Tuesday, December 24, 2024
spot_img

BALILE ‘ALIA’ CHUKI AKIHOJIWA SKANDALI YA KUGHUSHI

RIPOTA PANORAMA

DEODATUS Balile, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri linalomilikiwa na Kampuni ya Jamhuri Media Limited,  amelalama kuchukiwa alipokuwa akihojiwa kuhusu skandali ya kughushi mkataba wa ajira kati ya kampuni yake na Mwandishi wa Habari, Charles Ndagula.

Balile, badala ya kujibu maswali aliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu skandali inayoiandama Jamhuri Media Limited na yeye mwenyewe kutajwa moja kwa moja na Ndagula kwenye skandali hiyo, alitoa maneno yasiyofaa, akataja chuki, akalalama anafanyiwa uchimvi hivyo hataongea tena.

Kampuni ya Jamhuri Media Limited inachunguzwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kughushi saini, majina na sanduku la barua kwenye mkataba wa ajira baina yake na Mwandishi wa Habari Ndagula.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kuwepo kwa uchunguzi wa skandali hiyo na kueleza kuwa umekwishakamilika. Jalada la uchunguzi lilifunguliwa Novemba 2022 likiwa na namba KR/CD/PE/72/2022.

Balile naye alithibitisha kampuni anayoiongoza kuchunguzwa kwa skandali hiyo kwa kueleza kuwa kampuni yake imekwishawasilisha ushahidi wote mahakamani ikiwa ni pamoja na mkataba wa ajira wa mwaka mmoja iliyoingia na Ndagula chini ya mradi wa Mfuko wa Wakfu wa Waandishi wa Habari (TMF.)

Katika mahojiano aliyoyafanya awali na Tanzania PANORAMA Blog, pamoja na mambo mengine, Balile alisema alimwambia Ndagula Mungu atasimama upande wa haki nao watadai haki yao kesi ikiisha na akaongeza kuwa atashukuru habari kuhusu skandali hiyo ikiandikwa kwani itasaidia jamii kupima kati ya Ndagula na Jamhuri Media Limited nani anasema kweli.

Akizungumzia skandali hiyo hivi karibuni, Ndagula alisema alianza kuandika habari kwenye Gazeti la Jamhuri kama mwandishi wa habari wa kujitegemea (freelance journalist) 2017 bila kulipwa chochote.

“Nilianza kuwapelekea habari mwaka 2017 kama freelance na sikuwahi kulipwa mpaka 2019 walipoona kazi yangu ni nzuri, wakathamini mchango wangu wakaona kuna haja ya kuniajiri. Hiyo ni miaka miwili baada ya kuwa nawatumia story bila kulipwa chochote,” alisema Ndagula.

Alisema 2019 alipigiwa simu na Manyilizu Mageni ambaye alimuomba taarifa zake za benki kisha akamtumia Shilingi 450,000 kwa maelekezo kwamba anatakiwa kwenda Ofisi za Jamhuri Media Limited zilizopo Dar es Salaam kwa ajili ya kusaini mkataba wa ajira.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa.

Ndagula alisema alipofika Dar es Salaam alikutana na mwandishi wa habari mwingine aliyemtaja kwa jina la Editha Majura, aliyeitwa kutoka Dodoma kwa dhumuni la kwenda kusaini mkataba kwenye kampuni hiyo.

Alisema akiwa Dar es Salaam, hakusaini mkataba wa ajira na badala yake Balile alimwambia arudi Moshi kwa sababu mkataba wake una upungufu hivyo unarudishwa kwa mwanasheria wa kampuni kwa ajili ya kurekebishwa kisha atatumiwa ili ausaini.

“Siku tuliyofika, kesho yake kulikuwa na mafunzo ya hao TMF, tukaingia kwenye mafunzo hatukwenda ofisini, siku iliyofuata ndiyo tukaenda ofisini tukakaa hapo ofisini tukaongea badaaye Balile akanambia nirudi Moshi mkataba wangu una upungufu kidogo wataufanyia marekebisho halafu nitatumiwa nisaini lakini niendelee tu na kazi.

“Kwa hiyo mimi na Editha tukaondoka pale ofisini lakini hakuna mtu aliyemuuliza mwenzake kama amechukua mkataba ila Manyilizu aliniuliza kama nimepewa mkataba nikamwambia hapana, Balile amesema una upungufu mpaka waurekebishe.

“Nikarudi Moshi, nikaona mshahara umeanza kuingia, baada ya miezi miwili nikawakumbusha kuhusu mkataba nikaambiwa niendelee na kazi bado mwanasheria anaupitia,” alisema Ndagula.

Alisema mwaka 2020 alitumiwa barua ya kupunguziwa mshahara ikieleza uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao walichokaa wafanyakazi kisha akaanza kuingiziwa kwenye akaunti yake Shilingi 70,000.

Alisisitiza kuwa katika kipindi chote hicho hakuwahi kusaini mkataba wa ajira lakini alikuwa akilipwa mshahara kama mfanyakazi na aliamua kufungua shauri kwenye Tume ya Uamuzi na Usuluhishi (CMA) akilalamikia mshahara wake kupunguzwa bila kushirikishwa na wakati shauri hilo likiendelea kusikilizwa ndipo alipobaini kuwepo kwa mkataba ambao hakuhusika kuusaini.

“Mkataba ninaodai wameghushi wa 2017 siyo sehemu ya madai yangu CMA. Madai yangu ni mapunjo ya mshahara, kesi yangu ni kuanzia mwaka 2020 waliponipunguzia mshahara.

“Wao waliomba ruzuku TMF kwa ajili ya kuchunguza mambo ya bandarini. Na ili wapewe hiyo ruzuku ilikuwa lazima wawasilishe mikataba ya wafanyakazi. Sasa isingekuwa hii kesi mimi nisingejua lolote kuhusu mkataba huo, wao waliuleta wakijua kuwa mimi sitajua lolote,” alisema Ndagula.

Mwandishi wa Habari, Charles Ndagula.

Tanzania PANORAMA Blog, jana ilimuhoji Balile kama madai ya Ndagula kuwa hakuwahi kusaini mkataba wa ajira na Jamhuri Media Limited na iwapo ni kweli kuwa mwandishi huyo alikuwa akiliandikia gazeti hilo kwa miaka miwili mfululizo bila kulipwa chochote.

Balile aliulizwa pia kama alimuita Ndagula jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusaini mkataba na iwapo ni kweli mwandishi huyo hakusaini mkataba huo baada ya yeye kumwambia una upungufu hivyo unapaswa kurekebishwa kwanza ndipo atumiwe asaini, lakini hakuwahi kutumiwa.

Akijibu, Balile alisema suala hilo liko mahakamani na kuongeza kuwa anadhani mwandishi huyo anapaswa kupimwa afya ya akili, kisha akajibu tena kuwa asubiri kama alivyoahidiwa suala hilo lifikishwe mahakamani.

“Kaka hili suala liko mahakamani, jambo moja tu, nadhani Charles anapaswa kupimwa afya ya akili. Kama haya yapo asubiri tufikishwe mahakamani kama alivyoahidiwa nasi tutawasilisha ushahidi unaotakiwa,’ alijibu Balile.

Tanzania PANORAMA Blog alimuuliza Balile kuhusu mkanganyiko wa majibu yake yaliyoeleza kuwa suala hilo lipo mahakamani na hapo hapo akisema iwepo subira mpaka litakapofikishwa mahakamani naye alijibu kuwa kesi ipo Machi 8, 2024 na kushauri Tanzania PANORAMA ifike mahakamani.

Alipoulizwa kesi ipo mahakamani gani alijibu tofauti kuwa anaelewa mchezo unaoendelea kati ya mlalamikaji na anayemuhoji na kwamba hajasahau hitoria.

Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza Balile kuhusu mchezo anaodai kuwepo naye alisema chuki iwekwe kando, iandikwe habari kama habari na kuhoji ni mara ngapi ameandikwa hivyo anachokishuhudia ni mwendelezo kisha akahitimisha majibu yake kwa kusema hatajibu chochote tena.

Haya yanajiri sasa huku kukiwa na fukuto la chini kwa chini kuhusu waandishi wa habari  kutopewa mikataba ya ajira, kulipwa kidogo, kufanya kazi bila kulipwa na madai kuwa  baadhi ya waandishi  na wahariri walio nje kazi ya uandishi na wale waliopata kukamatwa na kushtakiwa mahakamani kwa tuhuma za makosa ya rushwa, wamekuwa wakijipatia mamilioni ya fedha kutoka taasisi na mashirika  ya umma kwa kazi hewa.

Aidha, yapo majukwaa ya wahariri yenye watu waliostaafu kazi, wasiokuwa na kazi na waliopo kazini yanayolipwa mamilioni ya fedha za umma na mashirika na taasisi za serikali kwa ajili ya kazi za kiuandishi, warsha na semina ambazo hazina tija inayostahili kwa mashirika na taasisi zinazotoa mamilioni hayo.

Tanzania PANORAMA Blog inaandaa ripoti ya jinsi fedha za umma zinavyoliwa kwa kutumia kivuli cha majukwa ya wahariri, ambayo itataja kampuni na taasisi za umma zilizolipa mamilioni ya fedha kwa majukwaa hayo na aina ya watu waliolipwa kwa ajili ya warsha, semina na kuandika habari.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya