Monday, December 23, 2024
spot_img

TUHUMA MIKOPO CHECHEFU ZACHAMBULIWA (1)

RIPOTA PANORAMA

SAKATA la tuhuma za kuwepo mikopo chefuchefu linalohusisha baadhi ya wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa, kampuni zao, benki, mawakili na watumishi wa mahakama limezungumziwa na wasomi na mawakili.

Tuhuma hizo ziliibuliwa kwanza kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, kisha ikaibuka mijadala mikali yenye hoja kinzani kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandaoni.

Tanzania PANORAMA Blog imefanya mahojiano na wasomi na mawakili mbalimbali ambao wametoa maoni yao kuhusu skandali hiyo, wakiweka kwenye mizani ya ulinganifu uzito wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya uhalisia wa kilichotuhumiwa.

Mtaalamu wa Masuala ya Utawala, Buberwa Kaiza ameulizwa maoni yake kuhusu tuhuma za kuwepo mikopo chefuchefu inayogusa baadhi ya watumishi wa muhimili wa mahakama, naye akijibu hilo kwa kusema tuhuma zisizokuwa na ushahidi ni uzushi.

Amesema mahakama ina utaratibu kuwa, wasioridhika na uamuzi uliotolewa dhidi ya mashauri au kesi zao hukata rufaa, na mtu anayedhani Hakimu au Jaji anayesiliza kesi yake hamtendei haki, ana haki ya kumkataa asisikilize kesi yake.

Amesema ni vigumu kuhukumu jumla jumla kwamba aliyesikiliza kesi na kuhukumu yupo kwenye mtandao wa aina fulani kwa sababu wadai na wanaodaiwa wana mawakili ambao ni wajuzi wa sheria wanaowawakilisha mahakamani.

Buberwa Kaiza

“Ni vigumu kuizungumzia mtaani ikawa na maana kwa sababu lazima uwe na ushahidi wa kutosha kutuhumu hivyo, vinginevyo inakuwa umbeya tu.

“Kimaadili huwezi kuzungumzia kitu ambacho kinawagusa watu, maslahi ya makampuni, maslahi ya benki juu juu tu bila kuwa na ushahidi wa kutosha. Zinabaki kuwa tetesi tu lakini siyo kitu cha kuaminika,” anasema Kaiza.

Akizungumza kuhusu Jaji kukataa kujitoa kwenye kesi, anasema ikitokea Jaji anakataa kujitoa kwenye kesi lazima anakuwa na sababu ingawa wapo baadhi ya majaji ambao hawapendi kutuhumiwa kwa lolote hivyo wanapobaini kuna ugumu wa uamuzi wao kuaminika huwa wanajitoa.

“Jaji anapokataa kujitoa kwenye kesi anakuwa na sababu, hawezi kukataa hivi hivi tu. Mfano akiangalia akakuta hakuna hoja ya msingi iliyoletwa ya yeye kujitoa, anaweza kukataa kujitoa.

“Lakini pia majaji wana hadhi tofauti ingawa wote ni majaji. Wapo ambao hawapendi kutuhumiwa kwa lolote na hii ni kwa sababu majaji wa aina hii wanajua Jaji anatakiwa aaminike. Sasa, hawa, muda wowote akiona ni vigumu kuaminika katika uamuzi atakaoutoa, huwa wanajitoa. Hawa huwa hawataki kabisa kutuhumiwa.

“Lakini wapo majaji ambao hawaoni tatizo kutuhumiwa, kwamba ataonekanaje, hataaminika, yeye haoni tatizo. Wao wanaweza kuendelea tu. Na ikitokea Jaji amekataa kujitoa kwenye kesi, huwezi kumtuhumu moja kwa moja.”

Kaiza anazungumzia pia Jaji mmoja kupewa kesi nyingi zinazohusu watuhumiwa wale wale kwa kueleza kuwa hilo linatokea kwa sababu mahakama huangalia ubobevu wao.

“Ninavyojua mimi. Unajua ingawa wote wanaitwa majaji lakini ni kama walivyo madaktari, kila mmoja amebobea katika eneo fulani kwa hiyo kama Jaji kabobea eneo hilo, mahakama inaangalia inampangia kulingana na ubobevu wake.

“Ndiyo maana unakuta Jaji huyo kapangiwa kesi nyingi za aina moja kwa sababu ya ubobevu wake. Ndiyo eneo lake hilo alilobobea,” anasema.

Buberwa alizungumzia pia madai ya baadhi ya watu kuchezea mhimili wa mahakama akieleza kuwa; “Kuna mambo mawili, kwanza mahakama haiwezi kujitibu yenyewe, inapelekewa malalamiko.

“Kuna utaratibu, kama mtu anaona hatendewi haki anaweza kupeleka malalamiko yake kwa Jaji Mfawidhi, yeye ataangalia na anaweza kupandisha malalamiko hayo kwa Jaji Kiongozi ambaye naye akiona ni suala gumu anaweza kupeleka malalamiko hayo kwa Jaji Mkuu.

“Ngazi zote hizo za majaji wana majopo yao. Mtu mmoja haamui kama anavyoona; kuna mashauriano, kukusanya ushahidi na mambo mengine. Sasa kama anayelalamika hajafuata utaratibu wa kuonyesha tatizo lilipo ni vigumu mahakama yenyewe kuona tatizo, inapaswa kupelekewa tatizo husika.

“Hili ulilouliza la mtu anayebainika kucheza na mahakama anaweza kushtakiwa kwa kifungu kipi cha sheria na anaweza kukabiliwa na adhabu gani, siwezi kutaja sheria mahususi.

“Lakini kuna sheria ya kulinda hadhi ya mahakama, inampa mamlaka Hakimu au Jaji kutoa adhabu. Sheria hii ni kwa nchi zote zilizo chini ya ‘commonwealth’ na ndiyo iliyomuhukumu Zuma (Jacob, Rais wa Zamani wa Afrika Kusini). Mahakama ina mamlaka ya kisheria kama mtu ataikosea; ina mamlaka ya kutoa adhabu kwa mtu kulingana na uzito wa kesi husika,” anasema Kaiza.

Wakili Denice Tumaini

Mwingine aliyefanya mahojiano ya Tanzania PANORAMA Blog kuhusu sakata hili ni Wakili na Mbia Kiongozi wa Ubia wa Mawakili wa Lexmicus Attorneys, Denice Tumaini ambaye alianza kwa kuziweka kwenye mizani ya ulinganifu tuhuma zilizotolewa dhidi ya uhalisia wa kilichotuhumiwa.

Wakili Tumaini anasema tuhuma ni mambo ambayo hayajathibitishwa. Inawezekana yana ukweli na inawezekana hayana ukweli.

“Hoja ya msingi katika maswali yako ambayo umeuliza ni watu wenye ukwasi mkubwa ambao wanadaiwa kuchukua mikopo kwenye benki za ndani kutumia muhimili wa mahakama kama kichaka cha kutolipa, tusema ili wasiweze kulipa madeni yao.

“Sasa kwenye kulichambua hilo, ni suala pana kidogo. Linaanzia mbali kidogo kwa maana moja. Mkopo kama mkopo ni mkataba baina ya taasisi ya fedha, iwe ni benki au taasisi ndogo za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania.

“Mkataba wa mkopo una vigezo ambavyo vimewekwa na Benki Kuu. Kwamba unapochukua mkopo lazima uweke dhamana isiyohamishika na dhamana hiyo mtu anaweza kuitoa yeye mwenyewe au akachukua mtu akamdhamini.

“Sasa hapa kuna uhusiano baina ya benki na yule anayechukua mkopo. Unapochukua mkopo ukapeleka dhamana ina maana mkopo upo salama na ili mkopo uwe salama benki; ni lazima upitie Benki Kuu. Hakuna benki yoyote Tanzania inayoruhusiwa kutoa mkopo; ambayo inachukua dhamana ya chini ya kima cha asilimia 130 ya mkopo husika.

“Yaani namaanisha hivi, mfano umeenda benki unataka kuchukua Shilingi milioni moja. Ili wakupe huo mkopo ni lazima uwepe dhamana yenye Shilingi milioni 1.3, kwa maana kwamba kama utashindwa kulipa huo mkopo benki inaweza kuuza dhamana ikapata ile milioni moja waliyokukopesha, gharama za kuiuza na kila kitu kwenye huo mkopo. Hilo ni takwa la kisheria. Sheria ya fedha na miongozo ya Benki Kuu. Na benki zikienda nje ya hapo huwa zinapigwa penati.

Jengo la Benki Kuu ya Tanzania

“Sasa mtu anaposema kuna watu hawataki kulipa kwa sababu wanakimbilia mahakamani ili kukwepa, kidogo inanipa ukakasi. Nitakwambia.”

Akifafanua hilo, Wakili Denice anasema; “Nimekwambia ule ni mkataba, mnaposhindwana kimkataba mnakwenda mahakamani kwa sababu mahakamani mtu yoyote anaruhusiwa kwenda. Katiba inatoa uhuru kwa mahakama kuwa ni chombo ambacho kina mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri mbalimbali kwa mujibu wa kanuni na taratibu.

“Mahakama inatoa haki na pia inawajibisha. Sasa kila mtu anaruhusiwa kwenda mahakamani bila kuangalia hoja aliyonayo ina mashiko kisheria au haina na hakuna Jaji wa Mahakama Kuu, Hakimu Mkazi, Wilaya au Mwanzo anayetakiwa kukurudisha njiani. Wanatakiwa kupokea kila kesi inayofika kwenye meza na kuirekodi kama inavyoripotiwa.

“Baada ya hapo mtu wa upande wa pili, anayelalamikiwa, anapewa nafasi ya kusikilizwa. Sasa mbinu ambayo watu wanasema kwamba inatumika, sijaelewa wanatumia kigezo gani kwa sababu kila kesi, inawezekana zikaonekana zina mfanano lakini lazima kuwe na kitu hata kama ni kidogo ambacho ni tofauti na kesi nyingine.

“Na siyo lazima ukipeleke kesi upewe ushindi hapo hapo. Jaji anaweza kuamua wewe umeshindwa na kama Jaji anaamua hivyo wakati ulitakiwa kushinda, unachotakiwa kufanya; kwanza unakuwa hujaridhika na maamuzi halafu unakata rufaa ngazi ya juu.

“Wanaotoa uamuzi ni binadamu, wengine wanakosea. Wanakose ama kwa kutokufahamu, kwa kutokuwa na uelewa mpana kwa jambo ambalo amelitolea uamuzi au kwa kughafirika kibinadamu.

“Kujibu hoja yako kwamba ninazungumziaje watu ambao wanaitumia mahakama kama sehemu ya kijificha, mimi nitasema kiuanasheria wangu, binafsi sijaona, sijapata ushahidi wa moja kwa moja. Kwa sababu ukishaenda mahakamani, kesi inasikilizwa, uamuzi unatolewa, unaruhusiwa kukata rufaa.

“Sasa nitakwambia kinachotokea. Huwezi kusema ni mahakama inafanya hivyo. sheria zetu zimegawanyika katika makundi mawili. Kuna Sheria zinazotoa haki na wajibu na kuna sheria za mwenendo, kama sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai au kanuni ya mwenendo wa mashauri ya madai.

“Zile sheria mle ndani zina vitu mbalimbali ambavyo vinatakiwa vifuatwe hususan ile kanuni ya mashauri ya madai, kwa mfano; mtu anaweza kufungua shauri leo kuishtaki benki, shauri likifunguliwa kuna kitu kinaitwa ‘technicality’, ushakisia. Sasa wakili anaishi pale.

“Sasa hiyo siyo ‘issue’ ya mahakama, kwa sababau wakili kila anachokiibua mahakamani kama wakili lazima Jaji akisikilize na akitolee uamuzi. Kuna wakili mwingine leo ataibua hili, kesho itabua lile na keshokutwa anaibua jingine.

“Na tukumbuke kwamba majaji hawa, tofauti na nchi za wenzetu ambako unakuta Jaji amekaa tu anasikiliza halafu kuna mtu anamwandikia mwenendo, hapa kwetu Jaji mmoja ndiye anayesikiliza, ndiye anayerekodi, ndiye anayetoa uamuzi wa msingi na uamuzi mdogo na anatakiwa asikilize kila kitu.

“Sasa hapo kwenye lazima kusikiliza ndipo kuna ‘technicality’, kwamba watu wanakuja na mapingamizi yasiyoisha, yasiyokuwa na kikomo, ndiyo maana utakuta kuna kesi zinakaa miaka mitano na zaidi kwa sababu kila mkisonga mbele mtu analeta pingamizi.

“Kwenye utaratibu kama huo nashindwa kusema kwamba mahakama inasaidia watu wasilipe madeni yao. Kanuni yetu na mwenendo wa masuala ya madai, kanuni ya 35 inatoa kitu kinaitwa ‘summary procedure’ ambayo ni mahususi kwa ajili ya mabenki, Taasisi za Serikali kama Tanesco na Shirika la Nyumba la Taifa na hata wenye nyumba za kupangisha

“Hawa wana uwezo, kama wanakudai, wanaweza kwenda kukushtaki mahakamani kwamba wanakudai na wamechukua nyumba yako kama sehemu ya mkopo. Sheria yetu inaruhusu benki kuuza nyumba bila kwenda mahakamani lakini hapo napo, mara nyingi ilikuwa nyumba zikianza kuuzwa mtu anakimbilia mahakamani.

“Sasa ili kuepuka usumbufu na gharama wanawahi kwenda mahakamani kwamba mimi huyu ninamdai na kwa kuwa namdai nataka anilipe hiyo pesa. Yakifanyika maombi ya ‘summary procedure’, yule unayemdai haruhusiwi kuleta utetezi mahakamani mpaka atakapothibitisha kwamba hakukopa huo mkopo au alikopa kisha akalipa. Nje ya hapo, kesi inakuwa imeisha hapo hapo ndiyo maana wameita ‘summary’ kwa sababu haiendi mbali. Nadhani naeleweka vizuri ndiyo maana nasita kukubali kuwa mahakama inahusika hapo.

“Kama kuna matukio hayo, siyo mahakama ni matukio ya mtu mmoja mmoja. Mambo ya mtu mmoja mmoja hayo ni makuzi ya mtu binafsi au tabia, kwenye wengi pana mengi huwezi ukawakosa watu wa aina hiyo. Na itashangaza kuwa na taasisi yenye watu, hivi sasa nadhani wanafika 150 kukosa mmoja mwenye tabia tofauti.

“Sasa hilo sitaki kulileta huko, kwamba ni mahakama. Sisi tupo mawakili elfu 20, wapo watatu au wanne ambao wana mambo ambayo siyo. Zaidi ni kwamba sijajua nani analalamika hapo kwa sababu kama kuna benki ambayo inadai pesa kwa mtu fulani, mkataba wako unasema mtu akulipe ndani ya mwaka na ameshindwa kulipa, wewe ndiyo unatakiwa kwenda mahakamani.

“Kama mtu haendi mahakamani kwa muda unaotakiwa au anakwenda mahakamani lakini hatimizi wajibu wake; mfano benki inaenda kushtaki, wakili anakwenda mahakamani, wakili wa upande wa pili anasema mheshimiwa mimi siwezi kuendelea na kesi nina sababu hii na wakati mwingine siyo sababu za msingi.

“Wakili wa benki badala ya kukataa kuwa sababu iliyotolewa siyo sahihi au haina ushahidi au wakili wa upande wa pili anapaswa kuthibitisha, anasema mimi sina pingamizi,” anapofika hapo Wakili Denice anaweka tuo kwa sekunde kadhaa kisha anaendelea.

“Nikwambie kitu kimoja, Jaji mmoja ana kesi nyingi sana kwa siku moja kwa hiyo ukikosa nafasi leo, akikupa tarehe ya karibu sana kwa kukuhurumia atakupa mwezi mmoja.

“Na siyo makusudi, kumbuka Jaji wetu sisi akitoka kusikiliza kesi anaenda kuandika maamuzi yote. Jaji mmoja anafanya kazi zaidi ya sita au saba kwa wakati mmoja na zote anatakiwa azitengee muda. Kwa hiyo wakili wa benki ndiye mwenye jukumu la kusema sababu iliyotolewa siyo sahihi ili kesi iendelee.

“Na wakati mwingine, wakili wa benki haendi mahakamani anatuma mtu amshikie mikoba, kwa sisi tulio nje tutasema ni mahakama ndiyo ina tatizo lakini huo siyo ukweli wenyewe.

Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma

“Mwaka juzi tulikaa kikao na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama wa Ardhi. Ajenda tuliyoijadili ni namna gani tunaweza kuchechemua uchumi kwa kushughulikia kesi ambazo hazina kichwa wala miguu zinazoletwa na watu ambao wanadaiwa na benki.

“Kwenye kikao kile miongozo ilipitiwa na hasa mwongozo wa Jaji Mkuu unaoelekeza mahakama na majaji kuzipa kipaumbele kesi za benki na mwaka jana na mwaka juzi utaona zilivyoenda.

“Na nakwambia wapo majaji ambao ukifika mbele yao unadaiwa, swali lake la msingi ni kwamba, je unadaiwa? ukisema ndiyo; kwa sababu sheria inamruhusu Jaji kukuhoji, anakwambia kama unadaiwa kabla sijaanza kusikiliza hii kesi tafuta suluhu na huyu mtu muingie makubaliano ya kulipana tofauti na hapo kesi hii siwezi kuiweka kwa sababu hela za watu zinashikiliwa.

“Mimi nimewahi kukusanya madeni ya benki tatu kubwa hapa nchini. Kushinda kesi ya madai ni jambo jepesi sana lakini kukaza hukumu ni jambo gumu sana. Nimekuwa wakili wa Benki ya CRDB, Exim, NBC na nyingine, nimeyafanya haya mashauri kwa kina.”

Wakili Denice pia anazungumzia uamuzi wa Jaji kubatilishwa na jopo la majaji inapotekea kesi husika imekatiwa rufaa mahakama ya juu kwa kusema; “ Tuelewe Jaji ana haki ya kuamua, akasema huna haki, ukakata rufaa Mahakama ya Rufaa ikasema una haki. Haturuhusiwi kumuhukumu Jaji aliyesema huna haki kwa sababu yeye alikuwa na mtizamo wake na ndiyo maana ukitoka Mahakama Kuu kwenda Mahakama ya Rufaa, idadi ya majaji inaongezeka kuwa watatu.

“Pengine huyu mmoja hakuona vizuri, je hawa watatu nao hawataona vizuri? Na kama utakuwa hujaridhika na uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufani, unaweza ukaomba mapitio, ikapitiwa na majaji watano. Haiwezekani Jaji mmoja aone kitu hicho, watatu hivyo hivyo na watano hivyo hivyo.

“Wanaongezwa ili kupunguza makosa ya kibinadamu. Jaji kuamua tofauti na matarajio yako hupaswi kumshambulia Jaji kwa majina yake, unapaswa kuushambulia uamuzi wake kwa kuonyesha matobo kwa sababu hukumu ikishatoka unaruhusiwa kuichukua na kuichambua. Sijaona mtu aliyetoa uchambuzi kama huo.

“Wafanyabiashara kuchelewa kukurudishia hela yako, kwao ni faida. Hiyo ni tabia ya wafanyabiashara wengi. anapokaa na pesa yako anatengeneza faida.

“Kuhusu mawakili. Ipo hivi, wakili anayetetea mtu mwenye kesi kubwa akafanikiwa kumuokoa, watu wengine wote wenye kesi kama hiyo wanamtafuta huyo wakili kwa sababu waamini wakili huyo ndiye anayejua kutetea kesi za aina hiyo. Kwa hiyo siyo jambo la ajabu kumkuta wakili mmoja ana kesi za aina nyingi zinazofanana.”

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya