Monday, July 7, 2025
spot_img

UNYANYAPAA WATIKISA SEKONDARI YA BUNJU A

DET’U KAKELAKAMBUZI

MAPAMBANO ya maneno makali baina ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunju A, Bupe Mkondola na Mwalimu Angelight Kimaro (pichani hapo juu) anayefundisha Somo la Kiswahili, yanaendelea.

Chanzo cha mapambano hayo kinadaiwa ni unyanyapaa unaofanywa na Mwalimu Mkuu Mkondola kwa Mwalimu Kimaro ambaye ni Albino.

Mwalimu Mkuu Mkondola naye amesema Mwalimu Kimaro siyo mtii wa maelekezo yake na amekuwa na akijibizana naye hivyo madai yake yanashughulikiwa na uongozi wa wilaya.

Aliyeibua taarifa za kuwepo kwa mapambano hayo ni Mwalimu Kimaro ambaye katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni, alisema yupo kwenye wakati mgumu lakini atapambana bila kuchoka dhidi ya unyanyapaa anaofanyiwa na Mwalimu Mkuu Mkondola.

Alisema Mwalimu Mkuu Mkondola anamuhukumu kuwa hana uwezo wa kufundisha kidato cha nne kwa sababu ya ulemavu wa ngozi alionao wakati uwezo huo anao.

Mwalimu Kimaro alisema, Mwalimu Mkuu Mkondola anaamini kuwa ulemavu aliona unamfanya asiwe na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi unaotakiwa hivyo amekuwa akitumia madaraka aliyonayo kuingilia utendaji wake wa kazi na kumnyanyapaa.

“Huu mgogoro umedumu muda mrefu. Alinikuta nafanya majukumu yangu yote kwa ushirikiano na wenzangu, lakini ujio wake umebadilisha mambo mengi,” alisema Mwalimu Kimaro.

Akizungumzia mambo yaliyobadilika baada ya Mwalimu Mkuu Mkondola kuhamishiwa shuleni hapo, alisema ni pamoja na kumnyima nafasi ya  kufundisha kidato cha nne.

“Huyu mama anashindwa kung’amua kati ya maumbile niliyonayo na taaluma ninayotakiwa kuitumikia. Mtazamo wake siwezi kufanya majukumu yangu yakaleta mafanikio kwa sababu anadai sina uwezo wa kuona vizuri.

“Utaratibu uliopo ofisini, kila mwalimu anaanza na mwanafunzi kidato cha kwanza hadi kidato cha nne. Tupo walimu 48 lakini anayenyimwa kufundisha kidato cha nne ni mimi peke yangu,” alisema Mwalimu Kimaro.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunju A, Bupe Mkondola

Alisema anatambua ni jukumu la Mwalimu Mkuu kumbadilisha mwalimu kutoka kidato kimoja kwenda kingine lakini hata anapoamua hivyo hapaswi kutumia maneno yenye unyanyapaa na kudhalilisha utu wa mtu kama anavyofanya kwake.

Alisema Mwalimu Mkuu Mkondola alimzuia kufundisha kidaro cha nne kwa kile alichoeleza kuwa ana uoni hafifu na alitangaza kwa walimu wenzake kuwa hafai kufundisha darasa hilo na kwamba maneno hayo yalimuumiza na kumfanya asiaminiwe na walimu wenzake.

“Niliamua kupambana kwa nguvu zangu zote bila kuomba msaada au kulalamika kwake kwani nilitaka kumthibitishia kuwa naweza. Nilifanikisha kuwafaulisha wanafunzi wote wa darasa langu lakini bado alikataa kusaini cheti changu cha kufaulisha wanafunzi wote huku vya wengine wote akivisaini. Nilijisikia kubaguliwa ila nilipata faraja kwa kuwa wenzangu walinikubali,” alisema Mwalimu Kimaro.

Aliongeza kuwa licha ya kuwa na udhuru wa kupangiwa zamu ili asikae juani kwa muda mrefu, Mwalimu Mkuu Mkondola alimempanga awe anashika zamu na kwamba alifanya hivyo ili apate sababu ya kumuondoa kufundisha kidato cha nne.

Alipoulizwa Mwalimu Mkuu Mkondola kuhusu madai ya Mwalimu Kimaro dhidi yake, alisema hajapata kumnyanyapaa bali siyo mtii wa maagizo yake hivyo madai yake yanashughulikiwa na uongozi wa ngazi ya wilaya.

Tanzania PANORAMA Blog imewatafuta bila mafanikiio Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Afisa Elimu kuzungumzia jambo hilo. Jitahada za kuwapa zinaendelea.

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya