Tuesday, December 24, 2024
spot_img

SINTOFAHAMU MITAMBO YA KUFUA UMEME KINYEREZI

RIPOTA PANORAMA

KUNA hali ya sintofahamu kuhusu idadi ya mitambo ya kufua umeme iliyopo Kinyerezi, inayozalisha umeme, inayoendelea kujengwa na iliyo katika mipango ya ujenzi.

Sintofahamu hii imekuja baada ya kupatikana taarifa zinazodai kuwa mmoja wa wafanyabiashara maarufu na mwenye ukwasi mkubwa hapa nchini (jina lake tunalihifadhi kwa sasa kwa sababu hajapatikana kuzungumza) amejenga mtambo wake unaozalisha zaidi ya megawati 30 za umeme anazoliuzia Shirika la Ugavi wa umeme (Tanesco).

Mtambo huo, unaodaiwa kupewa jina la Kinyerezi 5 Power Plant ni tofauti na mingine minne inayomilikiwa na Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) na inadaiwa kuwa haukuwa mipango ya serikali kuujenga.

Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vya habari mbalimbali zimedai kuwa mtambo huo ambao tayari unazalisha umeme na kuiuzia Tanesco, hauna mwendelezo mzuri wa uzalishaji umeme.

Inadaiwa kuwa Tanesco imekuwa ikimlipa mfanyabiashara huyo gharama za uzalishaji umeme bila kujali kama mtambo wake uko kwenye hali ya uzalishaji au hauzalishi.

“Inajulikana kwa umma kuwa Kinyerezi kuna mitambo minne ya kufua umeme, kuanzia Kinyerezi ‘one’ hadi ‘four’ lakini ukweli ni kwamba kuna Kinyerezi five, ni mali ya (anamtaja jina). Na analipwa bila kujali kama mtambo wake huo umezalisha umeme au haujazalisha.

“Kapewa miradi mingi sana lakini ni msiri mno na kwenye miradi yake mingine huwezi kukuta jina lake, lakini orodha ya miradi hiyo ipo, ana mtandao mkubwa na anasafiri kwenye ziara za viongozi wa serikali. Yote hayo sawa lakini shida hapa ni kwamba ni kwanini analipwa hata pale ambapo mtambo wake hauzalishi umeme?” Kilidai chanzo kimoja cha habari.

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasialino na Uhusiano kwa Umma wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) Irene Gowelle.

Kupata ukweli wa madai haya, Tanzania PANORAMA Blog, jumatatu wiki hii ilimtafuta Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Kinyerezi 1 Gas Plant, Marco Salu na kumuuliza idadi ya vituo vya kuzalisha umeme vilivyopo Kinyerezi na wamiliki wake.

Salu akijbu, alisema ipo mitambo minne ya kuzalisha umeme katika eneo la Kinyerezi. Miwili, Kinyerezi 1 na Kinyerezi 2 ndiyo inayofanya kazi lakini Kinyerezi 3 na Kinyerezi 4 bado ipo kwenye mipango wa utekelezaji wa ujenzi.

Alipoulizwa kuhusu uwepo wa Kinyerezi 5 unaodaiwa kuwa mali ya mfanyabiashara binafsi, alisema hilo halijua.

Alipoulizwa leo kuhusu hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Tanesco, Irene Gowelle yeye alisema mitambo inayozalisha umeme iliyopo Kinyerezi ni Kinyerezi 1 na Kinyerezi 2.

“Mitambo ya Kinyerezi 1 na 2 inazalisha umeme. Kinyerezi 3 na 4 ipo kwenye mipango lakini hilo uliloniuliza kuhusu Kinyerezi 5 silijua kabisa labda ngoja niulize nikipata majibu nitasema,” alisema Gowelle.

Charles Kitwanga

Naibu Waziri wa Nishati wa zamani, Charles Kitwanga ambaye ndiye aliyezindua mtambo wa Kinyerezi 1, mwaka 2012 amefikiwa na Tanzania PANORAMA Blog na kuzungumza naye; pamoja na mambo mengine aliulizwa kuhusu mpango wa serikali tangu awali wa ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme Kinyerezi.

Kitwanga alisema mpango uliokuwepo ni kujenga vituo kuanzia Kinyerezi 1 hadi 4.

“Mpango wa Serikali ulikuwa kujenga Kinyerezi 1 hadi 4 na Kinyerezi 1 niliizindua mimi nikiwa Naibu Waziri wa Nishati mwaka 2012,” alisema Kitwanga.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa kuna mtambo wa Kinyerezi 5 unaomilikiwa na mfanyabiasha binafsi ambao tayari unazalisha umeme na kuiuzia Tanesco, alisema hilo halikuwa kwenye mpango wa serikali.

Hata hivyo, Kitwanga alisema taarifa kuwa kuna Kinyerezi 5 inayomilikiwa na mfanyabiashara binafsi ambayo tayari inazalisha umeme na kuizuia Tanesco amezisikia lakini hajafika Kinyerezi kuona hali ilivyo na hapo alishauri waandishi na timu nyingine za uchunguzi kwenda Kinyerezi kujionea hali halisi ilivyo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya