Monday, December 23, 2024
spot_img

MABADILIKO KITITA CHA BIMA YA AFYA HAYAKUFUATA UTARATIBU – PST

RIPOTA PANORAMA

MABADILIKO ya kitita cha Bima ya Afya (NHIF), hayakufuata utaratibu.

Hayo yameelezwa na Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), kwenye maoni ya maboresho ya kitita hicho cha mwaka 2023.

PST kiliketi chini ya mwenyekiti wake, Fadhili Hezekiah na Katibu Mkuu, Benson Katundu mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya kuandikiwa barua na Wizara ya Afya, Machi 13, mwaka huu ikikiarika kutoa maoni na mapendekezo ya kitaalamu kuhusu utekelezaji wa kitita kipya cha Bima ya Afya cha mwaka 2023.

Pamoja na mambo mengine, PST kimeeleza kuwa uandaaji wa kitita kipya cha Bima ya Afya haukufuata utaratibu kwa sababu mabadiliko yaliyofanywa ni makubwa sana.

Kwamba uamuzi wa mabadiliko hayo haujibu changamoto zilizopo kwa sababu njia iliyotumika kufanya mabadiliko hayo siyo sahihi kwa tatizo lisilokuwa sahihi na kwamba watendaji walikuwa na mgongoni wa maslahi.

“Hii imesababisha kufanya maamuzi yasiyojibu changamoto kwa sababu imetumika njia isiyokuwa sahihi kwa tatizo lisilokuwa sahihi na zaidi ni kwa kuwa watendaji walikuwa na mgongano wa maslahi ama kwa kujua, kutaka au kwa kutokujua,” wanaeleza katika maoni na mapendekezo yao wafamasia hao.

Taarifa yao inaeleza pia kuwa kuna tafsiri potofu kuhusu malipo kwa ajili ya ushauri wa kitaalamu kuwa fedha ya daktari kulingana na tafsiri ya moja kwa moja iliyopo ambayo inatokana na historia ya kisekta na mfumo uliowaingiza kwanza madaktari kuanza kutoa huduma.

“Ukweli ni kwamba mgonjwa anaanza consultation (kupata ushauri) tangu anapoingia geti la kituo hadi anapotoka nje ya geti la kituo na kada nyingi za afya sasa wanafanya ubobezi,” wanaeleza.

PST kimetaja upungufu mwingine kilioubaini kwenye kuandaa mabadiliko hayo ni kuwekwa kando vyama vyote vya kitaalamu ambavyo wanachama wao ndiyo watendaji wakuu na wenye taarifa sahihi.

Kinataja makundi mengine yaliyopewa kisogo kwenye kuandaa mabadiliko ya kitita kipya cha Bima ya Afya kuwa ni wanazuoni hasa wenye uelewa wa afya na ufamasia, jumuiya ya wafanyabiashara hasa wazalishaji na waagizaji bidhaa na vyama vya wagonjwa hasa magonjwa yasiyoambukiza.

Kifaa tiba aina ya Paraffin Gauze Dressing

PST kimependekeza orodha ya dawa muhimu (NEMLIT) iboreshwe ili kuendana na maendeleo ya kimatibabu kwa mujibu wa maendeleo ya teknolojia duniani ikizingatiwa kuwa taifa linasomesha wabobezi wanaopaswa kupewa fursa ya kuutumia ubobezi wao kuwasaidia watanzania.

“Aidha, NEMLIT isifungamanishwe asilimia 100 na STG bali maandiko hayo mawili yasimamiwe na kamati au vyombo viwili tofauti ili kuondoa muingiliano wakati wa uandaaji na maboresho yake. SGT ndiyo itumike kuongoza masuala ya vitita vya Bima ya Afya  kwa sasa wakati NEMLIT inaboreshwa,” yanasomeka mapendekezo hayo.

Mapendekezo mengine ya PST ni gharama za ushauri ziwe gharama za ushauri wa kitaalamu, malipo ya huduma za kibingwa na malipo ya huduma bobezi na pia kukamilisha muundo wa Kurugenzi ya Dawa ya Wizara ya Afya.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya