RIPOTA PANORAMA
MAMBO ni magumu ndani ya Menejimenti ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), baada ya mkaguzi wa ndani wa shirika hilo kubainisha kukinzana kwa taarifa za fedha kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2023.
Vyanzo vya habari vya ndani ya kampuni hiyo pamoja na Ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa TFC ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona, vinaonyesha tofauti ya takwimu za mauzo kati ya kumbukumbu zilizowekwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na rekodi zinazowekwa na Kampuni ya Mbolea Tanzania.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa TFC ya ukaguzi wa manunuzi, usambazaji na uuzaji wa tani 4500 za mbolea yenye thamani ya Sh. 7,915,794,880, kumbukumbu za TFRA na rekodi za TFC katika kuzalisha taarifa za fedha ni tofauti.
Ripoti inaonyesha kuwa rasimu ya taarifa za fedha iliyowasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Agosti, mwaka jana, ya mauzo ya mifuko 77, 827 ya mbolea ina walakini.
Ripoti inafafanua kuwa takwimu za TFC za mauzo ya mifuko 77,827 ya mbolea ambayo ni sawa na tani 3,891.35 ni Sh. 7,907,392,062.66 lakini mfumo wa utunzaji kumbukumbu wa TFRA, kwa tarehe hiyo hiyo unaonyesha takwimu za mauzo ya mifuko 83,976 ambazo ni tani 4,198.80 zikiwa na thamani ya Sh. 8,449,775,171.
Kwamba; kwa mtazamo huo, mapato ya mauzo ya kampuni yanapelea Sh, 542,363,108.34 ikilinganishwa na kumbukumbu za TFRA.
Ripoti inaonyesha zaidi kuwa kwa kiwango kikubwa, TFC ilipata hasara kwenye mauzo ya mbolea hiyo.
Kwamba; kwa mujibu wa taarifa za fedha zilizowasilishwa kwa CAG kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2023, vituo vitano kati ya 11 vya mauzo ya mbolea ndiyo vilipata faida.
Inavitaja vituo hivyo kuwa ni Dar es Salaam, Sumbawanga, Makambako, Songea na Kyela vilivyoingiza faida ya Sh. 937,191,337.40 huku vituo sita ambavyo ni Tarime, Ifakara, Arusha/Moshi, Rungwe Nanchingwea na Mbeya vikizalisha hasara ya Sh, 218,792,524.17.
Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Samuel Ahad Mshote ameulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu ripoti ya mkaguzi wa ndani wa taasisi inayoiongoza kubaini ‘madudu’ kwenye manunuzi ya mbolea hiyo lakini hakujibu chochote.
Taarifa zaidi kutoka vyanzo vya habari vilivyo ndani ya TFC zinadai kuwa, watu watatu waliosoma chuo pamoja kisha wakatawanyika sehemu tofauti za ajira kabla ya hivi karibuni kuwekwa kwenye nafasi nyeti TFRA na TFC na kigogo mmoja, (majina tumeyahifadhi kwa muda) ambaye naye walisoma chuo pamoja, wanapambana kuhakikisha ripoti hiyo ya mkaguzi wa ndani ‘inayeyuka.’
Hivi karibuni, Tanzania PANORAMA Blog iliripoti ukiukwaji mkubwa wa sheria ya manunuzi ya umma kwenye manunuzi, usambazaji na uuzaji wa tani 4500 za mbolea yenye thamani ya Sh, 7,915,794,880 uliobaishwa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani ya TFC.
SOMA TANZANIA PANORAMA BLOG KUJUA MENGI ZAIDI YALIYOBAINIKA KWENYE UKAGUZI WA MANUNUZI, USAMBAZAJI NA UUZAJI WA MBOLEA ULIOFANYWA TFC.