MASHIRIKA YA KIMATAIFA
RAIS wa Iran, Ebrahim Rais aliyefariki dunia jumapili, Mei 19, 2024 kwa ajali ya helikopta huko Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo, anatarajiwa kuzikwa leo.
Helikopta iliyokuwa imembeba Rais Raisi ilipata ajali alipokuwa akitokea Mji wa Tasnim, ulio mpakani na Azerbaijan na kuua watu wote aliokuwa akisafiri nao akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje, Hossein Amir Abdollahian.
Kwa mujibu Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kabla ya kuzikwa, mwili wa Rais Raisi pamoja na aliokuwa akisafiri nao itafanyiwa uchunguzi na wataalamu wa uchunguzi katika Mji wa Tibriz.
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei amekaririwa na vyombo vya habari vya kimataifa akitangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa na amemuidhinisha Makamu wa Rais, Mohammad Mokhber kuwa Kaimu Rais.
Baraza la Mawaziri la Iran limemteua Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ali Baghari Kani kuwa Waziri wa Mambo ya Nje akichukua nafasi ya marehemu Abdollahian.
Rais Raisi alikuwa akitazamwa na wengi kama mtu ambaye angefaa kuchukua nafasi ya Kiongozi Mkuu wa Iran kutoka kwa Ayatollah Khamenei mwenye umri wa miaka 85 sasa.
Kifo cha Rais Raisi hakitarajiwi kubadilisha mwelekeo wa sera ya Iran au kuitikisa kwa namna yoyote lakini wafuatiliaji wa mambo wameeleza Iran inaweza kuingia majaribuni kutokana na kile kilichoonyeshwa na wapinzani wa Raisi kama ni kushangilia kifo chake.