Wednesday, June 25, 2025
spot_img

DEWJI ADAI ANA VIBALI VYA KUUNDA MAGARI KWA SPEA CHAKAVU

RIPOTA PANORAMA

MWENYEKITI wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (T) Limited (MeTL), Gullam Dewji amesema kampuni yake ina vibali vya kuunda magari hapa nchini kwa kutumia spea chakavu inazoagiza kutoka nje ya nchi.

Dewji ameyasema hayo wiki hii alipoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu kampuni yake kutajwa kuwa miongoni mwa zinazoagiza spea chakavu kutoka nje ya nchi kuja kuziunganisha kuunda magari hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo na uchunguzi uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog, wapo watu na kampuni binafsi zinazonunua magari nje ya nchi kisha kuyakatakata au kuyaachanisha na kuyasafirisha kwenye kontena kama spea chakavu hadi hapa nchini.

Taarifa hizo zinadai kuwa spea hizo chakavu baada ya kufikishwa nchini huunganishwa na kuwa magari ambayo huingia barabarani kutumika yakiwa hayajalipiwa kodi. Inadaiwa zaidi kuwa ujanja huo unatumiwa na baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi.

Dewji akijibu kupitia kwa msaidizi wake aliyejitambulisha kwa jina moja la Rachel, alisema biashara yake ya kuunda magari kwa kutumia spea chakavu imesajiliwa na uagizaji wa spea hizo unazingatia ulipaji ushuru wa serikali uliopo.

Alisema kodi zote stahiki zinalipwa na magari yanayoundwa kwa spea hizo chakavu yanakaguliwa na Shirika la Viwango (TBS) kabla ya kusajiliwa na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi na Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Hudson Kamoga.

Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza zaidi kuwa MeTL ilipata lini kibali cha kuunda magari kwa kutumia spea chakavu, tangu kuanza mpaka sasa ni magari mangapi ambayo kampuni hiyo imeunda kwa kutumia spea chakavu, mangapi yanatumika na iwapo magari hayo ni kwa ajili ya MeTL pekee au huingizwa sokoni kuuzwa kwa wateja wengine.

Akijibu, alisema yupo safarini atajibu maswali hayo atakaporejea.

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi na Huduma kwa Wateja wa TRA, Hudson Kamoga ameulizwa leo kuhusu kusajiliwa kwa MeTL kufanya biashara ya kuagiza spea chakavu kutoka nje ya nchi kuja kuziunganisha kuunda magari naye akijibu, amesema kazi ya TRA siyo kusajili biashara bali kutoza kodi.

Alisema mfumo wa ulipaji kodi una mnyororo mrefu unaohusisha taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo za udhibiti ubora na ukaguzi wa bidhaa ambazo baada ya kukamilisha kazi zake ndipo TRA hutoza kodi husika kwa kuzingatia nyaraka zilizoidhinishwa na taasisi hizo.

Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta Mkurugenzi Mkuu wa TBS kuzungumzia suala hilo na mmoja wa wasaidizi wake alielekeza aandikiwe maswali kwa maandishi ambayo ameahidi kuyatolea kauli Jumatatu, Juni 24, 2024.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya