Saturday, July 19, 2025
spot_img

HARUFU YA UFISADI KAMPUNI YA MBOLEA TANZANIA

RIPOTA PANORAMA

WAKATI ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) ikibainisha kuwepo kwa viashiria vya rushwa na kusiginwa kwa sheria ya manunuzi ya umma kwenye manunuzi ya tani 4500 za mbolea, nyaraka za fedha za kampuni hiyo nazo zimebainika kuwa ni batili.

Sambamba na hilo, ripoti hiyo ya mkaguzi wa ndani imebainisha zaidi kuwa idara yenye dhamana ya kuweka salio la hisa za mbolea, nayo haina kumbukumbu sahihi za salio la hisa za mbolea kutoka kwenye maeneo ya mauzo.

Haya yameelezwa kwenye ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa TFC ya ukaguzi wa manunuzi, usambazaji na uuzaji wa tani 4500 za mbolea yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 7.9 yaliyofanyika kati ya Januari na Juni 2023.

Ripoti imebainisha kuwa mwenendo wa manunuzi hayo una viashiria vya rushwa, ulikiuka sheria ya manunuzi ya umma na kwamba ulifanyika bila ruhusa ya menejimenti ambayo haina nyaraka yoyote kuhusu manunuzi hayo.

Pamoja na hayo, ripoti pia inafichua uwepo wa takwimu tofauti za mauzo ya mbolea hiyo kati ya kumbukumbu zilizowekwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na rekodi zilizowekwa na TFC na kwamba rasimu ya taarifa ya fedha iliyowasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali (CAG), Agosti mwaka jana ya mauzo ya mifuko 77,827 ya mbolea ina walakini.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere.

Kwa mujibu wa ripoti, kuna nyaraka zilizokosewa na au zisizokuwa sahihi za Sh. milioni 158.7 kwenye manunuzi, usambazaji na uuzaji wa tani 4500 za mbolea.

Ripoti inaeleza kuwa nyaraka hizo zilifanywa kwa mfumo wa kihasibu hivyo kuathiri takwimu za mauzo na kwamba marekebisho yaliyofanywa kwenye nyaraka hizo hayakuwa na uhusiano wa wingi wa mifuko ya mbolea iliyouzwa.

Mkaguzi katika ripoti yake anaeleza kuwa wakati wa uhakiki wa hati za mauzo ya tani 4500 za mbolea yenye thamani ya Sh. 7,933,184,869.52, ilibainika kuwa hadi Juni 30, 2023 idara yenye dhamana ya kuweka salio la hisa za mbolea ilishindwa kuonyesha au kuwasilisha kwa mkaguzi kumbukumbnu sahihi za salio la hisa za mbolea kutoka kwenye maeneo ya mauzo licha ya kuombwa na kukumbushwa mara kwa mara.

Anaendelea kueleza mkaguzi kuwa tani 4500 za mbolea iliyonunuliwa na TFC, ilipelekwa katika vituo mbalimbali kwa kutumia usafiri wa kukodi, kisha mifuko 4,346 ya mbolea ikasafishwa upya kutoka kwenye vituo ilivyokuwa na kupelekwa kwenye maeneo mbadala.

Mkaguzi anaeleza kuwa uamuzi huo uliisababishia TFC hasara ya Sh. 46,750,000.02 ambazo ni ongezeko la gharama ya usafirishaji.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Samuel Ahad Mshote

Dosari nyingine iliyobainishwa kwenye ripoti hiyo ni hatua ya kununua mifuko tupu 100,000 kutoka Kampuni ya Azania Poly Bagy Industy Ltd kwa ajili ya kufungia mbolea ya Urea na SA lakini haikutumika yote jambo linaloweza kusababisha usimamizi mbovu wa mifuko hiyo.

Aidha ripoti inaeleza kuwa wakati wa manunuzi ya tani 4500 za mbolea, tani 1000 zilinunuliwa kutoka kwa wauzaji wawili tofauti ambao ni Kampuni ya ETG Inputs Ltd ambako zilinunuliwa tani 500 kwa Sh. 60,000 kwa mfuko wa kilo 50 na Kampuni ya Premium Agro nayo iliiuzia TFC tani 500 kwa bei Sh. 62,000 kwa mfuko mmoja.

Mkurugenzi Mkuu wa TFC Samuel Ahad Mshote ambaye ametafutwa mara kadhaa kuzungumzia skandali hii, amekaa kimya kama ilivyo kwa Waziri Kilimo, Hussein Bashe ambaye simu yake imekuwa ikiita bila kupokelewa na hata alipotumiwa maswali kwa maandishi, aliyasoma kisha akakaa kimya kabisa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Tanzania PANORAMA Blog inamtafuta Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhimiza kilimo na matumizi ya mbolea huku akipambana na viongozi wanaokiuka sheria na wanaotumia vibaya fedha za umma ili kupata kauli yake kuhusu skandali hii.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya