Monday, December 23, 2024
spot_img

TISS, POLISI, TAKUKURU, TRA, DPP WATAJWA SAKATA LA N/ WAZIRI MNYETI

RIPOTI MAALUMU (3)

CHARLES MULLINDA

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti, akiwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Manyara aliunda kamati ya kuchunguza ujangili kwenye kitalu kinachomilikiwa na Kampuni ya HSK Safaris Ltd ya Dk. Hamis Kibola ambayo ripoti yake haikuwa na tija ikiwa na wajumbe kutoka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP).

Hivyo ndivyo inavyoelezwa kwenye Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyochunguza malalamiko ya matumizi mabaya ya madaraka yaliyodaiwa kufanywa na Mnyeti alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.

Ripoti inaonyesha kuwa ni Mnyeti mwenyewe ndiye aliyeieleza Tume kuhusu kuunda kamati hiyo baada ya kupokea barua kutoka kwa wananchi iliyokuwa ikieleza uwepo wa uwindaji haramu katika kitalu kunachomilikiwa na Kampuni ya HSK Safaris Ltd ya Dk. Hamis Kibola.

Hata hivyo, maelezo ya Mnyeti mbele ya Tume ilipokuwa ikimuhoji kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ya aliyekuwa akitekeleza amri zake dhidi ya Dk. Kibola, Afisa Mtendaji wa Kata ya Emboreet, Belinda Sumari yanaacha taswira kwamba; maelezo ya Mnyeti jumlisha ya Belinda ni sawasawa na malalamiko ya Dk. Kibola. HII NI RIPOTI MAALUMU.

Jaji Mathew Mwaimu

Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Oktoba 25, 2021 iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mathew Mwaimu kuhusu uchunguzi wa matumizi mabaya ya madaraka yaliyodaiwa kufanywa na aliyekuwa RC wa Manyara, Mnyeti inaeleza kuwa wakati wa uchunguzi wake iliwahoji viongozi na wadau muhimu wenye ufahamu kuhusu malalamiko hayo na lengo la kuwahoji lilikuwa kupata ufafanuzi kuhusu malalamiko iliyofikishiwa.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ipo kikatiba na mamlaka yake yanatamkwa kwenye Ibara ya 130 (I) (c) (f) na (g) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na vifungu vya 6 (I) (c) (f) na (g), 11 (I) (b) (i) na 22 (5) (a) vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Ripoti inaonyesha Tume ilimuhoji Mnyeti Juni 25, 2021 wakati huo akiwa Mbunge wa Misungwi na katika maelezo yake alisema alifahamu kuwepo kwa mgogoro wa kibiashara baina ya Dk. Kibola na Salum Al Amry na aliunda kamati ya uchunguzi baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu uwindaji haramu uliokuwa ukifanyika katika kitalu kinachomilikiwa na Kampuni ya HSK Safaris Ltd ya Dk. Kibola.

Kwamba barua iliyopelekwa kwake ilimtuhumu Dk. Kibola kufanya ujangili kwenye kitalu hicho kwa zaidi ya miaka kumi na alikuwa analindwa na wakubwa, lakini Tume ilipomuhoji Mnyeti wakubwa hao ni akina nani, hakuwataja.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti

Ripoti inaeleza zaidi kuwa Mnyeti alieleza kutokana na barua ya wananchi iliyokuwa na taarifa za uwindaji haramu katika kitalu cha Dk. Kibola, aliunda kamati ya uchunguzi ikiwa na wajumbe kutoka Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mamlaka ya Mapato na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa.

Kwamba Mnyeti aliieleza Tume kuwa Dk. Kibola alikamatwa Disemba 19, 2019 na Kikosi Kazi dhidi ya ujangili kiichoundwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, akiwa Dar es Salaam. Kikosi kazi hicho kilikuwa kikiongozwa na Meja Mbeho, kama mwenyekiti wake.

Sehemu ya ripoti hiyo inasomeka hivi; ‘kwamba ni kweli alimzuia mlalamikaji kwenda kitaluni kwa kumuandikia barua ambazo zilikuwa ofisini mkoani Manyara. Alitoa zuio hilo kwa kuwa wakati uchunguzi unaendelea pia kilikuwepo kikosi kazi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambacho kilikuwa kinafanya uchunguzi tofauti na kamati yake na matokeo yake, wote walibaini kuwepo kwa uwindaji haramu.

‘Baada ya kamati yake kumaliza uchunguzi ilitoa mapendekezo kuwa mlalamikaji afunguliwe kesi, ndipo Mkurugenzi wa Mashtaka alimfungulia kesi ya uhujumu uchumi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara ambayo inaendelea.’

Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inayo pia mahojiano iliyofanya na aliyekuwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Emboreet, Juni 30, 2021 ambayo kwa sehemu, yanapeana mgongo na yale ya Mnyeti.

Belinda Sumari

Inaeleza kuwa Belinda Sumari aliieleza Tume kulifahamu suala la Dk. Kibola na alikiri kwamba yeye ndiye aliyemzuia kuingia kwenye kitalu chake kwa maelekezo ya simu aliyoyapokea kutoka kwa Mnyeti.

Inasomeka hivi; ‘Alifafanua kuwa alikuwa anapata maelekezo kwa njia ya simu kutokana na hali ya kijiografia ya maeneo ya Simanjiro hivyo hakuwa na barua yoyote kuhusu maelekezo hayo.

‘Aliendelea kueleza kuwa alipokea simu kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akimueleza kuwa amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu uwindaji haramu eneo la Lokonwa, ambapo Kampuni ya HSK Safaris Ltd inayomilikiwa na Dk. Hamis Said Kibola ambayo ilikuwa inafanya shughuli za uwindaji hivyo asiruhusu kampuni hiyo kuingia kitaluni kwa kuwa kulikuwa na uchunguzi ukiendelea hadi pale maelekezo mengine yangetolewa.

‘Pia alielekezwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa aweke mgambo wawili kwa ajili ya kulinda eneo hilo ambao wangelipwa baada ya kesi iliyoko mahakamani kuisha.’

Belinda aliieleza Tume kuwa Dk. Kibola aliingia kwenye kitalu chake Juni 26, 2020 bila ruhusa na yeye alipigiwa simu na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, wakati huo Zephania Chaula akimueleza kuwa kuna maagizo kutoka kwa Mnyeti amkamate.

Ripoti inaonyesha zaidi kuwa Belinda pia alipigiwa simu na Mnyeti mwenyewe aliyemweleza kuwa amekosea kumwacha Dk. Kibola kuingia kwenye kitalu chake hivyo amkamate ampeleke kituo cha polisi.

“Mlalamikaji alikamatwa tarehe 26/6/2020, saa tatu usiku na kufikishwa Kituo cha Polisi Orkesumet, Simanjiro saa saba usiku. Baada ya kumfikisha kituo cha polisi hakuendelea zaidi ya hapo.’

Belinda aliieleza Tume kuwa alihamishwa kutoka Kata ya Emboreet kwenda Kata ya Loiborsoit tarehe 16/12/2020 na anaamini uhamisho huo ulikuwa wa kawaida.   

Dk. Hamis Kibola

Dk. Kibola aliyekimbilia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kumlalamikia Mnyeti na Belinda,  alihojiwa na Tume Julai 5, 2021 na pamoja na kujieleza kwa mdomo, pia aliwasilisha maelezo ya maandishi mbele ya Tume.

Ripoti ya Tume inaonyesha kuwa, akijieleza, Dk. Kibola alisema Disemba 19, 2019 alipigiwa simu na Belinda kumtaarifu kuwa haruhusiwi kuingia kwenye kitalu cha uwindaji Simanjiro na siku hiyo hiyo alikamatwa akiwa mkoani Dar es Salaam na kupelekwa Arusha.

Kwamba akiwa Arusha, aliwekwa mahabusu Kituo cha Polisi Utalii kwa muda wa siku saba bila kufikishwa mahakamani.

Inaendelea ripoti kuwa Dk. Kibola na mkewe ni wamiliki wa Kampuni ya HSK Safaris Ltd, yeye akiwa na hisa asilimia 80 na mkewe aliyemtaja mbele ya Tume kwa jina la Gilder Fanuel Kibola akiwa na asimilia 20 na kampuni yao inamiliki vitalu viwili, kimoja kikiwa Pori Tengefu la Simanjiro Magharibi na kingine Ngalambe, Tapika wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa ripoti, Dk, Kibola aliingia ubia wa kibiashara na Saleh Al Amry kwa makubaliano ya mdomo kuwa HSK Safaris Ltd itoe kitalu na Amry ajenge kambi katika Kijiji cha Lokonwa, mahali kilipo kitalu.

Hapo, ripoti inasomeka hivi. ‘Kwamba kipindi wanafanya biashara kulitokea kutoelewana na ndipo walipoacha kufanya biashara pamoja, sababu kubwa ya mgogoro kati yao ilikuwa kutokuwepo kwa faida katika biashara yao ya pamoja.

‘Kwamba aliamini kuwa Saleh ndiye aliyepeleka malalamiko kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Mnyeti kuhusu kuwepo kwa matatizo ya ujangili katika kitalu cha Simanjiro. Kwamba aliamini Mhe, Alexander Mnyeti alitaka kumnyang’anya kitalu cha uwindaji kwa manufaa ya Saleh.

‘Kwamba kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa ilimuhoji lakini hakupewa nakara wala mapendekezo ya taarifa hiyo bila sababu. Kwamba alizuiliwa kuingia na kufanya shughuli za uwindaji kitaluni kwa miezi nane bila sababu licha ya kuwa na vibali vyote.

‘Kuzuia huko kulikuwa kwa manufaa ya Saleh kwa sababu lengo la zuio lilikuwa kumdhoofisha yeye kibiashara. Wakati wa zuio Saleh aliruhusiwa kwenda kitaluni na alikuwa na ushahidi.’

Ripoti inakariri zaidi maelezo ya Dk, Kibola kuwa zuio alilowekewa halikuwa halali ndiyo maana Mnyeti alikataa kuonana naye na wala hakujibu barua alizomwandikia, yeye na Belinda.

Inasomeka; ‘kwamba Saleh ni mshirika wa Alexander Mnyeti na alimchimbia visima vya maji jimboni kwake kama msaada.’

Dk. Kibola aliieleza Tume kuwa hakutenda kosa lolote la kuhatarisha amani alipoingia kitaluni kwake bali alikwenda kufanya shughuli zake na uthibitisho wa hilo ni kuwekwa mahabusu kisha kuachiwa bila kufikishwa mahakamani.

Pia aliieleza Tume kuwa kesi namba 11/2020 aliyofunguliwa ya ukwepaji kodi ilitengenezwa lengo ashindwe kulipa katika plea bargaining ili biashara yake ichukuliwe na Saleh na kwamba hata ushahidi wa picha zilizotumika kwenye taarifa ya kamati ya Mnyeti zilitolewa Instagram.

Alisema picha hizo hazina uhusiano na shughuli zake za uwindaji bali zilitumika kutimiza lengo la kuthibitisha uwindaji haramu lakini wenye picha hizo wanafahamika.

ITAENDELEA KESHO…    

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya