Monday, December 23, 2024
spot_img

MNYETI KITANZINI RIPOTI YA TUME ASHTAKIWE MAHAKAMANI

RIPOTI MAALUMU (6)

CHARLES MULLINDA

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyochunguza tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka zilizomkabili Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti alipokuwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Manyara ilimtia hatiani na kupendekeza ashtakiwe mahakamani.

Ripoti ya Tume hiyo ilitoa mapendekezo saba kwa mamlaka na taasisi za umma pamoja na mlalamikaji, Dk. Hamis Kibola.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ipo kikatiba na ilifanya uchunguzi wa tuhuma za Mnyeti na kutoa ripoti yake kwa mujibu wa Ibara ya 130 (1) (c) (f) na (g) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na vifungu 6 (1) (c ) (f) na (g), 11(I) (b) (i) na 22 (5) (a) vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, sura ya 391 ambavyo vinaipa tume hiyo mamlaka ya kutekeleza majukumu hayo. HII NI RIPOTI MAALUMU

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mathew Mwaimu

Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaeleza kuwa baada ya Tume kusikiliza maelezo, kupokea taarifa na vielelezo na kufanya uchambuzi ilibaini kuwa Naibu Waziri Mnyeti, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara alikiuka misingi ya uadilifu, utawala wa sheria, uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji na akiwa kiongozi wa umma hakutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Tume inashauri Dk, Kibola kumshtaki mahakamani Mnyeti kumdai fidia ya madhara ya kukamatwa kinyume cha utaratibu na hasara aliyopata kwa kushindwa kufanya kazi kwa miezi nane kutokana na zuio alilowekewa na Mnyeti.

Inashauri zaidi kuwa Dk. Kibola apeleke vielelezo vya picha alivyonavyo kwa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA) zilizopigwa na watu wengine wanaojulikana lakini zilitumika kwenye taarifa ya uchunguzi iliyoundwa na Mnyeti kuonyesha kuwa anajishughulisha na uwindaji haramu ili TAWA aingalie kama kuna makosa ya jinai kwa waliopiga picha hizo, iwachukulie hatua stahiki.

Pendekezo la pili lililo kwenye ripoti ya Tume linaelekezwa Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), linasomeka;

“Ingawa kwa sasa Mnyeti siyo Mkuu wa Mkoa lakini alitenda matendo hayo akiwa kwenye madaraka ya Mkuu wa Mkoa. Tume inapendekeza wizara hii kuendelea kuwaelekeza wakuu wa mikoa na wilaya kuzingatia misingi ya sheria na utawala bora pamoja na kujua mipaka katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wananchi wanaowahudumia.”

Ripoti ya Tume katika pendekezo lake la tatu inaeleza kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka apitie tena hati ya mashtaka na ushahidi uliomo kwenye kesi ya uhujumu uchumi ambayo mlalamikaji ni Jamhuri dhidi ya Dk. Kibola na wenzake saba.

Kesi hiyo namba 11/2020 ipo Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na Tume inaeleza kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka anapaswa kujiridhisha iwapo kosa la kukwepa kulipa kodi linalomkabili Dk. Kibola na wenzake ni miongoni mwa makosa ya uhujumu uchumi na iwapo Dk. Kibola anapaswa kuendelea kuwa mtuhumiwa katika kesi hiyo.

Pendekezo la nne kwenye ripoti ya Tume limeelekezwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) linalosema ichunguze uhusiano wa Mnyeti na Saleh Salum Al Amry ambaye alikiri kumjengea Mnyeti visima vya maji katika jimbo lake la uchanguzi wakati wa mgogoro kati yake na Dk. Kibola.

Dk. Hamis Kibola

Inaeleza kuwa uchunguzi huo ufanyike ili kubaini endapo uhusiano wao ndiyo sababu ya Mnyeti kuchukua hatua za kumzuia Dk. Kibola kufanya shughuli za uwindaji katika kitalu chake.

“Pia ifanyie kazi tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka kama yalivyobainishwa katika taarifa hii ikiwa ni pamoja na Mnyeti kufanya kazi nje ya mamlaka yake,” inasomeka ripoti.

Pendekeo la tano ni kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo ni msimamizi wa shughuli zote za uwindaji kuwa itoe elimu ya sheria na kanuni za wanyamapoti kwa wenye vitalu vya uwindaji ili wanapopata matatizo katika shughuli zao wayawasilishe wizarani au kwa taasisi zinazoshughulika na masuala ya uwindaji.

Pendekezo la saba kwenye ripoti ya Tume ni kwa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA) kufuatilia malalamiko ya wenye vibali vya uwindaji kukamatwa na watendaji wa Kata na viongozi wa vijiji vyenye shughuli za uwindaji katika maeneo yao ili kuchukua hatua stahiki za kulinda biashara ya uwindaji ambayo inaliingizia pato Taifa.

Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na UItawala Bora inahitimisha mapendelezo yake kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwa ifuatilie mwenendo wa kimaadili wa Mnyeti baada ya Al Amry kuieleza Tume kuwa alimjengea visima vya maji katika jimbo lake wakati wa mgogoro kati yake na Dk. Kibola ili kuchukua hatua stahiki.

Tayari pendekezo la kwanza limeishatekelezwa la Naibu Waziri Mnyeti kushtakiwa Mahakamani lakini kuna sintofahamu kuhusu utekelezaji wa mapendekezo mengine ya Tume kwa mamlaka na taasisi za Serikali kama yalifanyiwa kazi kabla ya Mnyeti kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

KUFAHAMU ZAIDI IWAPO MAMLAKA NA TAASISI ZA SERIKALI ZILIFANYIA KAZI MAPENDEKEZO YA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YALIYOMTIA HATIANI NAIBU WAZIRI MNYETI KWA MAKOSA YA KIMAADILI AKIWA KIONGOZI WA UMMA, USIKOSE KUSOMA TANZANIA PANORAMA BLOG.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya