RIPOTA PANORAMA
MWENYEKITI wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (T) Limited (METL), Ghulam Dewji (pichani hapo juu) amekana kampuni yake kuwa na uhusiano wa aina yoyote na Kampuni ya ITEL East Africa Limited.
Amesema masuala yanayohusu Kampuni ya ITEL East Africa Limited yasihusishwe na kampuni yake huku akionyesha wasiwasi kuulizwa maswali kuhusu uhusiano wa kampuni yake na ITEL, akisema anayemuuliza ametumwa na watu.
Dewji alizungumza na Tanzania PANORAMA Blog wiki iliyopita baada ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kuitaja METL kwenye skandali ya sukari aliposema iko nyuma ya Kampuni ya ITEL inayofanya biashara ya kuuza rejereja simu za mkononi, kompyuta na vifaa vingine vya mawasiliano lakini ilipewa zabuni ya kuagiza tani 60,000 za sukari na Bodi ya Sukari.
“Mpigie mwenyewe umuulize, mimi siyo mtu wa ITEL. Kama unaniuliza umetumwa na watu. Ukweli ITEL kampuni inajulikana wenyewe na kuna wakurugenzi. Ukikuta mimi nimehusika kwenye ITEL uniambie mimi muongo. Nimemaliza, kama una maswali zaidi niandikie,” alisema Dewji.
Tanzania PANORAMA Blog ilimwandikia Dewji kumuuliza ni nini kauli yake kuhusu kampuni yake kwa miaka kadhaa kutajwa kuhusika kwenye migogoro inayohusisha uagizaji sukari kutoka nje ya nchi na hivi karibuni, Mbunge Mpina ameonyesha kuwa ilitumia Kampuni ya ITEL kuagiza tani 60,000 za sukari na bidhaa hiyo kuwekwa kwenye maghala ya METL.
Swali la pili aliloulizwa Dewji ni; ‘METL ina uhitaji mkubwa wa sukari kwa ajili ya viwanda vyake vya vinywaji baridi, je hii ndiyo sababu ya kampuni yako kutajwa mara kwa mara kwenye kashfa zinazohusu sukari?
Dewji aliulizwa pia ni wapi METL inanunua sukari kwa ajili ya kuendesha viwanda vyake vya vinywaji baridi ambapo inaelezwa hutumia maelfu ya tani kwa siku.
Akijibu, alisema msaidizi wake atatuma majibu ya maswali hayo na muda mfupi baadaye, mtu aliyejitambulisha kwa jina la Rachel alituma ujumbe wa maneno kwa simu yake ya kiganjani akieleza kuwa jambo hilo limetolewa kauli na Bunge na Serikali na linaendelea kufanyiwa kazi hivyo hawezi kulizungumzia.
Tanzania PANORAMA Blog inazo taarifa kuwa METL inatumia zaidi ya tani 150 za sukari kwa siku moja kwa ajili ya viwanda vyake vya vinywaji baridi lakini imekuwa ikijiweka kando kueleza bayana inanunua wapi shehena ya sukari kwa ajili ya viwanda vyake.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina
Mpina alizungumza na waandishi wa habari Juni 14, 2024 mkoani Dodoma kuhusu ushahidi aliouwasilisha kwa Spika wa Bunge kuthibitisha kauli yake kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema uongo bungeni; pamoja na mambo mengine, Mpina alisema zipo taarifa kuwa ITEL East Africa Limited inatumiwa na Kampuni ya METL kwa mgongo wa nyuma kuagiza sukari nje ya nchi kwa niaba yake.
Alisema taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonyesha kuwa mzigo wa sukari wa Kampuni ya ITEL ukifika bandarini hutolewa na Kampuni ya METL na kwamba taarifa za uhakika zinazonyesha baada ya mzigo kutolewa bandarini hupelekwa bandari kavu (ICD) ya METL.
Mpina alisema mzigo huo wa sukari unapotolewa kwenye ICD ya METL hupelekwa kwenye maghala ya METL na baadaye kuuzwa rejereja na alitaja risiti ya TRA ya EFD yenye namba 32 ya Februari 22, 2024 na risiti yenye namba ya uthibitisho 28630946606 ya Februari 23, 2024 iliyotolewa na Kampuni ya METL kama uthibitisho wa maelezo wake.
“Mahusiano ya kibiashara baina ya Kampuni ya Mohammed Enterprises (T) Ltd na ITEL East Africa Ltd hayako wazi na yanaweza ikawa ni mkakati wa kutakatisha fedha haramu na kukwepa kodi za serikali,” alisema Mpina.
Tanzania PANORAMA Blog imeonyeshwa baadhi ya risiti zinazodaiwa kutumiwa na kampuni hiyo kuuza sukari kwa rejereja na hivi karibuni itaripoti kwa kina baada ya kukamilika kwa uchunguzi inaoufanya kuhusu skandali hii.
Kwa mujibu wa taarifa ya maandishi ya Mpina ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona, inaeleza kuwa Kampuni ya ITEL East Africa Limited iliandikiwa barua yenye kumb. Namba SBT/DGO/09/VOL11/2-10 kuitaarifu kuwa serikali imeiidhinisha kuingiza tani 50,000 za sukari.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Kwamba barua hiyo iliandikwa Januari 2, 2024 na kutiwa saini na Lusomyo Buzingo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari lakini Januari 9, 2024 Kampuni ya ITEL ilipewa vibali vya kuingiza tani 60,000 za sukari hapa nchini ikiwa ni zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa kwenye barua na inavitaja vibali hivyo kuwa ni chenye namba SR. 8652445335 na 944600548.
Sehemu ya taarifa ya Mpina inasomeka; “pia vibali alivyopewa ITEL ni zaidi ya viwanda vyote vitano ambavyo jumla vimepewa tani 50,000 tu kwa maana ya tani 10, 000 kila kiwanda.
“Baada ya kufanya upekuzi BRELA tarehe 10 Juni, 2024 ilibainika kuwa Kampuni ya ITEL East Africa Limited imesajiliwa tarehe 15, Februari 2013, yenye ofisi zake Ilala, Dar es Salaam kwa ajili ya biashara za kuuza simu, kompyuta, Tehema na vifaa vingine vya mawasiliano na sio biashara ya sukari.”
Skandali hii imeibuliwa na Mpina huku Taifa likiwa bado na kumbukumbu ya maumivu ya bei aghali ya sukari iliyosababishwa na kuadimika kwa bidhaa hiyo na baada ya Mpina kuiibua, kuna mjadala mkubwa katika jamii kuhusu utaratibu unaotumiwa na Bodi ya Sukari kutoa vibali vya kuagiza sukari nje kwa wafanyabishara wasiokuwa wazalishaji wa sukari.