Tuesday, December 24, 2024
spot_img

SERIKALI YAWATAKA WANANCHI KUFUNGA KIFAA CHA KUZUIA ATHARI ZA UMEME MAJUMBANI

*Lengo ni kujilinda na athari za umeme
*Kapinga ataja juhudi zinazofanywa na Serikali kuimarisha hali ya umeme Jimbo la Segerea
*Asema usambazaji umeme vijijini unaendelea, vitongoji 4000 kupatiwa umeme 2024/2025

TERESIA MHAGAMA

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka wananchi kufunga vifaa vya kuzuia athari za umeme kwenye nyumba (circuit breaker) ili kujilinda na majanga yanayoweza kutokea umeme unapokuwa mwingi au kupungua.

Kapinga amesema hayo leo Juni 13, 2024 bungeni, Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli aliyehoji mpango wa serikali kwa wananchi wanaopata hasara kutokana na kukatika kwa umeme au nyumba kuungua.

Amesema uchunguzi unapothibitisha kuwa tatizo la kuungua kwa nyumba limesababishwa na TANESCO, Serikali inachukua hatua kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Akizungumzia hali ya umeme katika Jimbo la Segerea, Kapinga ameeleza kuwa changamoto ya kukatika kwa umeme katika jimbo hilo ilitokana na kuzidiwa kwa kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Gongo la Mboto ambacho kinapeleka umeme Segerea.

Amesema hali ya upatikanaji umeme Segerea sasa imeimarika baada ya serikali kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza; na alitaja moja yah atua zilizochukuliwa ni kuwezesha baadhi ya wakazi wa eneo hilo kupata umeme kutoka kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Kipawa.

Kapinga amesema serikali kupitia TANESCO  inatekeleza miradi ya upanuzi wa Kituo cha Gongo la Mboto na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ubungo hadi Tabata ili kuimarisha zaidi upatikanaji wa umeme.

Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso aliyehoji mpango wa serikali kupeleka umeme kwenye maeneo muhimu katika eneo la Mishamo, hasa kwenye Soko na Kituo cha Afya.

Akijibu; Kapinga amesema ni mkakati wa serikali kuhakikisha umeme unakwenda kila kijiji na miradi  ya usambazaji umeme inaendelea ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/25 vitongoji 4,000 vitapata umeme.

Akijibu swali la Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa aliyetaka kujua mkakati wa serikali kuimarisha umeme kwenye Vijiji vya Namtumbo vinavyopata umeme mdogo, Kapinga amesema tayari serikali inatekeleza mpango wa kuongeza nguvu umeme kwenye maeneo ya vijijini.



Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya