Tuesday, December 24, 2024
spot_img

WATAALAMU POSTA AFRIKA WASHAURIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA

MWANDISHI WETU – WHMTH

Arusha

WATAALAMU wa Posta Afrika wameshauriwa kutumia maendeleo ya teknolojia ili yaiwezeshe sekta hiyo kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuongeza kasi ya ukuaji uchumi.

Ushauri huo ulitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Mzee Suleiman Mndewa alipokuwa akifungua vikao vya kamati za wataalamu wa masuala ya Posta wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU).

Vikao hivyo ni vya utangulizi kabla ya Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la PAPU linalotajiwa kuketi kwa siku mbili, Juni 11 hadi 12 mwaka huu Jijini Arusha.

Akizungumza katika hotuba yake ya ufunguzi wa vikao hivyo, Dk. Mndewa alisema ili Nchi za Afrika zifanikiwe katika masuala ya Posta na kuendana na kasi ya ukuaji wa biashara mtandao, ni wajibu wa wataalamu wa nchi wanachama kushiriki katika uchumi wa kidijitali.  

“Kupitia mkutano huu ni wajibu wenu kuhakikisha mnatafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokabili nchi wanachama kwa sababu changamoto bado zipo katika Nchi za Afrika, ikiwemo miundombinu na teknolojia ambavyo vinahitaji kupatiwa ufumbuzi ili kurahisisha mawasiliano,” alisema Dk. Mndewa.

Katibu Mkuu huyo alisema Nchi za Afrika zinapaswa kutumia teknolojia ili kupunguza gharama na kutimiza malengo ambayo nchi zimejiwekea.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Salome Kessy aliwataka washiriki wa vikao hivyo kuhakikisha majadiliano yao yanazaa matunda na ushauri wao uwe na matokeo chanya.

“Tushirikiane kwa pamoja kutumia uwezo wa Sekta ya Posta kuhakikisha tunajenga mustakabali wa kidijitali, jumuishi na endelevu kwa manufaa ya waafrika wote,” alisema Salome.

Salome alitumia fursa hiyo kupigia chapuo utalii alipowaalika washiriki wa mkutano huo kufurahia mandhari ya Jiji la Arusha na viunga vyake na pia kuitumia vizuri nafasi ya uwepo wao nchini kutembelea vivutio vya utalii zikiwemo mbuga za wanyama.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa PAPU, Dk. Sifundo Chifu Moyo alisema zipo changamoto kadhaa zinazokabili Sekta ya Posta zinazowafanya wateja kutokuwa na furaha ingawa hivi sasa viongozi wa Nchi za Afrika wameanza kuzitafutia ufumbuzi.

Alitaja moja ya changamoto hizo kuwa ni kutikisika kwa mauzo ya hisa katika soko na kushuka kwa mapato hivyo vikao vya kamati hizo  za wataalamu vinatarajiwa kutoa majibu ya namna teknolojia inavyoweza kuwa suluhu ya changamoto hizo ili kurejesha imani ya wananchi katika sekta hiyo.

“Kama wote mnavyoelewa, teknolojia haimilikiwi na mtu yeyote, kwa hiyo kila mmoja anayo fursa ya kuitumia vizuri teknolojia ili kujikwamua kiuchumi na Sekta ya Posta haipaswi kuwa nyuma. Kwa sasa Posta inaichukulia teknolojia kwa uzito mkubwa na ipo kwenye sera zake na ina hakikisha inapeleka teknolojia karibu zaidi na wananchi,” alisema Dk. Moyo.

Alielezea furaha yake kwa mkutano huo kufanyika kwenye jengo la PAPU ambalo ni moja ya vitega uchumi vyake na kielelezo cha uwepo wa umoja huo. Alisema ilikuwa na ndoto ya miaka 40 kwa PAPU kuwa na jengo lake hivyo ni jambo la furaha ndoto hiyo kutumia.

Maharage Chande

Awali, Postamasta Mkuu, Maharage Chande alisema mchango wa Posta ni kuhakikisha sheria, kanuni na sera zinasaidia kufanya maboresho mbalimbali katika Sekta ya Posta sambamba na kusaidia biashara na uchumi katika Nchi za Afrika.

“Tunataka kuzungumza kwa karibu na kuangalia namna tutakavyoweza kufanya biashara kwa urahisi kutoka Kusini kwenda Kaskazini. Mtagundua biashara kubwa inatoka Kaskazini yaani nchi za Ulaya kuja Kusini, lakini lazima tuondoke kwenye utaratibu huo na tunataka kuhakikisha kanuni zinafuatwa katika kufanikisha biashara hiyo,” alisema.

Chande alisema ili kufanya maboresho katika masuala ya bima, Posta kwa sasa inasisitiza matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelgence), na jitihada za makusudi zinafanyika ili kuachana na utaratibu wa zamani wa kutuma barua kwa mkono hivyo hatua zinachukuliwa kwenda sambamba na teknolojia ya sasa.

“Sekta ya Posta bado ina mchango mkubwa katika uchumi na maendeleo kwa kuzingatia masuala ya utawala ikiwemo ajenda ya kupokea na kufanyia kazi matumizi ya akili mnemba yaani (Artificial intelligence). Katika hali hiyo ipo haja kwa mataifa haya kuzidi kuimarisha shughuli za kibiashara ili kukuza uchumi,” alisema Chande.

Vikao vya kamati za wataalamu wa masuala ya Posta, ni utangulizi wa Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika ukiwakutanisha wataalamu mbalimbali kutoka mataifa zaidi ya 30 wanaojadili mikakati, kanuni na sera za kuboresha sekta hiyo kwa manufaa ya mataifa wanachama.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya