Monday, December 23, 2024
spot_img

HUKUMU YA JAJI NANGELA AKIKATAA KUJITOA KESI YA TSN GROUP DHIDI YA BENKI ZA EQUITY

RIPOTA PANORAMA

Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, Deo John Nangela, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 25 ya mwaka 2021 aliyofunguliwa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara na Kampuni za TSN dhidi ya Benki za Equity alitoa hukumu dhidi ya maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wadaiwa, wakiomba ajitoe kuisikiliza kwa sababu msimamo wake dhidi yao ulikuwa unajulikana.

Hukumu hiyo aliitoa Juni 30, 2023 ambapo katika kesi ya msingi namba 25 ya mwaka 2021 mdaiwa wa kwanza alikuwa Benki ya Equity Tanzania na mdaiwa wa pili Benki ya Equity Kenya huku mdai wa kwanza akiwa Kampuni ya TSN Oil Tanzania Limited, mdai wa pili TSN Supermarket, wa tatu TSN Logistics na wa nne TSN Distributors Limited.

Akisoma hukumu yake, Jaji Nangela alisema uamuzi wake unatokana na barua ya wadaiwa ya Mei 12, 2023 iliyokuwa na kichwa cha habari, “Maombi ya kutojihusisha katika usikilizaji shauri,” iliyopokelewa mahakamani hapo Mei 15, 2023.

“Kama kichwa cha habari kinavyoonyesha, wadaiwa wanaomba mimi kujiondoa kama Jaji niliyeko katika shauri la biashara namba 25 la mwaka 2021, shauri ambalo uamuzi huu unahusiana nalo na shauri la biashara namba 103 la mwaka 2022 kati ya ZAS dhidi ya Equity Benki Tanzania na Equity Benki Kenya, wadaiwa katika shauri hili. 

“Shauri ambalo pia linaendelea mbele yangu na mashauri mengine yajayo ambayo wadaiwa wanaweza kuhusika nayo. Na kwanini ombi hili? Hilo nitalifafanua kwa ufupi kutoka kwenye barua yao,” inasomeka sehemu  ya hukumu hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona.

Akifafanua hilo katika hukumu yake, Jaji Nangela anaeleza kuwa katika barua ya wadaiwa, wameweka malalamiko kadhaa kama sababu au msingi wa ombi lao la kutaka yeye kujiondoa na kwamba malalamiko yao yamefafanuliwa vema zaidi kwenye aya ya pili hadi ya tisa.

Akirejea barua hiyo, Jaji Nangela anasema wadaiwa wameeleza kuwa imebainika kuwa ni yeye aliyesikiliza shauri la biashara namba 105 la mwaka 2021 lililofunguliwa na NAS Hauliers Limited na wengine wawili dhidi ya wadaiwa wale wale katika shauri lililo mbele yake ambapo hukumu ilitolewa dhidi ya wadaiwa.

Anaendelea kuirejea kuwa imebainika anasikiliza mashauri yaliyoainishwa juu ya barua hiyo  yaliyo katika hatua mbalimbali za usikilizaji na kwamba anasikiliza mashauri matatu yanayofanana dhidi ya wadaiwa wale wale katika kitengo kimoja cha mahakama kuu, jambo linalowapa wasiwasi mkubwa.

Jaji Nangela anaendelea kurejea barua ya wadaiwa wakieleza kuwa wana mashaka makubwa kama hilo limefanywa kwa makusudi au kwa bahati mbaya hasa ikizingatiwa kwamba kuna majaji wengine wenye uwezo katika kitengo hicho cha mahakama kuu.

Akirejea aya ya tano ya barua ya wadaiwa katika hukumu yake Jaji Nangela anasema walieleza kuwa mnamo Aprili 19, 2023 katika kesi ya NAS Hauliers dhidi ya benki hizo kwa msingi wa kushangaza alihukumu kesi ya ZAS na NAS Hauliers dhidi ya wadaiwa hao na kwamba atakuwa na msimamo huo huo hivyo hakuna maana ya kesi kama pande zinajua msimamo wa mahakama hata kabla ya kuanza kusikilizwa. 

Akiendelea, Jaji Nangela anaeleza kwamba wadaiwa walieleza kuwa katika kesi ya NAS Hauliers Limited dhidi ya benki mbili za Equity alitoa hukumu dhidi ya benki hizo kwa misingi wanayohisi ni ya kushangaza na kwamba wanatarajia atadumisha msimamo huo jambo ambalo linapunguza imani yao kwake.

Sehemu ya hukumu ya Jaji Nangela iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza, kwa tafasiri isiyo rasmi ya lugha ya Kiswahili inasomeka; “Wakati kesi ya ZAS ilipoitishwa kwa ajili ya kutayarisha hoja bishaniwa, ulilalamika waziwazi mara mbili kwamba ilikuwa ni Equity Benki ya Kenya ambayo haikutaka kumaliza mzozo na hata benki zinajua walichofanya. Baada ya maoni yako mabaya uliamua kesi ya NAS Hauliers dhidi ya benki.

“Pia tumefahamishwa kuhusu hukumu yako ya tarehe 18 Aprili, 2023 kwenye shauri la Kilimanjaro Oil Company dhidi ya KCB Benki ya Tanzania na KCB Benki ya Kenya ambayo ukweli wake ni sawa na kesi zilizotajwa katika barua hii. Katika shauri hilo tena uliamua dhidi ya Benki ya KCB.

“Kwa kuzingatia kufanana kwa masuala na mambo mengine yanayobishaniwa, tunaamini kwa nguvu kuwa hukumu kuhusu mashauri haya mawili itatolewa dhidi ya wadaiwa wa sasa kwa namna au mtindo unaofanana. Mawazo na msimamo wa mheshimiwa ni wazi na tunajua; hivyo kupunguza asili, maana na dhamira ya haki kutendeka mahakamani.

“Kwa hiyo, na ili kuhakikisha haki inatendeka waziwazi, tunaomba ujiondoe na ujitenge mwenyewe na kuacha kuamua mashauri haya mawili yaliyofunguliwa na TSN Group na ZAS dhidi ya wadaiwa na kuruhusu Jaji mwingine mwenye mawazo mapya kukamilisha na kuamua mambo haya badala yako.

“Tunaelewa kuwa hili ni suala gumu kutokana na hatua ambayo shauri limefikia lakini hatuna chaguo jingine zaidi ya kuomba ujitoe wewe mwenyerwe katika shauri hili.”

Tanzania PANORAMA Blog itaendelea kuripoti hukumu hii na nyingine zilizoibua mjadala mkubwa kwenye jamii dhidi ya kampuni kubwa zinazodaiwa kukopa mabilioni ya fedha benki na kukataa kulipa kwa kukimbilia mahakamani.

Wakati huo huo, mjadala kuhusu kampuni zinazodaiwa kukopa fedha nyingi benki kisha kukataa kulipa umeanza pia kuwaibua baadhi ya wanasheria kuzizungumzia na Tanzania PANORAMA Blog itaripoti maoni yao.

Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii lilisambaa andiko lililotaja baadhi ya kampuni na wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa kukopa pesa benki ya kukataa kulipa kwa mtindo wa kukimbilia mahakamani kabla ya kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Andiko hilo lilizitaja kampuni hizo, benki husika, wakili mmoja anayedaiwa kusimamia kesi hizo mahakamini na Jaji ambaye kesi nyingi za aina hiyo hupelekwa mbele yake.

Lilienda mbali zaidi kwa kudai kuwa tafsiri ya skandali hiyo ni fedha za mitaji ya watu wa chini zinatumika kunufaisha watu wachache wanaojua kucheza na mahakama.

Farouq Baghoza

Aidha, lilidai kuwa Benki ya Azania ambako kumechotwa  mabilioni na baadhi ya kampuni hizo inamilikiwa na taasisi za umma hivyo wakopaji wanaokopa kwenye benki hiyo kisha kukataa kulipa wanatafuna fedha za umma.

Tayari Tanzania PANORAMA Blog imekwishamfikia kwa simu yake ya kiganjani bosi wa Kampuni za TSN, Farouq Baghoza na kumuuliza kuhusu jina lake kutajwa moja kwa moja kwenye skandali hiyo lakini ‘alikacha’ kujibu swali hilo.   

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya