Monday, September 8, 2025
spot_img

ESTHER BULAYA ‘AMCHANACHANA’ MWIGULU MAFAO YA WASTAAFU  

 RIPOTA PANORAMA

BUNGE limeambiwa kuwa serikali inavunja sheria kulinda makosa yake ya kupoka mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Hayo yameelezwa leo bungeni Dodoma na Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya alipokuwa akichangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali iliyowasilishwa wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.

Bulaya amesema sheria namba 6 (3) iliyotungwa na Bunge mwaka 2018 inaipa mamlaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kulipa mafao ya wastaafu hivyo hotuba ya bajeti ya Kuu ya Serikali iliyosomwa na Waziri Mwigulu ikieleza kuwa serikali italipa mafao, inakinzana na sheria.   

“Sheria ya mwaka 2018, PSSSF kifungu cha 6 (3) kinaeleza mamlaka ya kulipa wanayo mifuko, NSSF sheria ya mwaka 2018, kifungu cha 3 (2) kinaeleza mwenye mamlaka ya kulipa ni mifuko. Ninyi mnataka mvunje sheria kuficha makosa yenu.

“Unasema mmesimamisha, mtalipa mpaka 2029, mnalipa ninyi kama nani? Tumetunga sheria mwaka 2018, imetaja wazi mwenye mamlaka ya kulipa wastaafu ni mifuko ya Hifadhi ya Jamii,” amesema Bulaya.

Akichangia; alinukuu kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akipokea gawio kutoka mashirika ya umma ambapo alieleza kutoridhishwa na mwenendo wa ufanisi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Wabunge wakiendelea na majukumu yao ndani ya ukumbi wa Bunge, Dodoma

Kwamba Rais alisema makosa ya wengine ikiwemo serikali, yasiwaonee watumishi wa umma na kwamba Rais alizungumzia uwekezaji usiokuwa na tija kwenye maeneo mbalimbali kupitia fedha za mifuko ya jamii.

“Kamati ya bejeti, ukurasa wa 87 wamezungumzia uwekezaji usiokuwa na tija na kuathiri mifuko na hii inasababisha watumishi wanapunguziwa mafao yao.

“Mnaleta sheria siyo kwa ajili ya kulinda bali kuacha mifuko hohehahe na mnataka kuwadhulumu watumishi wa umma.

“Hotuba ya waziri, ukurasa 101 anasema wamerudisha kikotoo asilimia 40, yaani kama zawadi. Watu walikuwa wakichukua mafao kama kikotoo kwa asilimia 50 na walikuwa wakiendelea kulipwa pensheni za kila mwezi kwa miaka 15. Ninyi vyote hivyo mmepunguza halafu mnasema lengo ni kuwasaidia watumishi wa umma,” amesema Bulaya.

Amesema serikali imewekeza miradi isiyolipa na inayotengeneza hasara.

Bulaya amesema serikali inadaiwa na mifuko ya Hifadhi ya Jamii zaidi ya Shilingi trilioni 2 na kushauri izilipe ili mifuko hiyo iweze kufanya kazi ipasavyo.

Aliishauri pia serikali kuacha kutumia fedha za mifuko kufanya uwekezaji holela ili mifuko hiyo iwe na uwezo wa kuwalipa vizuri wastaafu mafao ya mkupuo na pensheni za kila mwezi.

“Haya mambo mnakaa wenyewe mnaamua bila kuwashirikisha, ndiyo maana leo mnaenda kuchukua mamlaka ambayo siyo yenu.

“Hizi pesa mnazosema mnalipa pelekeni kwenye mifuko wenyewe walipe. Walipeni madeni, fanyeni mifuko iwe imara ili siku moja watumishi  wanaofanya kazi kwa jasho na damu waamue hata kuchukua mafao yao kwa mkupuo kwa asilimia 70. Inashindikana nini kama mifuko iko imara?” amesema Bulaya

Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba

Aidha, Bulaya alihoji serikali kuhusu kile alichokiita ‘mortgage,’ alichosema kimewekwa kwenye sheria iliyotungwa mwaka 2018.

“Ilikuwa danganya toto wakati mnawashawishi wakubali asilimia 33, inatekelezeka? Najua kanuni tayari za mwaka 2024, GN imetoka namba 140 tangu Machi 8, 2024, kiko wapi.

“Mliwambia mtawapa asilimia 33 halafu watakuwa na uwezo wa kwenda kukopa kupitia pensheni zao waweze kujenga nyumbna ili hata wakipata kidogo wawe na ahueni.

“Leo hakuna mtu anayeruhusiwa kwenda kukopa. Anayepata milioni 17, nusu yake atajenga nyumba?  wafanyakazi siyo watoto wadogo, wana familia ila hawawezi kuandamana, wanaandamana kwenye mioyo,’ amesema.

Mbunge huyo  aliweka angalizo kuwa bajeti ya Shilingi trilioni 49 inayopitishwa na Bunge haiwezi kusimamiwa ipasavyo na wafanyakazi wenye manung’uniko na wanaodhulumiwa.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya