MASHIRIKA YA HABARI YA KIMATAIFA
RAIS wa zamani wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma amezuiwa na Mahakama ya Juu ya Kikatiba ya nchi hiyo kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Vyombo vya habari vya Afrika Kusini na Mashirika ya Habari ya Kimataifa, jana yaliripoti kuwa hukumu ya kumzuia Zuma kugombea ubunge ilitolewa na Jaji wa Mahakama ya Juu ya Kikatiba ya Afrika Kusini, Leona Theron.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Theron alisema kifungo cha miezi 15 jela alichohukumiwa Zuma mwaka 2021 baada ya kukutwa na kosa la kupuuza amri ya mahakama ni uhalifu chini ya sheria za Afrika ya Kusini.
Alisema Zuma alikutwa na hatia ya kukataa kutoa ushahidi kwenye kesi ya ufisadi uliotokea wakati akiwa Rais.
Zuma amekuwa akifanya kampeni kwa tiketi ya Chama cha Umkhonto weSizwe (MK) baada ya kufarakana na chama tawala cha African National Congress (ANC).
Mawakili wa Zuma waliiambia mahakama kuwa aliachiwa kutoka gerezani na Rais Cyril Ramaphosa baada ya kutumia kifungo kwa muda wa miezi mitatu hivyo kifungo chake kilichosalia kilifutwa.
Mahakama ilikataa utetezi huo kwa maelezo kuwa urefu wa muda aliokaa gerezani haukuwa na maana kwani Katiba ya Afrika Kusini inapiga marufuku mtu yoyote aliyehukumiwa kifungo cha miezi 12 gerezani bila kulipa faini kuwa mbunge ili kulinda uadilifu kwa viongozi wa umma.
Akizungumza baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Katibu Mkuu wa MK, Sihle Ngubhane alisema chama chake kimesikitishwa na uamuzi huo wa Mahakama ya Juu ya Kikatiba lakini hautathiri kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa wiki ijayo.
Alisema jina a Zuma litaendelea kubaki kwenye karatasi za kupigia kura kwa sababu bado ni kiongozi wa Chama cha MK.
Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini imesema jina la Zuma litaondolewa kwenye orodha ya wagombea ubunge lakini sura yake itasalia kwenye karatasi za kupigia kura.