RIPOTA PANORAMA
SKANDALI mpya inayowahusisha polisi akiwamo kamanda mmoja wa juu wa jeshi hilo ya uporaji wa Shilingi mil. 25, kwenye akaunti ya raia katika Benki ya CRDB imefichuka.
Katika skandali hii, polisi wa Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) Mkoa wa Dodoma wanadaiwa kushirikiana na Blanca Adolph, ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Angelva inayojihusisha na utoaji mikopo, kupora fedha za Valeria Thadey Oisso zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti yake iliyopo Benki ya CRDB.
Polisi wanaotajwa kwenye skandali hii ni Inspekta Edward Mwandinga na wengine wawili wa kike wanaotajwa kwa jina moja moja, ambao ni Happy na Tatu na pamoja nao ni Kamanda mmoja wa juu aliyepata kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa mmoja hapa nchini (jina lake limehifadhiwa kwa muda.)
Valeria Oisso aliyeibua skandali hii amezungumza na Tanzania PANORAMA Blog akidai kuwa tukio hili lilitokea Juni, 2023 na sasa ni zaidi ya miezi sita tangu alipofikisha malalamiko yake kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, lakini wako kimya.
Valeria anadai Juni, 2023 akiwa mfanyakazi wa Kampuni ya Angelva alifuatwa kazini kwake na Inspekta Mwandiga na Afande Tatu wakamtaka aandamane nao kwenda Ofisi ya RCO, Kituo cha Polisi Dodoma.
Anadai, akiwa mikononi mwa polisi hao, Inspekta Mwandiga alimtaka atoe fedha alizoiba kwa bosi wake Blanca tangu alipohamishiwa kituo cha kazi cha Dodoma, naye alikana madai hayo akisema tangu alipohamishiwa Dodoma hakuwa ameweka fedha yoyote kwenye akaunti yake na kwamba fedha alizonazo benki amezipata kwa kufanya biashara ndogo ndogo.
Valeria anadai kanusho hilo lilijibiwa kwa vitisho kutoka kwa Inspekta Mwandinga aliyesema kwa sababu hataki kusema ukweli atafia kituoni kama wengine.
Anadai, Inspekta Mwandinga aliamuru alazwe mahabusu ili akili yake ikae sawa hadi siku inayofuata akatoe fedha kwenye akaunti yake akabidhiwe Blanca.
“Tarahe 2/6/2023. Saa 4 asubuhi, Inspekta Mwandinga alikuja kunitoa mahabusu akanipeleka ofisini kwake, akanikabidhi kwa polisi wawili wa kike, Tatu na Happy pamoja na Blanca; huku akinitisha aliamuru wanipeleka Benki ya CRDB Tawi la Bunge nikatoe pesa.
Jiji la Dodoma
“Tukiwa pale Bunge kwenye Benki ya CRDB, askari hao waliniamuru nitoa pesa zangu shilingi milioni 25 huku wakisema nisipotekeleza hilo sitarudi salama mahabusu kwani wanaweza kunifanya kama mwizi.
“Nilitekeleza matakwa yao kisha tukatoka CRBD Bunge hadi NMB, Jengo la LAPF walikonitaka kuweka fedha hizo kwenye akaunti ya Blanca Adolph lakini kabla sijaziweka walipigiwa simu wasitishe zoezi hilo na pesa zipelekwe ofisini kwao.
“Tuliondoka hadi Ofisi ya RCO Dodoma, tukamkuta msaidizi wa RCO ambaye aliwaamuru warudishe hizo fedha kwenye akaunti yangu. Tukatoka polisi nikiwa chini ya ulinzi wa Inspekta Mwandinga na Happy hadi CRDB, Tawi la Chamwino nikarudisha fedha zangu kwenye akaunti yangu.
“Baada ya hapo nilirudishwa polisi, wakaanza kuchukua maelezo yangu kisha nikanyang’anywa simu zangu akapewa Blanca ambaye ndiye alikuwa mlalamikaji, mimi nikarudishwa mahabusu,” anasema Valeria.
Anaendekea kudai kuwa alikaa mahabusu hadi Juni 6, 2023 alipofuatwa na Inspekta Mwandiga aliyemweleza kuwa ametafutiwa mdhamini na Blanca lakini akaunti yake imefungwa.
Kwamba alidhaminiwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Hilary Mark Leshira na kupelekwa nyumbani kwa mlalamikaji Blanca kwa ajili ya mazungumzo na wakiwa hapo mlalamikaji Blanca alipigiwa simu na ofisa wa juu wa polisi aliyesema anawasaidia ili kesi hiyo ifutwe hivyo waongee hapo nyumbani.
Valeria anadai afisa huyo wa polisi alielekeza iadikwe barua ya kuondoa shauri polisi na uandikwe muhtasari wa kikao unaoonyesha Valeria akikiri pesa zake ni za Blanca.
“Blanca aliita watu kwa ajili ya kikao hicho na alikuwepo yeye mwenyewe, Setasi Massawe, Hilary Mark na mdogo wangu Gema aliyekuwa mwanachuo Udom.
“Blanca alimwelekeza mdogo wangu Gema kukopi muhutasari ulioandikwa na mdhamini kuwa nimekiri kosa. Baadaye walinichukua hadi Benki kuuliza kama akaunti yangu imefunguliwa wakaambiwa bado imefungwa kwa amri ya polisi na kesho yake Juni 12, 2023 nilipigiwa simu na Afisa wa Benki nikaambiwa akaunti yangu imefunguliwa kwa maelekezo ya polisi.
“Saa 9 alasiri ya siku hiyo nilichukuliwa na afisa wa juu wa polisi pamoja na Blanca. Afisa huyo wa polisi alisema kesi yangu imefutwa lakini ninapaswa kuandamana nao hadi benki nikatoe pesa nimpe Blanca. Afisa huyo wa polisi alikuwa na bastola na alinitisha kuwa atanipoteza nisipotii maelekezo.
Bastola
“Nilikataa kutoa pesa zangu, afisa yule wa polisi akinirudisha tena mahabusu lakini muda mfupi baadaye alikuja Inspekta Mwandinga akasema ninawasumbua sana na bosi wao amekasirika sana. Nikapelekwa Ofisi ya RCO.
“Huko wakachukua simu zangu wakasema zinapelekwa maabara kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kisha nikapelekwa kupigwa picha, wakachukua alama za vidole akaitwa mdhamini akaambiwa ajitoe kwenye udhamini.
“Mpaka hapo nijiona kama nimekufa kwa mateso yale. Walikuja jioni kunichukua wakanipeleka kwa wakala wakaniamuru nitoe pesa, wakala hakuwa na pesa za kutosha alikuwa na Shilingi milioni 5 tu. Nilizitoa nikaamrishwa niziweke kwenye akaunti ya Blanca.
“Baada ya hapo nikapelekwa benki wakaniamuru nifanye uhamisho wa pesa zilizosalia niziweke kwenye akaunti ya Blanca, nikatii. Ndipo nikaachiwa,” anasema Valeria.
Akiendelea kuelezea mkasa huo, anasema baada ya akili yake kutulia, alipeleka malalamiko yake Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
Valeria anasema amefikisha malalamiko yake Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara wa Mambo ya Ndani na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kwa zaidi ya miezi sita sasa lakini kote huko pako kimya.
Tanzania PANORAMA Blog imewatafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Theopista Mallya, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime, Kamanda wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Dodoma, mpelelezi wa kesi, Afande Omary Nasir, afisa katika Ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani anayeshughulikia malalamiko ya Valeria na Blanka mwenyewe kuzungumzia skandali hii.
Ili kujua kilichojiri baada ya watumishi hao wa umma kuulizwa kuhusu skandali hii, mlalamikaji Blanca na pia kumjua Kamanda wa Juu wa Polisi anayedaiwa kutumia bastola kushinikiza raia kutoa pesa zake benki, soma Tanzania PANORAMA Blog kesho.