Monday, December 23, 2024
spot_img

MPINA AKOA MANZA BUNGENI

RIPOTA PANORAMA

BUNGE limeelezwa kuwa tangazo lilitolewa Disemba 15, 2023 na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo la kufuta Mashirika na Taasisi za Umma na mengine kuunganishwa halina msingi wa kisheria.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina aliyasema hayo Mei 13, 2024 alipokuwa akichangia Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/205 iliyosomwa bungeni na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Mpina alisema Bunge halikushirikishwa kwenye uamuzi wa kufuta na kuunganisha mashirika hayo na kwamba Aprili 22, 2024 Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alitoa mwongozo bungeni kuwa Mashirika na Taasisi za Umma zilizoanzishwa kwa sheria iliyotungwa na Bunge, hayawezi kufutwa au kuunganishwa nje ya utaratibu wa Bunge.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

Mpina aliishauri Serikali kufuta tangazo lilitolewa na Waziri Mkumbo ili kuruhusu Taasisi na Mashirika ya Umma yanayokusudiwa kuunganishwa na kufutwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria hadi hapo itakapoamriwa vinginevyo.

Akizungumzia athari za tangazo hilo la Waziri Mkumbo, alisema limesababisha Mashirika na Taasisi za Umma 20 kushindwa kuweka na kutekeleza mikakati, mipango na programu za kila mwaka na watumishi wa mashirika na taasisi zilizotajwa hawajui hatma yao.

Mpina aliitaja Taasisi ya Chakula na Lishe ambayo kwa lugha ya kimombo inaitwa Tanzania Food and Nutrition Centre (TFNC) iliyotajwa na Waziri Mkumbo kwenye orodha ya Taasisi na Mashirika ya Umma yanayopaswa kufutwa na kuunganishwa kuwa haipaswi kufutwa kwa sababu ya umuhimu wake kwa taifa na kimataifa.

Alisema TFNC inafanya tafiti nyingi za lishe, ina maabara ya kipekee katika Bara la Afrika inayofanya uchunguzi na uchambuzi wa viashiria vya lishe kwa kutumia sampuli za chakula na kibailojia ambayo inaaminika na Shirika la Chakula Duniani (WHO), Shirika la Kudhibiti Magonjwa ya Maambukizi barani Afrika (CDC) na Shirika la Maendeleo ya Kiserikali Afrika Mashariki (IGAD).

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

“Pia taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu ya lishe kwa umma. TFNC ina mikataba na baadhi ya nchi kadhaa barani Afrika, Ulaya Mashariki na Mashariki ya Kati inayohusu huduma za uchunguzi lishe wa kimaabara,” alisema Mpina.

Akiendelea kuchangia, Mpina alisema baada ya tangazo la kufutwa kwa taasisi hiyo, mashirika ya kimataifa ambayo ni wadau wa maendeleo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WFP) na mengine yamesita kueleza ushiriki wao kwenye kuchangia Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa ajili ya kusaidia programu za lishe.

Alisema mashirika hayo ya kimataifa huwa yanachangia zaidi ya Shilingi bilioni nane katika Bajeti ya Serikali kila mwaka.

Alisema kuanzia Julai Mosi, 2024, TFNC haitakuwa na fedha za kutekeleza majukumu yake ya msingi na kuhoji majukumu hayo yatatekelezwa na nani.

“Hivi sasa shughuli za TFNC zinasuasua kutokana na kutojulikana hatma ya taasisi hiyo na hivyo kushindwa kuweka na kutekeleza mipango na program zinazofanywa na taasisi hiyo kila mwaka.

“Sintofahamu hii iliyopo ya kutangazwa kufutwa kwa taasisi hii inaweza kusababisha kuvunjika kwa mikataba hiyo na hivyo kuharibu uhusiano wa kidiplomasia na nchi husika lakini pia nchi kukosa manufaa ambayo ilikuwa inapata kupitia mikataba hiyo,” alisema Mpina.

TFNC ilianzishwa na sheria ya Bunge, namba 24 ya mwaka 1973. Iko chini ya Wizara za Afya na sekretariati ya National Multi sectoral Nutrition Action Plan 2021/2022 hadi 2025/26 chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo (kushoto) akiwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu.

Disemba 15, 2024, Waziri Mkumbo akiwa ameambatana na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alikutana na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kutangaza kuwa Serikali imeamua kufuta na kuunganisha Mashirika na Taasisiza Umma 20.

Waziri Mkumbo aliwataka mawaziri kutekeleza agizo hilo ndani ya mwaka wa fedha wa 2023/2024.

Alisema uamuzi wa kufutwa na kuunganishwa kwa mashirika na taasisi hizo umefikiwa baada ya tathimini ya utendaji wake iliyofanywa na timu ya wataalamu wa serikali.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya