DET’U KAKELAKAMBUZI
WATUMISHI wa Bandari ya Dar es Salaam wamepewa fursa ya kuchagua kuajiriwa na Kampuni ya DP World ya Dubai au kuendelea na ajira zao TPA katika mabadiliko ya usimamizi na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam yanayoendelea kutekelezwa sasa.
Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano ya TPA, ilieleza kuwa mabadiliko ya usimamizi na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam yalianza rasmi kutekelezwa Oktoba 22, 2023.
Ilieleza kuwa kutokana na mabadiliko hayo katika Bandari ya Dar es Salaam, menejimenti imewapa fursa watumishi ya ama kuchagua kubaki kwenye ajira walizonazo TPA au kusitisha mikataba yao ya ajira kwenye mamlaka hiyo na kuajiriwa na Kampuni ya DP World papo hapo.
Taarifa ilieleza zaidi kuwa watumishi watakaoridhia kujiunga na DP World kwa hiari wawasilishe taarifa zao ghorofa ya 32, katika jengo la Makao Makuu ya TPA kabla au ifikapo Machi 29, 2024.
“Aidha, watumishi ambao hawatapenda kujiunga na DP World watabaki TPA kwa kuwa mamlaka itaendelea kuhitaji watumishi watakaotoa huduma katika bandari zinazoendelea kuboreshwa katika maeneo mbalimbali nchini,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kuhusu mchakato wa mabadiliko hayo, taarifa ilieleza kuwa Machi 20, 2024 TPA ilitoa taarifa kwa watumishi wake kuhusu mabadiliko ya usimamizi na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kuanzia gati namba sifuri hadi namba saba.

Hafla ya utiaji saini mkataba wa usimamizi na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam iliyofanyika Dar es Salaam mwaka jana.
Kwamba kuwepo kwa mabadiliko hayo kunatokana na mkataba ulioingiwa kati ya TPA na DP World wa uendeshaji na uendelezaji wa gati namba sifuri hadi saba za Bandari ya Dar es Salaam kwa muda wa miaka 30, ulioanzia Oktoba 22, 2023.
“Kutokana na mabadiliko haya ya usimamizi na uendeshaji wa maeneo tajwa, watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam walitakiwa kuchagua ama kubaki TPA au kusitisha mkataba wa ajira na TPA na kuajiriwa na DP World papo hapo,” inasomeka sehemu nyingine ya taarifa.
Aidha, inaeleza zaidi kuwa TPA itaendelea kuwathamini watumishi wake ambao ni rasilimali muhimu zaidi kwenye mamlaka hiyo na wakati wa utekelezaji wa mabadiliko yanayoendelea sasa, maslahi ya pande zote husika yatazingatiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria za nchi.