Tuesday, December 24, 2024
spot_img

MAWAKILI EQUITY BENKI WALIDAI UWEPO WA ‘UADUI’, ‘UPENDELEO WA WAZI’ – JAJI NANGELA

RIPOTA PANORAMA

JAJI wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, Deo John Nangela alipokuwa akitoa hukumu ya kesi ya kibiashara namba 25 ya mwaka 2021 ambapo wadaiwa waliomba ajitoe kuisikiliza kwa sababu msimamo wake dhidi yao ulikuwa unajulikana, alisema mawakili wa wadaiwa walisema walitambua uwepo wa ‘uadui’ kati yao na Jaji wa kesi.

Jaji Nangela aliyasema hayo Juni 30, 2023 alipokuwa akiendelea kufafanua hoja za mawakili wa wadaiwa; Benki za Equity Tanzania na Equity Kenya waliowasilisha ombi la kumtaka ajitoe kusikiliza kesi namba 25 ya mwaka 2021 iliyofunguliwa na Kampuni za TSN Oil Tanzania, TSN Supermarket, TSN Logistics na TSN Distributers Ltd.

Akiendelea kufafanua barua hiyo ya Mei 12, 2023 ambayo ilipokelewa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara Mei 15, 2023 anasema ili kufafanua zaidi wasiwasi wa wadaiwa, wasilisho la maandishi la mawakili wa wadaiwa linaeleza mshangao wa wadaiwa ni kwanini kesi zote ambazo wanahusika nazo anapewa Jaji mmoja tu wakati kuna majaji wengine wenye uwezo katika kitengo hicho cha Mahakama Kuu.

Jaji Nangela anasema katika hukumu yake hiyo ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona kuwa kwa msingi wa hoja hiyo, imani ya wadaiwa imevurugika na wana hofu iwapo watasikilizwa kwa haki.  

Sehemu ya hukumu ya Jaji Nangela iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza; kwa tafasri isiyo rasmi ya lugha ya Kiswahili inasomeka;

“Ili kuunga mkono hoja hiyo hapo juu, Kamara na Saghan, walitumia Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, kama ilivyorekebishwa mara kwa mara; na walidai kwamba, kama suala la haki, haki sio tu inapaswa kufanywa bali inapaswa kuonekana kufanywa na zaidi ya hayo ni wajibu wa mahakama kuhakikisha kwamba pande zote mbili zinapewa haki ya kusikilizwa kwa haki.

“Walidai kwamba kinachosababisha wasiwasi zaidi kwa wateja wao ni ukweli kwamba, hukumu ya Mheshimiwa Jaji Nangela katika kesi ya NAS Hauliers (supra) inao ushahidi sawa kabisa na ambao uko katika tamko la shahidi ambalo liliwasilishwa katika kesi ya ZAS siku chache kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

Jaji Deo John Nangela

“Ilidaiwa kwamba, ukweli kama huo, kwa maoni ya wadaiwa haionyeshi kuwa ni tukio la bahati mbaya tu.

“Mawakili wasomi wa wadaiwa wamenukuu sheria mbalimbali ili kuunga mkono mawasilisho yao na madai ya wadaiwa. Miongoni mwa hayo ni kesi ya Laurean G. Rugaimukamu dhidi ya Mkuu wa Polisi na wengine, Rufaa ya madai namba 13 ya mwaka 1999.

“Pingamizi dhidi ya Jaji au Hakimu linaweza kuwasilishwa kihalali katika yafuatayo; mosi kuna ushahidi wa uhasama kati ya mhusika katika kesi na Jaji au Hakimu husika na mbili, Jaji ana uhusiano wa karibu na upande pinzani au mmoja wao.

“Tatu kama Jaji au mwanafamilia yake wa karibu ana maslahi katika matokeo ya kesi tofauti na usimamizi wa haki.

“Kesi nyingine iliyotegemewa ni uamuzi wa Mahakama ya Rufaa katika Golden Globe International Services dhidi ya Millicom (T) N.V, rufaa ya madai namba 19/01 ya mwaka 2017. Mawakili wa wadaiwa walidai wakinukuu kutoka uamuzi huu kwamba kutokuwa na sifa kwa afisa wa mahakama kwa upendeleo wa wazi si suala la hiari.

“Mawakili wawili wasomi walisema kwamba wadaiwa wametambua uwepo wa ‘uadui’ kati ya Jaji wa kesi na wadaiwa na ‘upendeleo wa wazi’, hivyo basi kutoa sababu kwa nini Jaji wa kesi anapaswa kujiondoa katika kesi zote zinazohusiana na mashauri yanayowahusu wadaiwa.

“Kueleza dhana ya ‘uadui’ inayojumuisha msaada unaotolewa katika Kamusi ya Kiingereza ya Kimataifa ya Cambridge; Cambridge University Press, 1995 kwenye ukurasa wa 92 ambayo inamaanisha ‘hisia mbaya za chuki na ukosefu wa kuaminiana.’

“Rejea pia ilifanywa kwa Longman Dictionary of Contermporary English, Paul Procter, Ed, 1978, Pitman Press kwenye ukurasa wa 64 ambapo neno ‘uadui’ limefafanuliwa kumaanisha ‘hisia mbaya, hisia za hasira.’

“Kutokana na uelewa huo, mawakili wawili wasomi walihitimisha kwamba pale ambapo upande mmoja unasemakana kuwa na ‘hisia mbaya’ au ‘hisia za chuku’ au ambapo yeye huonyesha ‘ukosefu wa kuaminiana’ mtu huyo anasemekana kuwa na hisia mbaya dhidi ya upande pinzani.

“Kurejea kifungu cha saba cha barua ya wadaiwa, mawakili wasomi wa wadaiwa walidai kwamba jambo linaonyesha uwepo wa ‘uadui’ au ‘hisia mbaya’ au ‘hisia za hasira’ au ‘ukosefu wa kuaminiana’ dhidi ya Jaji wa kesi na kinyume chake hali ambayo inaathiri vibaya kanuni za kusikilizwa kwa haki.

“Pia walitumia kesi ya Laurean Rugaimukamu kuhusu upendeleo wa wazi. Mawakili wa upande wa wadaiwa walisema kuna ubaguzi wa wazi na kama ilivyo kwenye barua yao kuwa Jaji wa kesi alitoa maoni hasi kuhusu mshtakiwa wa pili kwamba hawakutaka kusuluhisha mgogoro wao hivyo benki unajua walichofanya.”

Hukumu hii ilitolewa na Jaji Nangela baada ya wadaiwa; Benki za Equity Tanzania na Equity Kenya kuiandikia barua Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara kuomba Jaji Nangela ajitoe kusikiliza kesi namba 25 ya mwaka 2021 iliyokuwa imefunguliwa na Kampuni za TSN dhidi ya benki hizo.

Kwa upande mwingine, Tanzania PANORAMA Blog inaripoti hukumu hii na itaripoti hukumu nyingine zinazohusu kampuni zinazodaiwa kukopa mabilioni ya fedha kwenye benki za ndani na kukataa kulipa kwa kukimbilia mahakamani kama moja ya jukumu lake la msingi la kupasha habari umma.

Kwa mara ya kwanza, madai kuwa zipo kampuni zinazomilikiwa na baadhi ya wafanyabiashara wa ndani zilizokopo mabilioni ya fedha kisha kukataa kulipa kwa kukimbilia mahakamani ziliibuliwa kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kisha kuibua mijadala mikali inayohusisha makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo wanasheria.

Farouq Baghoza

Kati ya Kampuni zilizotajwa kwenye madai hayo ni TSN Group iliyodaiwa kukopa Shilingi bilioni 15 kutoka Benki ya National Micro finance Bank (NMB) na Shilingi bilioni 80 kutoka Benki ya Equity kwa utaratibu wa kudhaminiwa (letter of credit); fedha ambazo imekataa kulipa kwa kukimbilia mahakamani ambako ilipewa ushindi.

Tanzania PANORAMA Blog imemfikia bosi wa TSN Group, Farouq Baghoza kwa njia ya simu yake ya kiganjani na kumuuliza pamoja na mambo mengine kuhusu jina lake kutajwa moja kwa moja kwenye madai hayo lakini ‘alikacha’ kujibu swali hilo.

Katikati ya habari hii, Tanzania PANORAMA Blog itaripoti mahojiano iliyofanya na baadhi ya wanasheria waliozungumza lugha ya kisheria dhidi ya skandali hii iliyopewa jina la mikopo chefuchefu kabla ya jumatatu itakapoendelea kuripoti hukumu hii.       

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya