Saturday, April 19, 2025
spot_img

DUNIA YATAZAMA HIFADHI YA TAIFA BURIGI – CHATO

RIPOTA PANORAMA

DUNIA imeanza kuitazamana Hifadhi ya Taifa ya Burigii – Chato kwa namna ya pekee baada ya kugundulika kuwa, asilimia 20 ya wanyama aina ya mbega wenye rangi ya kijivu na nyekundu waliopo duniani, wanapatikana kwenye hifadhi hiyo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri) ikishirikiana na watafiti wa masuala ya nyani kutoka Uganda, wanyama hao ambao kwa lugha ya kimombo wanafahamika kwa jina la ‘ashy red colobus monkey’; katika Hifadhi za Taifa 21 zilizopo nchini, Hifadhi ya Burigi – Chato ndiyo pekee yenye wanyama hao.

Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato anayeshughulikia Uhusiano wa Jamii, Utumishi na Utawala, Ombeni Hingi amezungumzia uwepo wa wanyama hao kwenye hifadhi hiyo kulivyoifanya kuwa ya kipekee nchini na katika uso wa dunia pamoja na mtizamo wa watafiti wa wanyama wa kimataifa walioonyesha nia ya kuifikia ili kufanya utafiti wa kina kuhusu wingi wa wanyama hao hifadhini hapo.

Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato anayeshughulikia Uhusiano wa Jamii, Utumishi na Utawala, Ombeni Hingi

Katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu hifadhi hiyo kuwa na mbega wenye rangi ya kijivu na nyekundu wengi kuliko maeneo mengine duniani; pamoja na mambo mengine; Hingi anaeleza kuwa ubunifu na uthubutu wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kutengeneza filamu ya Royal Tour ni moja ya mambo yaliyowavuta watafiti wa mambo ya uhifadhi na wanyama kuitizama Tanzania kwa jicho la pekee lililobaini hifadhi hiyo kuwa makao makuu ya mbega wenye rangi ya kijivu na nyekundu duniani.

Haina shaka, ugunduzi huo utavutia watafiti wengi zaidi wa kimataifa wa mambo ya uhifadhi na wanyama kufika kwenye hifadhi hiyo kufanya utafiti wao na pia ni fursa kwa watafiti wa ndani kufanya utafiti wa kina kuhusu eneo hilo kuwa makao makuu ya mbega wenye rangi ya kijivu na nyekundu ambao unaweza kuzidi kuipaisha Tanzania kwenye uso wa dunia na kuchangia kuinua soko la utalii.   

“Hifadhi ya Burigi – Chato ni makao makuu ya wanyama aina ya mbega wenye rangi ya kijivu na nyekundu duniani ikiwa na asilimia 20 ya wanyama wote wa aina hiyo waliopo kwenye uso wa dunia. Na katika ukanda wa Afrika Mashariki, wanyama hao wanapatikana pia kwenye hifadhi moja iliyopo nchini Uganda,” anasema Hingi na kuongeza;

“Ni hifadhi ya kipekee sana kwani pamoja na kuwa na wanyama hao kwa wingi, pia ina mandhari nzuri na wageni wanaoitembelea wanayo fursa ya kukutana na wanyama walio katika kundi la wanyama linalojulikana kama ‘big five.’”

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mtayarishaji wa filamu ya The Royal Tour, Peter Greenberg alipokuwa akitengeneza filamu hiyo

Kundi la wanyama wanaojulikana kama ‘big five,’ linajumuisha simba, tembo, nyati, chui na faru. Hingi anasema katika hifadhi hiyo ni faru pekee ambaye hayupo hivyo mgeni anayetembelea Hifadhi ya Burigi – Chato, mbali na kupata fursa ya kuona maelfu ya familia za mbega wenye rangi ya kijivu na nyekundu pia anaweza kuwaona wanyama hao wakubwa na adimu duniani.

Hingi anasema Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato ilianzishwa kwa tangazo la serikali namba 508, mwaka 2019 baada ya kupandishwa hadhi mapori ya akiba matatu; mapori hayo ni Kimisi, Burigi na Biharamulo.

Anasema hifadhi ina ukubwa wa kilomita za mraba 4707 na ni miongoni mwa hifadhi kubwa nchini ikishika nafasi ya nne kati ya Hifadhi za Taifa 21 zilizopo nchini zinazosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Kwa mujibu wa TANAPA. Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato inatanguliwa kwa ukubwa wa eneo na Hifadhi za Taifa za Nyerere, Ruaha na Serengeti na serikali iliamua kuipandisha hadhi kuwa Hifadhi ya Taifa ili kunusuru viumbe wa pekee walio kwenye hifadhi hiyo pamoja na kutunza Ikolojia yake muhimu.

FURSA ZA UWEKEZAJI

Twiga; wanyama wenye umaarufu na sifa kubwa duniani ambao wanapatikana kwenye Hifadhi ya Taifa ya Burigi- Chato.

Hingi anasema Hifadhi ya Burigi Chato ina fursa nyingi za uwekezaji na tayari; kwa kiasi kikubwa serikali imeishafungua barabara za ndani ya hifadhi na barabara kuu zinazoelekea kwenye hifadhi hiyo, hivyo inafikika kipindi chote cha mwaka, wakati wa mvua na wakati wa kiangazi.

Anasema serikali pia imenza kujenga nyumba za kulala wageni na mpaka sasa nyumba zenye uwezo wa kulaza wagemi 24 kwa siku zimeishakamilika kujengwa na mara tu zitakapowekewa samani za ndani zitaanza kuhudumia watalii wa ndani na wa nje.

“Nyumba hizo zipo sehemu mbili, zipo zenye uwezo wa kulaza wageni 24. Hizi zipo eneo la Mikonje lililopo Kanda ya Burigi na pia kuna mahema ya kudumu ambayo yana uwezo wa kulaza wageni 12 ambayo pia yanasubiri kuwekewa samani za ndani ili yaanze kutumika.

“Hadi kufikia Julai mwaka huu, hema hizo zitaanza kulaza wageni. Matarajio yetu ni kuanza kulaza wageni 36 hifadhini kwa siku,” anasema Hingi.

Hingi anasema, kwa kasi aliyonayo Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Mussa Juma Kuji kukuza sekta ya utalii na ari walinayo watumishi hasa baada ya kubainika Hifadhi ya Burigi – Chato ina vivutio vya kipekee duniani ambavyo vikitangazwa kwa bidii, hifadhi hiyo inaweza kufikiwa na wageni wengi wakiwemo watafiti na watalii, nguvu zimeelekezwa kwenye uboreshaji wa huduma na miundombinu.

Mbega mwenye rangi ya kijivu na nyekundu wanaopatikana kwa wingi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato

Anasema wawekezaji wa ndani wanapaswa kutumia fursa iliyopo sasa kujenga hoteli pembezoni na ndani ya hifadhi, kujenga majengo ya huduma za chakula na kampuni za waongoza watalii kufungua ofisi.    

 “Hifadhi hii ni kubwa sana, inahitaji huduma zaidi za malazi, huduma zaidi za kampuni za waongoza watalii na huduma za chakula hivyo wawekezaji wa kitanzania na wa kigeni wanakaribishwa kuwekeza.

“Serikali imeweka mazingira mazuri sana kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwani eneo hili ndani ya muda mfupi mtu anaweza kukosa eneo la kuwekeza kwa sababu tunaamini likitangazwa vizuri na kwa namna dunia inavyolitazama sasa, litakuwa moja ya maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa watu na shughuli nyingi.

“Kuna maeneo ya kujenga hoteli pembezoni na ndani ya hifadhi na maeneo ya kuwekeza yametengwa vizuri. Uwezo wa hifadhi ni kupokea wageni zaidi ya 500 kwa siku lakini idadi ya sasa kulingana na uwekezaji wa serikali ni kupokea wageni 36 kwa siku,” anasema Hingi.

Lango la Kuhita la kuingia kwenye Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato

Hifadhi ya Burigi – Chato inafikika kirahisi kwa kutumia usafiri wa anga. Wageni wanaweza kufika hifadhini kwa kutumia kiwanja cha ndege cha kimataifa kilichopo Chato ambacho kiko umbali wa kilomita 50 kutoka lango la kuingilia hifadhini la Meja Kijuu.

Kwa njia ya barabara, hasa kwa wageni wanaotokea mikoa ya Kanda ya Ziwa na maeneo mengine ya jirani, wanaweza kufika hifadhini kwa kutumia barabara ya Mwanza, Biharamulo na kuingilia lango la Chato, Meja Kijuu lililopo eneo la Katete na au mgeni anaweza kusafiri kwa kutumia barabara ya Dodoma, Bukoba hadi Biharamulo na kupokewa makao makuu ya hifadhi kisha kuingia hifadhini kufanya utalii.

Wageni kutoka nchi jirani za Burundi na Rwanda wanaweza kufika hifadhini hapo kwa kupitia mpaka wa Rusumo ambao upo umbali wa kilomita 60 tu kutoka hifadhini na kwa wageni wanaotokea Uganda wanatumia lango la Kuhita. Vipo pia viwanja vya ndege vidogo vya Ngara, Biharamulo na Bukoba vinavyoweza kutumiwa na wageni kufika hifadhini.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya