kiswahili inaanza kwa kusomeka; ‘mkataba wa huduma.

Inasomeka kuwa mkataba huo umefanyika mwezi Julai mwaka 2023, wahusika wakiwa mshauri mwelekezi na mtoa huduma, ambao rasimu hiyo haiwataji majina yao.

Baadhi ya vipengele vya rasimu ya mkataba huo; vinasomeka hivi; ‘ambapo pande zote kwenye mkataba huu zimekubaliana kimsingi ya kwamba, ikiwa mtoa huduma amemuhakikishia na kumthibitishia mshauri elekezi kuwa ana uwezo wa kupata kibali cha kuagiza sukari kutoka nje kwa ajili ya mteja wa mshauri elekezi kutoka kwenye Bodi ya Sukari na ya kwamba mshauri elekezi anatamani kutumia huduma ya mtoa huduma kwa makubaliano yafuatayo.

‘Kwamba mtoa huduma atatafuta na kumpa kibali cha kuagiza sukari kutoka kwa Bodi ya Sukari Tanzania kwa ajili ya mteja wa mshauri elekezi bila kushindwa kwa ajili ya kuagiza tani za kimetriki 25,000 kuja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‘Kwamba mtoa huduma atalipwa ujira wa Shilingi za kitanzania 125 kwa kila kilo moja ya mzigo wote wa tani za kimetriki 25,000 na kwamba mshauri elekezi atamlipa mtoa huduma asilimia 50 ya jumla ya malipo yote baada ya kukabidhi kwa mshauri elekezi, ‘control number’ ya malipo na kiasi kinachobakia cha asilimia 50 atalipwa baada ya siku 14 za kulipia kibali cha kuagiza sukari.

‘Makubaliano haya yataanza kuanzia …. Mwezi ….. mwaka 2023 na utakoma baada ya pande zote kumaliza wajibu wao uliotajwa kwenye mkataba huu.

‘Pande zote kwenye makubaliano haya hawatakiwi kutoa maudhui ya mkataba huu au maelezo ya kina ambayo yanaweza kuathiri utekelezaji wa mkataba huu na kuleta mgongano wa maslahi.

‘Pande zote zinatakiwa kutimiza masharti ya mkataba huu kikamilifu kwa malengo ya kufanikisha lengo linalotarajiwa.

‘Notisi zote kati ya pande zote zitakabidhiwa kwa maandishi kwa njia ya kukabidhiana, barua pepe, fax au barua iliyothibitishwa. Notisi zote zitakuwa tayari kushughulikiwa baada ya kupokelewa au siku saba baada ya kutumwa kwa chochote kitakachotokea kwanza.

‘Pande zote hazitawajibika chini ya mkataba huu kama utekelezaji utazuiwa kutokana na tukio ambalo wahusika wa mkataba huu hawakulitarajia na lipo nje ya udhibiti wao. Matukio hayo yatahusisha lakini siyo kwa ukomo wa majanga ya asili, mioto, vita, maandamano, migomo, kufungiwa, usumbufu wa kikazi na matendo ya Mungu.’

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina.

Kwa mujibu wa rasimu ya mkataba huu, mtoa huduma ambaye ana wajibu wa kutafuta kibali cha kuagiza sukari nje ya nchi bila kushindwa kutoka Bodi ya Sukari analipwa Shilingi 3,125,000,000.

Fedha hizi analipwa kwa mikupuo miwili, mkupuo wa kwanza analipwa Shilingi 1,562,500,000 anapofanikisha kupatikana kwa ‘control number’ ya kulipia kibali na mkupuo wa pili analipwa baada ya wiki mbili za kulipia kibali.  

Kupatikana kwa rasimu hii ya mkataba baina ya mawakala wa wafanyabiashara wanaosaka vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi na watu wanaoonekana kuwa na ushawishi na au waliopata kushika nyadhifa za juu serikalini kunafichuka sasa ikiwa ni siku chache baada ya skandali ya ukiukwaji wa utoaji vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi kulitikisa Bunge.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina alimtuhumu bungeni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwa kusema uongo kuhusu nakisi ya sukari nchini wakati wa uhaba wa bidhaa hiyo na pamoja na mambo mengine; ukiukwaji wa taratibu za utoaji vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alimtaka Mpina kuthibitisha tuhuma zake dhidi ya Bashe, jambo ambalo Mpina alilitimiza, kisha akaongea na waandishi wa habari.

Baada ya Mpina kuongea na waandishi wa habari, Spika Tulia aliliambia Bunge kuwa huko ni kumkosea yeye kama Spika na Bunge kwa ujumla kisha alimpeleka kuhojiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ambayo iliwasilisha taarifa yake bungeni ikithibitisha kauli ya Tulia dhidi ya Mpina ambaye aliadhibiwa kutohudhuria vikao 15 vya Bunge.

Kabla ya kupitishwa kwa adhabu hiyo, Spika Tulia aliwapa fursa wabunge kujadili taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ambapo wabunge waliopewa nafasi ya kuzungumza akiwemo Kigwangalla walimshambulia Mpina.

Baada ya kuadhibiwa bungeni, Mpina alizungumza tena na waandishi wa habari akieleza kutotendewa haki na Tulia na nia yake ya kumshtaki mahakamani pamoja na Waziri Bashe na tayari zaidi ya mawakili 10 wamekwishajitokeza kumuwakilisha kwenye kesi hiyo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya