RIPOTA PANORAMA
WIZARA ya Kilimo inasubiri Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuthibitisha hoja za Mkaguzi wa Ndani wa Kampuni ya Mbolea (TFC), zinazoonyesha kuwepo kwa viashiria vya rushwa na ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya umma kwenye manunuzi ya tani 4500 za mbolea.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli (pichani juu) alisema hoja zilizoibuliwa na Mkaguzi wa Ndani wa TFC kwenye ukaguzi wa manunuzi, usambazaji na uuzaji wa tani 4500 za mbolea yenye thamani ya Sh. 7.9 bilioni, zitathibitishwa na CAG.
Alisema baada ya Mkaguzi wa Ndani wa TFC kufanya ukaguzi wake na kuibua hoja alizoziona, wapo wakaguzi wengine wa nje ya TFC watakaofanya ukaguzi na mwisho CAG atafanya ukaguzi wake na ripoti yake itafanyiwa kazi kwa uwazi.
Akifafanua hilo, Mweli alisema ukaguzi wa ndani unalemga kumsaidia Mkurugenzi Mkuu wa TFC kufanyia kazi hoja zilizoibuliwa na kwamba huo ndiyo msingi wa ripoti ya mkaguzi wa ndani kuelekezwa kwake.
“Nimeyaona maswali yako lakini ujue hii ni ripoti ya ndani ambayo sasa siwezi kuizungumzia. Hoja zilizoibuliwa na mkaguzi wa ndani zinapaswa kujibiwa, mkaguzi wa ndani anafanya ukaguzi wake kumsaidia mtendaji mkuu wa kampuni kuona lilipo tatizo.
“Lakini wapo wakaguzi wengine wa nje ambao watafanya ukaguzi na mwisho CAG naye atafanya ukaguzi na ripoti yake itakuwa wazi na tutaifanyia kazi. Kwa sasa haya mambo bado ni ya ndani siwezi kuyasemea kwa sababu hoja zilizoibuliwa lazima zijibiwe na au zifanyiwe kazi,” alisema Mweli.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere
Alipoulizwa kuhusu menejimenti ya TFC kuendeshwa kienyeji jambo lililodhihirishwa na ripoti ya mkaguzi wa ndani inayoeleza kuwa hakuna zabuni iliyotangazwa ya manunuzi, usambazaji na uuzaji wa tani 4500 za mbolea, menejimenti kutokuwa na nyaraka yoyote iliyoandaliwa nayo kwa ajili ya manunuzi hayo na kutokuwepo kwa kikao chochote kilichoketi kuamua kufanyika kwa manunuzi, Mweli alisema hoja hizo zinapaswa kujibiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TFC ambaye amekabidhiwa ripoti.
Kwa muda mrefu, Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Samuel Ahad Mshote kuzungumzia skandali hiyo lakini hatoi ushirikiano.
Ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa TFC inayoishia Juni 30, 2023 ya manunuzi, usambazaji na uuzaji wa tani 4500 za mbolea yaliyofanyika Januari hadi Juni, 2023 inabainisha kukiukwa kwa sheria ya manunuzi ya umma, kukinzana kwa ripoti za fedha za kampuni na kutokuwepo kwa nyaraka yoyote ya manunuzi ya mbolea hiyo.
Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona, inabainisha kuwa idara yenye dhamana ya kuweka salio la hisa za mbolea nayo haina kumbukumbu sahihi za salio la hisa za mbolea kutoka kwenye maeneo ya mauzo.
Mkaguzi wa ndani katika ripoti yake anaeleza kuwa wakati wa uhakiki wa hati za mauzo ya tani 4500 za mbolea iliyogharimu Sh. 7.9 bilioni, alibaini kuwa hadi Juni 30, 2023 kumbukumbu sahihi za salio la hisa za mbolea halikuwepo kwani idara inayohusika na utunzaji kumbukumbu hizo alifikiwa kuombwa lakini haikutoa na hata ilipokumbushwa mara kwa mara kuzitoa, haikuwa nazo.
Ripoti inafichua uwepo wa takwimu tofauti za mauzo ya mbolea kati ya kumbukumbu zilizowekwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na rekodi zilizowekwa na TFC na kwamba rasimu ya taarifa za fedha iliyowasilishwa kwa CAG, Agosti, mwaka jana ya mauzo ya mifuko 77,827 ya mbolea ina walakini.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea (TFC) Samuel Ahad Mshote
Inakwenda mbali zaidi ikionyesha uwepo wa nyaraka zilizokosewa au zisizokuwa sahihi za Sh. 158.7 milioni kwenye manunuzi, usambazaji na uuzaji wa mbolea hiyo.
Kwamba nyaraka hizo zilifanywa kwa mfumo wa kihasibu hivyo kuathiri takwimu za mauzo na kwamba marekebisho yaliyofanywa kwenye nyaraka hizo hayakuwa na uhusiano wa wingi wa mifuko ya mbolea iliyouzwa.
Haya yanajiri wakati Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akitenga bajeti kubwa kwenye Wizara ya Kilimo mwaka hadi mwaka ili kuinua Sekta ya Kilimo, akilia na mtandao wa mchwa wanaotafuna bila huruma fedha za umma.
Kauli ya hivi karibuni ya Rais Samia kuhusu wizi wa fedha za umma aliielekeza kwa wakuu wa mikoa na wilaya aliposema kuna mtandao wa serikali unaokwenda sambamba na wa wizi na kuwataka kuudhibiti.

Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mtandao upo na unaenda, wanaambizana na unachepusha fedha nyingi sana….,” alisema Rais Samia.
Mbali na hayo, inadaiwa mwenendo wa mambo ndani ya Wizara ya Kilimo si shwari kutokana na baadhi ya maafisa kutobaliani na uteuzi wa kundi la watu waliosoma chuo kikuu kimoja na kuhitimu pamoja kuwekwa kwenye nafasi nyeti za wizara hiyo.
SOMA TANZANIA PANORAMA BLOG UPATE HABARI ZA UHAKIKA ZILIZOFANYIWA UTAFITI WA KINA.