RIPOTA PANORAMA
‘UNAJUA nyota ngapi zamulika usiku huhesabu na mawingu yanayosafiri juu, Mungu anajua yote aongoza viumbe vyote, kaa akili uake kuu,’ na ‘Twinkle twinkle little star, how i wonder what you are, up above the world so far like diamonds in the sky.’
Hizi ni nyimbo mbili ambazo watalii wa ndani na kutoka nje ya nchi wanaweza kuimba wakikumbuka maisha yao ya shule wanapokuwa wakitizama mamilioni ya nyota angani wakiwa eneo maalumu lililopo Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato. Eneo hili linamuwezesha mtalii kuona vizuri nyota angani pasipo kutumia darubini.
Uhalisia wa nyimbo hizo mbili unajieleza kwa mtalii anayetembelea Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato kwani uzuri wa hifadhi hii na vivutio ilivyonavyo huleta hisia kwa mtalii ya namna uumbaji wa Mungu ulivyo wa ajabu.
Kaimu Mhifadhi, Kitengo cha Utalii anayesimamia Sayansi ya Uhifadhi (Ikolojia), Mhifadhi Daraja la Pili wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato, Leticia Magesa.
Kaimu Mhifadhi, Kitengo cha Utalii anayesimamia Sayansi ya Uhifadhi (Ikolojia), Mhifadhi Daraja la Pili wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato, Leticia Magesa anaeleza kuwa katikaeneo maalumu ambalo mgeni anaweza kutazama nyota usiku, anga linaonekana vizuri hivyo mtalii hahitaji darubini kuzitazama.
Anasema kwa watalii wa ndani hususani wanafunzi wanaofanya ziara za kimasoma, eneo hilo linafaa zaidi kwao kwa sababu linatoa fursa ya kujifunza na kuuona uzuri wa nchi yao hivyo kuwajengea moyo wa kuipenda.
Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato pia ina mandhari nzuri za maumbile ya hali ya nchi yenye milima na mabonde. Humo wametapakaa wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo wanyama adimu ambao hawapatikani kwenye hifadhi nyingine.
Tayari imethibika kuwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato ndiyo pekee hapa nchini yenye wanyama aina ya mbega wenye rangi ya kijivu na nyekundu, na ndiyo eneo pekee duniani lenye wanyama wengi wa aina hiyo, likiwa na asilimia 20 ya wanyama wote wa aina hiyo duniani.
Mbega mwenye rangi ya kijivu na nyekundu anayepatikana kwenye Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato. Asilimia 20 ya wanyama hawa waliopo duniani wapo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato.
Mnyama mwingine adimu anayepatikana Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato ni mbuzi mawe. Mbuzi mawe hawaonekani kwa wingi katika maeneo mengine isipokuwa kwenye hifadhi hii ambako mtalii anaweza kuwaona kwa karibu.
Wanyama aina ya Mbuzi mawe ambao wanapatikana kwa wingi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato.
Magesa anaeleza kuwa Hifadhi ya Taifa Burigi – Chato ni makazi ya aina nyingi za ndege akiwamo ndege anayefahamika kwa jina la domo kiatu ambaye kwa sasa haonekani lakini zipo dalili kuwa alipata kuwepo kwenye hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato.
Anasema tafiti zinaonyesha ndege huyo alitoweka kutokana na usumbufu na hivi sasa wataalamu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wanafanya utafiti kubaini kama bado yupo au alikwitoweka.
Aidha, Magesa anaeleza kuwa mtalii anayetembelea Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato anaweza kupata mlo wa usiku wa kipekee akiwa mbugani. Anasema hiyo ndiyo sehemu pekee inayoweza kumpa mtalii uzoefu wa kipekee hasa kwa watu wenye matukio ya kumbukumbu muhimu kwenye maisha yao.
Sambamba na mazuri yote hayo katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato, pia kuna utalii wa kutembea kwa miguu. Utalii wa aina hii unafaa kwa watu wote wakiwamo wagonjwa kwani unawasaidia kufanya mazoezi.
Utalii wa kutembea kwa miguu kwenye hifadhi unafanyika katika maeneo machache ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato na hii kwa sababu inahitaji maeneo maalumu na yenye usalama wa kutosha kwa watalii kutembea wakipishana na wanyama wa aina mbalimbali kwa karibu.
Tembo wanaopatikana Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato.
Katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato, njia za utalii wa kutembea kwa miguu zimetengenezwa zikiwa na urefu wa kilimita mbili mpaka tano na zimetengenezwa katika maeneo tofauti tofauti ili kumuwezesha mtalii kuona mandhari nzuri ya hifadhi.
Magesa anasema njia za utalii wa kutembea kwa miguu zimetengenezwa kwenye maeneo ya milimani, mabonde na kando kando ya ziwa ili kutoa fursa kwa mtalii kujionea mandhari ya hifadhi vizuri zaidi na kwamba mtalii anayo fursa ya kuamua atembee umbali gani na katika njia anayoitaka.
Anasema njia za utalii wa kutembea kwa miguu zimetengenezwa kwenye maeneo ambayo hakuna wanyama wakali hivyo mtalii hawezi kuogopa kushambuliwa na wanyama.
Aina nyingine ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato ni utalii wa boti inayofahamika kama boat safari.
Aina hii ya utalii inamuwezesha mtalii kufanya uvuvi wa ndoano huku akiangalia wanyama na mandhari nzuri ya hifadhi hiyo.