RIPOTA PANORAMA
TUHUMA zilizoibuliwa na Mwalimu Angelight Kimaro, mwenye ualbino anayefundisha Somo la Kiswahili Shule ya Sekondari Bunju A za kufanyiwa vitendo vya unyanyapaa na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bupe Mkondola zinachunguzwa.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kinondoni, Mtundi Nyamhanga, alipokuwa akieleza hatua zilizochukuliwa na ofisi yake kushughulikia tuhuma hizo.
Nyamhanga alisema tuhuma hizo zinashughulikiwa bila ubabaishaji na uchunguzi unaangalia mambo matano.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni vitendo vya kumnyanyapaa mwalimu ambavyo ni lazima uchunguzi wake ufanyike kwa umakini na pili utendaji kazi wa mwalimu anayelalamika upoje kwa wanafunzi anaowafundisha.
Jambio la tatu alilolitaja kwenye uchunguzi huo ni iwapo Mkuu wa Shule, Mwalimu Mkondola anamsimamia Mwalimu Kimaro kwa kufuata taratibu na kanuni za utumishi na nne uchunguzi utaangalia iwapo kuna mizozo binafsi, aidha inayosababishwa na Mkuu wa Shule, Mwalimu Mkondola au Mwalimu Kimaro.
Alisema uchunguzi huo pia utawahusisha walimu wengine na wanafunzi wa shule hiyo ambao watafikiwa ili kueleza wanachokijua kuhusu mgogoro uliopo baina ya Mwalimu Kimaro na Mwalimu Mkuu Mkondola.

Mwalimu Angelight Kimaro
Afisa elimu huyo alisema yeye binafsi amekwishakutana na kuzungumza na Mwalimu Kimaro na Mwalimu Mkuu Mkondola na baada ya hatua hiyo, timu ya uchunguzi kutoka kwenye ofisi yake itakwenda shuleni hapo kufanya uchunguzi wa kina.
Alisema uchunguzi wa timu yake utakamilika kati ya Machi 13 na 14 lakini aliweka sharti kwamba iwapo Tanzania PANORAMA Blog itataka kuzungumza naye kuhusu matokeo ya uchunguzi huo ni lazima ipate kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Hanifa Suleiman.
Mwalimu Kimaro aliibua tuhuma za kufanyiwa vitendo vya unyanyapaa na Mwalimu Mkuu Mkondola hivi karibuni alipofanya mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog na kueleza kuwa yupo kwenye wakati mgumu lakini atapambana bila kuchoka dhidi ya unyanyapaa anaofanyiwa.
Alisema Mwalimu Mkuu Mkondola anamuhukumu kuwa hana uwezo wa kufundisha kidato cha nne kwa sababu ya ulemavu wa ngozi alionao wakati uwezo huo anao.
Alisema Mwalimu Mkuu Mkondola anaamini ulemavu alionao unamfanya asiwe na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi unaotakiwa hivyo amekuwa akitumia madaraka yake kuingilia utendaji kazi wake na kumnyanyapaa.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunju A, Bupe Mkondola
Mwalimu Kimaro alisema Mwalimu Mkuu Mkondola amemzuia kufundisha kidato cha nne kwa kile anachoeleza kuwa ana uoni hafifu na alitangaza kwa walimu wenzake kuwa hafai kufundisha darasa hilo; maneno ambayo yalimuumiza na kumfanya asiaminiwe na walimu wenzake.
Alieleza pia kuwa licha ya kuwa na udhuru wa kupangiwa zamu ili asikae juani kwa muda mrefu, Mwalimu Mkuu Mkondola amempangia zamu kwa lazima na kwamba alifanya hivyo ili apate sababu ya kumuondoa kufundisha kidato cha nne.
Mwalimu Mkuu Mkondola alipoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu madai hayo, alisema Mwalimu Kimaro siyo mtii wa maelekezo yake na amekuwa akijibizana naye hivyo madai yake yanashughulikiwa na uongozi wa wilaya.