Friday, July 18, 2025
spot_img

TPA YASEMA DP WORLD NI MPANGAJI BANDARINI, SERIKALI NI MMILIKI NA MWENDELEZAJI

RIPOTA PANORAMA

SERIKALI inamiliki eneo lote la Bandari ya Dar es Salaam likiwemo ililoipangisha Kampuni DP World ya Dubai.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Plasduce Mbossa alipothibitisha kuwa Serikali imekopa Sh. 864 bilioni kutoka Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni kuhusu matumizi ya fedha za mikopo iliyotolewa na Benki ya Dunia pamoja na Serikali ya Uingereza kwa Serikali ya Tanzania kisha kuelekezwa TPA, Mbossa alisema Serikali ina wajibu wa kuendeleza bandari zote nchini kwa sababu inazimiliki.

Katika mahojiano hayo, Mbossa alifafanua kwa mara nyingine uwepo, mwenendo na majukumu ya Kampuni ya DP World katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kusudi la kuweka rekodi sahihi dhidi ya taarifa zinazotolewa kwenye majukwaa mbalimbali na kuibua mijadala yenye mwelekeo hasi kuhusu uwepo wa kampuni hiyo bandarini hapo.

Mbossa alisema Kampuni ya DP World imepangishwa kwenye maeneo ambayo Serikali imekwishayafanyia maboresho kwa fedha za mkopo, Sh. 864 bilioni zilizotolewa na Benki ya Dunia.

Alisema Serikali ina jukumu la kuboresha miundombinu ya bandari zote nchini kwa sababu inazimiliki na kwamba utekelezaji wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ulifadhiliwa na Benki ya Dunia na Serikali yenyewe.

Magari yakiwa yamehifadhiwa Bandari ya Dar es Salaam baada ya kushushwa kwenye meli.

“Kampuni ya DP World imepangishwa kwenye maeneo ambayo Serikali imeishafanya maboresho ya miundombinu ya msingi tu. Ni jukumu lake kufanya hivyo kama mmiliki na mwendelezaji wa bandari nchini na imefanya hivyo kupitia mradi uliotekelezwa kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia pamoja na Serikali yenyewe,” alisema Mbossa.

Akizungumza kuhusu matumizi ya fedha za mkopo huo, Mbossa alisema zilitumika kuboresha gati za kuhudumia shehena mchanganyiko na makasha, maeneo ya kuhifadhia makasha, ujenzi wa gati jipya la kuhudumia meli za magari na ujenzi wa eneo la kuhifadhia magari.

Alisema fedha hizo pia zilitumika kugharamia upanuzi na uongezaji wa kina cha lango na njia ya kupitisha na kugeuzia meli, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya maboresho ya gati pamoja na usimikaji wa miundombinu ya umeme katika magati.

Mbossa alikanusha madai kuwa mkopo huo ulitolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kufanya ununuzi wa mifumo, usimamizi wa taarifa na mifumo ya uendeshaji wa vituo katika gati. Alisema fedha hizo hazikutolewa kwa lengo hilo.

“Hakuna mifumo inayotekelezwa kupitia fedha za mkopo na kwa kuwa Serikali imeishirikisha Sekta Binafsi katika uendeshaji wa maeneo hayo, jukumu la uwekezaji wa mifumo ya uendeshaji kwenye maeneo walikopangishwa Sekta Binafsi ni la mwekezaji aliyepangishwa,” alisema Mbossa.

Alisema, Serikali kupitia TPA imeimarisha na kuongeza kina cha gati namba moja mpaka saba ambayo sasa kina chake kinafikia mita 14.5 kutoka wastani wa kina cha mita 10 cha awali na kwamba gati namba nane mpaka 10 hajafanyiwa maboresho ya aina yoyote.

Gati namba moja la Bandari ya Dar es Salaam wakati likifanyiwa maboresho.

Kwa nyakati tofauti, hoja kuhusu mikopo iliyotolewa na taasisi za fedha za kimataifa na zile zilizotolewa na nchi wahisani pamoja na mambo mengine, zimekuwa zikiibuliwa mitandaoni na kuzuia mijadala mikali.

Baadhi ya wachangiaji wakiwemo wenye ushawishi kwa kufuatiliwa na watu wengi mitandaoni wamekuwa wakichangia kwenye kurasa za Tanzania PANORAMA Blog kwa maandishi yenye ukakasi kuyaandika kuhusu habari za TPA inazoziripoti kutoka kwa watu wenye mamlaka na maelezo sahihi.

Katika mjadala wa hivi karibuni, ilidaiwa kuwa mwaka 2017, Benki ya Dunia iliikopesha Tanzania Sh. 864 bilioni; mkopo huo unatakiwa kulipwa ndani ya miaka saba na ulikusudiwa kujenga lango la Bahari la Dar es Salaam (DSMGP) kwa kuongeza kina na kuimarisha gati namba moja hadi 11.

Aidha, ilidaiwa kuwa Serikali ya Uingereza kupitia Idara ya Maendeleo ya Kimataifa (Department for International Development – DFID) imetoa mkopo wa Dola za Marekani 12 milioni kwa Serikali ya Tanzania ambayo uliuelekeza TPA lakini miaka mitano baadaye, Kampuni ya DP World imepewa eneo la bandari ambalo limejengwa kwa mkopo huo huku ikisamehewa kulipa kodi.

Pamoja na mambo mengine, ilidaiwa pia kuwa mkopo kutoka Benki ya Dunia ulilenga ununuzi wa mifumo ya usimamizi wa taarifa na mifumo ya uendeshaji wa vituo katika gati; madai ambayo yamejibiwa na Mkurugenzi Mkuu Mbossa kwa ufafanuzi wa kina.

Hata hivyo, Mbossa aliiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa mwenye mamlaka ya kuzungumzia masharti ya mkopo uliotolewa na Benki ya Dunia ikiwemo riba na umri wa kulipa ni Wizara ya Fedha.

Na hata alipoulizwa kuhusu masharti ikiwemo umri wa mkopo na riba ya mkopo wa Dola za Marekani 12 milioni uliotolewa na Serikali ya Uingereeza kupitia Idara yake ya Maendeleo ya Kimataifa, Mbossa alisema hilo nalo iulizwe Wizara ya Fedha.

TANZANIA PANORAMA BLOG INAPENDA KUWAHAKIKISHIA WASOMAJI WAKE KUWA ITAENDELEA KURIPOTI HABARI ZA UHAKIKA KUTOKA MAMLAKA HUSIKA NA ITARIPOTI BILA WOGA WALA UPENDELEO WOWOTE.  

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya