Vatican
PAPA wa Kanisa Katoliki ambaye ni Askofu wa Roma, Papa Fransisco amewataka waumini wa Kanisa Katoliki kuishi katika umoja na kutotengana kwa sababu ya kile alichokiita, uchafu na najisi.
Amesema kanisa na jamii havipaswi kumtenga au kumchukulia mtu ni mchafu au najisi bali kila mtu, bila kujali maisha yake ya zamani apokewe na kupendwa bila alama na chuki.
Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican, Papa amefundisha hayo leo katika mahubiri aliyoyatoa kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro huko Vatican alikoongoza tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana kwa mahujaji na waumini waliohudhuria Ibada ya Dominika ya 13 ya mwaka B.
Papa alianza tafakari yake kwa kueleza kuwa Injili ya Liturujia ya Dominika ya 13 ya mwaka B inaeleza juu ya miujiza miwili inayofanana iliyofanywa na Yesu Kristu.
Amesema Yesu alipokuwa njiani kwenda kwenye kaya ya Yairo, mwananke mmoja aliyekuwa mgonjwa akisumbuliwa na tatizo la kutoka damu aligusa vazi lake akapona.
Papa amesema wakati huo huo, binti wa Yairo aliyekuwa tayari amekufa, Yesu alipofika kwenye kaya ya Yairo alikwenda chumbani kwake, akamshika mkono, akamuinua, akamfufua.
Amesema miujiza hiyo miwili mmoja wa uponyaji na mwingine wa ufufuo ilifanywa kwa mawasiliano ya mwili; wa kwanza ukiwa wa mwanamke aliyegusa vazi la Yesu na wa pili kumshika mkono binti aliyekuwa amekufa.
“Hata kabla ya kufanya uponyaji wa kimwili, Yesu alipinga imani ya kidini ya uongo kwamba Mungu huwatenganisha walio safi, akiwaweka upande tofauti na wasio safi. Mungu hafanyi utenganisho kwa sababu sisi sote ni watoto wake.
“Uchafu hautokani na chakula, magonjwa au kifo, uchafu hutoka katika moyo mchafu,” amesema Papa Fransisco na kuongeza.
“Mbele ya mateso ya kimwili na ya kiroho, ya majeraha ambayo roho zetu hubeba. Juu ya hali zinazotuponda na hata katika uso wa dhambi, Mungu hatuweki mbali.
“Mungu hatuonei haya, Mungu hatuhukumu. Kinyume chake yeye hukaribia ili kujiruhusu mwenyewe kuguswa na kutugusa na hutufufua daima kutoka katika wafu. Daima anatushika mkono na kusema, binti, mwana, inuka.”
Papa amesema mtu anaweza kusema yeye ana dhambi lakini Yesu humjibu ajitahidi kwenda mbele kwani amekuwa mdhambi kwa ajili yake ili amuokoe.
“Unaweza kusema bwana mimi ni mwenye dhambi, lakini yeye atakujibu jitahidi kwenda mbele; nimekuwa mdhambi kwa ajili yako ili nikuokoe na wewe utasema lakini wewe bwana si mwenye dhambi, naye atakujibu hapana, nimevumilia matokeo yote ya dhambi ili kukuokoa,” amesema Papa.