RIPOTA PANORAMA
MAMLAKA ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inatapanya hovyo fedha za umma huku viongozi wake waandamizi wakiishi maisha ya anasa tupu.
Madai haya ya wizi na anasa yametolewa mapema mwezi huu na Katibu wa Baraza la Wafugaji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Alaitole, James Moringe katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Halmashauri ya Walaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha.
Moringe, akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafugaji na viongozi wa Serikali wa Ngorongoro alimnyooshea kidole moja kwa moja aliyekuwa Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Richard Kiiza (pichani juu) na maafisa wengine zaidi ya 50 wa mamlaka hiyo kwa kutapanya fedha za taasisi hiyo na kuishi maisha ya anasa kupitiliza.
Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameishamfukuza kazi Kiiza na Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza kuanzisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizotolewa na Moringe na wenzake.

Diwani wa Kata ya Alaitolei, iliyopo Tarafa ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha, James Moringe
Taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa umma iliyotolewa Aprili 2, 2024 ikiwa imesainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, John Mapepele ilieleza kuwa serikali inazo taarifa kuhusu tuhuma zilizotolewa dhidi ya NCAA na amekwishaanza kuzifanyia kazi.
“Wizara ya Maliasili na Utalii inazo taarifa za madai na tuhuma mbalimbali zinazowahusu watumishi kadhaa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ambazo zimekuwa zikisambazwa na mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
“Wizara inapenda kuuhakikishia umma kwamba tayari ilishaanza kuzifanyia kazi kwa kushirikisha vyombo mbalimbali vya serikali kabla ya mitandao ya kijamii kuanza kuzisambaza,” inasomeka taarifa hiyo.
Taarifa inaeleza zaidi kuwa, Serikai itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya watumishi watakaobainika kuhusika na kwamba hakuna mabadiliko yoyote ya uhamaji wa hiari kutoka Eneo la Hifadhi la NCAA.
Kwa mujibu wa Moringe ambaye alimpongeza Rais Samia kwa kumfukuza kazi Kiiza, akiwa Kamishna wa Uhifadhi wa Eneo la Ngorongoro alitapanya hovyo fedha za taasisi hiyo kufanya mambo ya anasa, alikichafua Chama Cha Mapinduzi (CCM) na alitumia mali za NCAA kwa mambo yake binafsi.

Alisema Kiiza aliyafanya hayo akishirikiana na wasaidizi wake inaosemekana alihama nao kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na kuwaweka Idara ya Ulinzi na Intelenjensia ya NCAA.
“Kwa kipindi cha muda mfupi cha aliyekuwa Kamishna, bwana Richard Kiiza, fedha za taasisi zimechotwa na wasaidizi wake ambao inasemekana alikuja nao kutoka TANAPA na kuwaweka Idara ya Ulinzi na Intelenjensia ambapo ndiyo imekuwa uchochoro wa kupitishia fedha kwa kisingizio kuwa zinaenda kufanya kazi maalumu na kuimarisha Chama Cha Mapinduzi kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais.
“Hili ni jambo ambalo limetunyanyua sisi kama viongozi na ni viongozi wa chama tawala, tuliposikia jambo hili halikutupendeza na tunampongeza Rais kwa kuchukua hatua hiyo,” alisema Moringe.
Akiendelea, alidai Kiiza na genge lake walikuwa wakiwatisha wenyeji wa Ngorongoro kuwa serikali inakusudia kuwaondoa kwa nguvu katika maeneo yao kuwapeleka Kijiji cha Msomera, kilichopo Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga na kwamba kile ilichokuwa ikikisema ni uhamaji wa hiari ni kiini macho tu.
Alidai, mbali na kuwatisha wakazi wa Ngorongoro, Kiiza na genge lake pia walikuwa wakiwatisha watumishi wa umma kuwa wasipojiandikisha kuhama kwa hiari wataondolewa kwa nguvu na watafukuzwa kazi.
Akizungumza kuhusu anasa zilizokuwa zikifanywa na Kiiza kabla hajafukuzwa kazi, alisema tangu alipoteuliwa kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hadi alipofukuzwa kazi na Rais Samia alikuwa analala kwenye Hoteli ya Kitalii yenye gharama kubwa aliyoitaja kwa jina la Member of Grand Melia, zamani ikijulikana kwa jina la Wild Life.
Moringe alidai kuwa Kiiza alikuwa akitumia fedha za NCAA, Dola za Marekani 1250 ambazo ni zaidi ya Shilingi milioni 3 kwa siku, kulipia malazi katika hoteli hiyo tangu alipoteuliwa kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA.
Alidai fedha zilizotumiwa na Kiiza kugharamia malazi yake akiwa Kamishna wa Uhifadhi ni zaidi ya Sh. 400 milioni ambazo zingeweza kusomesha wanafunzi 154 wa jamii masikini ya wamasai.
Aidha, Moringe alidai zaidi kuwa Kiiza akiwa Kamishna wa Uhifadhi, katika kipindi cha takribani miezi mitatu alitumia Sh. 154 milioni za NCAA kugharamia mafuta ya ndege aliyokuwa akisafiri nayo kwa shughuli zake binafsi huku akidanganya kufanya safari za kikazi.