Monday, December 23, 2024
spot_img

MWELEKEO WA UTEKELEZAJI SHUGHULI ZA TPA BAJETI YA 2024/2025

MAKALA MAALUMU

MWELEKEO wa Utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 umejikita kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020.

Ibara ya 59b(i-vi) katika Ilani ya uchaguzi ya CCM inaelekeza uboreshaji na uimarishaji wa miundombinu na utoaji wa huduma bora za Bandari.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa katika hotuba yake ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa 2024/2025 anaeleza kuwa katika kufanyia kazi maelekezo hayo, TPA imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na uboreshaji Bandari za Ukanda wa Mwambao wa Bahari ya Hindi, Maziwa Makuu na Bandari Kavu.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Anasema TPA inaendelea kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kufungua ofisi nje ya nchi, kutafuta masoko na kununua vifaa na mitambo kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma za Bandari nchini.

Profesa Mbarawa anasema Ofisi za TPA zilizo nje ya nchi zimeendelea kutafuta masoko, kujitangaza na kutafuta fursa zaidi za kibiashara kwa nchi jirani zinazotumia Bandari za Tanzania.

Anazitaja nchi hizo kuwa ni Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zimbabwe.

Anasema jitihada zilizofanywa na TPA zimewezesha shehena ya mizigo iliyosafirishwa kwenda nchi jirani kuongezeka hadi kufikia tani 8,871,438 kwa mwaka 2023 kutoka tani 8,239,112 kwa mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 7.67. 82.

Anazungumzia pia mpango wa TPA kuratibu ununuzi wa vifaa na mitambo kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za Bandari nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) Plasduce Mbossa

Anasema hadi Machi 2024, TPA imenunua na kupokea vifaa na mitambo 121, sawa na asilimia 53.78 ya lengo la kununua mitambo na vifaa 225 na kwamba ununuzi wa mitambo hiyo umeongeza ufanisi wa utoaji huduma bandarini.

Kwa watumishi, waziri huyo anasema 2,749 kati 2,288 waliopagwa kuhudhuria mafunzo, walihudhuria kama ilivyokusudiwa na Serikali kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa TPA.

Idadi hiyo ya watumishi waliohudhuria mafunzo ni sawa na asilimia 83.23 ya lengo ambapo 1,646 walishiriki mafunzo ya vikundi, 486 walishiriki mafunzo ya kitaaluma (professional), 57 walishiriki mafunzo ya muda mfupi kwa mtu mmoja mmoja na 99 walishiriki mafunzo ya muda mrefu.

Profesa Mbarawa anaeleza katika hotuba yake kuwa TPA imeendelea kusimamia Bandari za Mwambao wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu kwa kuendeleza miundombinu na utoaji wa huduma za kibandari na kuweka taratibu na viwango kwa watoa huduma za Bandari.

Anasema, pia TPA imeendelea kusimamia na kudhibiti huduma za Bandari, kulinda mazingira na usalama wa Bandari kwa viwango vinavyokubalika na kuweka mazingira mazuri yanayovutia uwekezaji katika Sekta ya Bandari.

Kwamba TPA imeendelea kutangaza Bandari kimasoko kwa kushirikisha Sekta Binafsi katika uendeshaji wa shughuli za kibandari.

Kuhusu huduma za TPA, Profesa Mbarawa anasema Julai, 2023 hadi Machi, 2024 TPA ilihudumia tani milioni 20.72 ya shehena ikilinganishwa na tani milioni 14.56 ya shehena ya mizigo iliyohudumiwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 42.31.

Kwa upande wa uhudumiaji makasha,  anasema TPA ilihudumia makasha 805,167 ikilinganishwa na makasha 688,609 yaliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 16.92.

Makasha ya mizigo

Anasema ongezeko hilo la shehena ya mizigo na makasha limetokana na mikakati mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na TPA ikiwamo uboreshaji wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Kuhusu uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Profesa Mbarawa anasema TPA imeendelea na kazi ya kuchimba urefu wa kina ambacho sasa kimefikia mita 15.5 na upanuzi wa lango la kuingia na kugeuzia meli ambalo upana wake umefikia mita 200.

Kwa sasa, Bandari ina uwezo wa kupokea meli kubwa zenye urefu wa mita 305 lakini pia upembuzi yakinifu wa kuboresha gati namba 8 – 11 na ujenzi wa gati namba 12 – 15 bado unaendelea kwa ajili ya kuhudumia meli na shehena.

Mkurugenzi Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho

Anabainisha katika hotuba yake kuwa mkataba wa kuendeleza miundombinu ya kupokelea mafuta (Single Receiving Terminal – SRT) unaohusisha ujenzi wa matenki 15 ya mafuta (tank farms) pamoja na miundombinu yake yenye uwezo wa kuhifadhi kiasi cha mita za ujazo 420,000 umesainiwa Februari 26, 2024 na maandalizi ya kuanza ujenzi yanaendelea.  

Kuhusu uboreshaji wa Bandari ya Tanga awamu ya pili anasema umekamilika kwa asilimia 100 na anataja kazi zilizofanyika ni kuboresha magati mawili yenye urefu wa mita 450, uboreshaji wa eneo la kuhifadhia makasha lenye ukubwa wa mita za mraba 6,400 na uwezo wa kuhudumia makasha 1,020 TEUs.

Nyingine ni ununuzi wa jumla ya mitambo 16 ambayo ni Forklift (4), Crane (3), Container spreaders (4), Terminal Tractors (2) Front end loader (1), Empty handlers stacking (1) na Grabs (1) kwa ajili ya kuhudumia shehena.

Anasema TPA imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuhudumia shehena ya mzigo mchafu (dirty cargo) kama vile makaa ya mawe na saruji.

Kazi ya upembuzi yakinifu imekamilika mwezi Februari, 2024 na sasa taratibu za ununuzi wa mkandarasi na mhandisi mshauri wa ujenzi zinaendelea.

Anataja lengo la utekelezaji wa mradi huo kuwa ni kuiwezesha Bandari ya Mtwara kutoa huduma kwa ufanisi katika mizigo mingine tofauti na mizigo michafu.

Kuhusu Bandari ya Bagamoyo anasema Serikali imekamilisha ulipaji fidia kwa wananchi wanaopisha eneo la mradi lenye ukubwa wa hekta 887 na hivi sasa mradi huo upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa kuhuisha upembuzi yakinifu.

Mwonekano wa Bandari ya Tanga

Ujenzi wa Bandari hiyo ni wa kimkakati kwa kuwa itachochea shughuli za viwanda na biashara katika eneo la Ukanda Maalumu wa Kiuchumi (Special Economic Zone).

Ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa kilomita 15.5 kutoka Barabara Kuu ya Morogoro hadi Bandari Kavu ya Kwala umekamilika na ujenzi wa yadi ya sakafu ngumu (pavement) yenye ukubwa wa hekta tano (5) kwa ajili ya kuhifadhi shehena unaendelea na utekelezaji wake umefikia asilimia 96.

Bandari Kavu hii imeanza kutoa huduma za kibandari kwa kutoa makasha kutoka Bandari ya Dar es Salaam na kwenda Kwala kwa njia ya reli.  

Pia anasema TPA imeendelea kuboresha Bandari zilizopo Ziwa Victoria ambapo uboreshaji wa Bandari ya Bukoba umefikia asilimia 47 na Bandari ya Kemondo umefikia asilimia 52.

Uboreshaji wa Bandari ya Mwanza North umefikia asilimia 40 na uboreshaji wa Bandari ya Mwanza South utaanza baada ya kukamilika kwa baadhi ya miundombinu ya Bandari ya Mwanza North ili kutoathiri shughuli za kibandari katika mkoa huo.

Maboresho haya yatawezesha kuhudumia meli kubwa kama MV. Mwanza Hapa Kazi tu katika Ziwa Victoria.

Profesa Mbawara anasema Serikali pia imeendelea kuongeza wigo wa huduma zake za kibandari kwa kujenga Bandari katika maziwa makuu nchini.

Meli ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu

Katika hilo anasema ujenzi wa Bandari katika Ziwa Tanganyika ambapo mradi wa ujenzi wa Bandari za Kibirizi unaohusisha ujenzi wa gati, uongezaji wa kina, maghala ya mizigo, jengo la abiria na ofisi mbili na Bandari ya Ujiji unaohusisha ujenzi wa gati, jengo la abiria, jengo la kuhifadhi mizigo, ujenzi wa uzio na kuongeza kina.

Mkataba wa uboreshaji wa Bandari ya Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa umesainiwa Januari 11, 2024 na utekelezaji unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kazi zinazofanyika kwa sasa ni maandalizi ya awali ya mradi (mobilisation) yanayojumuisha ukusanyaji wa vifaa, mitambo pamoja na usanifu wa mradi.

Ujenzi wa Bandari hii utaongeza fursa za ajira katika Ushoroba wa Kusini mwa nchi kwa kuunganisha nchi za Malawi na Zambia.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya