DET’U KAKELAKAMBUZI
MAJIBU ya maswali magumu na ufafanuzi wa hoja nzito ambazo zimekuwa zikiibua mijadala mikali katika mitandao ya kijamii kuhusu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) yaliyotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Plasduce Mbossa yameibua mjadala mpya wa umuhimu wa viongozi wa umma kutoa taarifa za mambo wanayoyatekeleza.
Ikiwa ni takribani siku tano sasa tangu Mbossa alipofanya mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog na kueleza jinsi fedha za mikopo zilizotolewa na Benki ya Dunia (WB) pamoja na Serikali ya Uingereza kwa Tanzania kisha kuelekezwa TPA zilivyotumika kutekeleza miradi mbalimbali katika Bandari ya Dar es Salaam, mjadala kuhusu viongozi wa umma kujibu hoja na kufafanua mambo ambayo wananchi wanahitaji majibu, umeshika kasi.
Mbossa alizungumza na Tanzania PANORAMA Blog akijibu na kufafanua uwepo, mwenendo na majukumu ya Kampuni ya DP World ya Dubai katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kueleza kuwa serikali inamiliki eneo lote la Bandari ya Dar es Salaam likiwemo ililoipangisha Kampuni ya DP World na jinsi mkopo wa Sh. 864 bilioni kutoka WB na Dola za Marekani 12 milioni za Serikali ya Uingereza zilivyotumiwa na TPA kuboresha Bandari ya Dar es Salaam.
Katika mahojiano hayo, Mbossa alikiri kutolewa kwa mikopo hiyo huku akieleza jinsi ilivyotumika kuboresha gati za kuhudumia shehena mchanganyiko na makasha, maeneo ya kuhifadhia makasha na ujenzi wa gati jipya la kuhudumia meli na kuhifadhia magari.
Matumizi mengine ya fedha hizo aliyoyataja ni kugharamia upanuzi na uongezaji wa kina cha lango la njia ya kupitisha na kugeuza meli, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya maboresho ya gati pamoja na usimikaji wa miundombinu ya umeme katika magati.
Kauli hiyo ya Mbossa inaelekea kuhitimisha mjadala mkali na wa muda mrefu uliobuliwa na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa mwaka 2017, WB ilitoa mkopo wa Sh, 864 bilioni kwa Serikali ya Tanzania wenye masharti ya kulipwa ndani ya miaka saba na mkopo mwingine ulitolewa na Serikali ya Uingereza kupitia Idara ya Maendeleo ya Kimataifa (Department for International Develompent – DFID).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Plasduce ,Mbossa.
Kwamba mikopo hiyo ilikusudiwa kujenga lango la Bahari la Dar es Salaam (DSMGP) kwa kuongeza kina na kuimarisha gari namba moja hadi 11, kununua mifumo, usimamizi wa taarifa na mifumo ya uendeshaji wa vituo katika gati lakini miaka mitano baadaye Kampuni ya DW World ya Dubai imepewa eneo la Bandari ya Dar es Salaam ambalo limejengwa kwa mkopo huo huku ikisamehewa kulipa kodi.
Kwenye mjadala wa sasa kuhusu umuhimu kwa viongozi wa umma kujibu maswali na hoja zinazoibuliwa ili kuwapa wananchi uelewa wa mambo yanayofanywa na serikali na taasisi zake, TPA ni kama imeweka chumvi kwenye kidonda dhidi ya mambo ambayo hayajafafanuliwa au kujibiwa ipasavyo na serikali licha ya wananchi wengi kuwa na kiu na majibu.
“Serikali iwe inafanya hivi sasa. Hapa tumeelewana kama kuna mwenye hoja kinzani ailete lakini majibu tumepata. Hili jambo limetuchukulia muda mrefu kumbe kweli mikopo ipo na matumizi yake yapo wazi. Hawa TPA wawe wanafanya hivi, wananchi tunataka taarifa sahihi, tukizikosa ndiyo tunabeba tunachosikia ila hapo kwenye DP World watuambie vizuri imekaaje kaaje,” ameandika Geofrey Mshana akiwa miongoni mwa wengi waliochangia kwenye ukurasa wa Tanzania PANORAMA Blog.
Msomaji mwingine, Abihud Mussa yeye ameandika akitaka taasisi zinazohusika na mapambano dhidi ya rushwa zitoe taarifa ya utekeleza wa ripoti ya CAG.
“Sasa walikuwa wapi siku zote kusema au huwa wanasemea wapi? Kumbe majibu wanayo wamekaa nayo kimya wakati umma hatujui. Kukopa siyo dhambi kama mkopo unatumika kwa manufaa ila kinacholeta shida ni usiri wao ndiyo maana wanaambiwa wanachukua ten percent. Hao tumemaliza nao, sasa tuletee taarifa ya …… maana CAG alisema kuna wizi mkubwa sana,” ameandika Mussa.
Mwingine aliyejitambulisha kwa jina Abou Othman wa Demark ameandika akieleza umuhimu wa matumizi ya mitandao ya kijamii kwa serikali kufikisha taarifa kwa umma kwa wakati.

Mwonekano wa gati namba moja katika Bandari ya Dar es Salaam wakati likifanyiwa maboresho.
“…. Huko nyumbani kuna mambo mengi ambayo sisi tulio mbali tunataka kuyajua. Viongozi watumie social media kutoa taarifa kwani ni chapchap tu kila mtu anajua kinachoendelea badala ya kujifungia na habari kwenye ofisi zao. Hili suala tumejadili nadhani mwezi mzima na tulijua tumepigwa, leo majibu ndiyo anayatoa. Lakini imesaidia kwa sababu sasa tuna share link kwenye groups zetu watu wanasoma wanajua nini kinaendelea nyumbani,” amesema Othman.
Neema Shayo aliyejitambulisha kuishi Finland yeye ameandika, “PANORAMA asante sana kwa kushare hii limk yenye habari hii, huyo Bwana Mbossa mpe maua yake. Hizi mambo ndiyo tunataka wawe wanasema pesa zetu wanazifanyia nini siyo kuzitumbua tu. Tunataka viongozi wanaojiamini wa aina hii, wanaosimama kujibu hoja siyo wanaoulizwa wanaanza mikwara. Tunaomba na Bima ya Afya …… tuletee habari zao.”
Aysha Ramadhani aliyejitambulisha kuwa yupo Tabata, Dar es Salaam yeye ameandika; “Tukiwa na viongozi kama watano wa aina hii taifa litapona. Kopa, ukiulizwa toka, simama, sema nimekopa kwa ajili hii na nimefanya hivi. Nimempenda bure huyo jamaa, lakini bado mwambie atuambie na masharti ya mkopo hajayasema, hilo hujaliandika mbona?”
Pamoja na maoni haya ya wasomaji na wafuatiliaji wa mambo, katika siku za karibuni upatikanaji wa taarifa kutoka kwa viongozi wa umma umekuwa wa kuridhisha kwa kiwango kikubwa ingawa bado kuna changamoto kwa baadhi ya viongozi kutoa ushirikiano kwa waandishi, wanapofikiwa kuulizwa baadhi ya mambo.