Monday, December 23, 2024
spot_img

WAZIRI NDUMBARO ALIPASWA KUWA WA MWISHO KUZUA SOKOMOKO KWENYE MICHEZO 

RICHARD MBUNDA

“ATAKAYEVAA jezi ya Al Ahly au Mamelod Sundowns hataruhusiwa kuingia kwa Ben Mkapa isipokuwa ameonyesha passport. Na ukileta vurugu, polisi watashughulika na wewe……” hiyo ni kauli ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lina sheria na utamaduni wake. Ukipenda, waite muhimili wa michezo unaojitegemea. Hata kama hupendi lakini sifa yao kubwa ni moja, huwa wanalinda masilahi yao kwa choyo kubwa dhidi ya wavamizi, yaani serikali za nchi husika.

Ibara ya 17 ya Sheria za FIFA inafafanua kuwa kila mwanachama wa FIFA ataendesha shughuli zake kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu wa tatu. Hii ina maana FIFA wananuna mno pale ambapo mtu wa tatu ambaye ni serikali husika zinaingilia mambo ya vyama vya soka.

Kuna maeneo mawili ambayo yanaguswa katika hoja ya kuingilia mambo ya soka. Mosi, pale ambapo mahakama inaingilia mambo ya soka lakini pili kuingilia mambo ya utawala wa soka. 

Wachezaji wa timu za Simba ya Al ahly wakimenyama katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kusaka nafasi ya kucherza nusu fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika.

Suala aliloibua Waziri Ndumbaro linaweza kutafsiriwa kuwa linagusa usimamizi wa soka katika muktadha wa utawala. 

Naomba nisisitize kuwa hakuna ubaya kuhimiza uzalendo kwa nchi na bila shaka hii ni kazi ya wanasiasa, lakini katika muktadha wa soka, hili linapaswa kuwa ombi siyo shuruti. Huwezi kushurutisha uzalendo kwenye michezo. 

Uingereza kwa mfano, timu za Arsenal na Tottenham Hot Spurs ni watani wa jadi. Mwaka 2006 Arsenal ilicheza fainali ya UEFA dhidi ya Barcelona lakini mashabiki wa Spurs walishabikia Barcelona na kutamani Arsenal wasibebe kombe la UEFA.

Vivyo hivyo mashabiki wa Arsenal walifurahi Liverpool kuizuia Spurs kuchukua ubingwa kwenye fainali ya UEFA 2019.

Waziri Ndumbaro kama mwanasheria na Mwanamichezo anafahamu jambo hilo vyema kabisa. Ananishangaza tu jinsi alivyolishughulikia kwa matamshi yake ya wazi.

Kikosi cha timu ya Arsenal ya Uingereza

Waziri Ndumbaro ana historia ndefu kwenye michezo. Alishawahi kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ligi lakini pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba.

Hakika Waziri Ndumbaro ni mwanafamilia wa mchezo wa soka nchini Tanzania pia ana kumbukumbu ya kufungiwa na TFF mwaka 2014 kwa muda wa miaka saba kujihusisha na soka la nje na ndani ya nchi.

Huenda kifungo kilikuwa na figisu nyingi na sasa tunaweza kusema kifungo kimeisha. Pole sana kwake lakini bado Waziri Ndumbaro ana uelewa wa soka wenye upeo wa juu zaidi kuliko mawaziri wengi tukimwondoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mwenye taaluma hiyo.

Hoja yangu ni kuwa, katika matamshi yake, Waziri Ndumbaro aliiweka nchi kwenye tishio la kufungiwa na FIFA kwa kuwa yeye kama mwakilishi wa serikali ameingilia mambo ya utawala wa soka.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro

Na labda niongeze tu, tunapaswa kuhimiza uvumilivu kwenye michezo ambayo ni moja ya R4 za Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba waziri wake ameshindwa kutafsiri hilo kama sehemu ya ustahimilivu unaohimizwa katika falsafa hiyo.

Na nisisitize tu kuwa timu za Yanga na Simba zimeimarika na sasa kuwa timu tishio Afrika kwa utani wao wa kuchekana zinapofanya vibaya na hivyo kulazimisha kila timu iwekeze na ijitahidi katika mashindano ya ndani na yale ya CAF. Kwa hiyo timu hizi zinahitaji changamoto na siyo kubebwabebwa kwa namna yeyote. 

Niliwahi kuandika siku za nyuma kuwa serikali itusaidie kuwekeza kwenye ujenzi wa ‘youth sports academies’ ili kukuza vipaji vya soka na michezo mingine katika kila kanda. Nilitamani kusikia matamko ya aina hii kutoka kwa waziri, naibu wake na viongozi wengine katika sekta ya michezo.

Kwa kuhitimisha, niwaombe wadau wa michezo nchini tuitike wito wa serikali kuhusu uzalendo, ingawa suala la uzalendo siyo wajibu kwetu. Natumaini hawa viongozi watatupa maelezo tofauti wakati ujao.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya