RIPOTA PANORAMA
JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linachunguza tuhuma za kughushi mkataba wa ajira ilioingiwa baina ya Kampuni ya Jamhuri Media Limited na Mwandishi wa Habari, Charles Ndagula.
Jamhuri Media Limited inayomiliki Gazeti la Jamhuri imefunguliwa Jalada la Uchunguzi katika Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kilimanjaro, Novemba 2022 lenye namba KR/CD/PE/72/2022 ikituhumiwa kughushi saini, majina na sanduku la barua kwenye mkataba wa ajira baina yake na Ndagula.
Aliyeifikisha polisi, Jamhuri Media Limited ni Ndagula ambako ameomba wataalamu wa maandishi wa polisi wauchunguze mkataba huo akidai zaidi kuwa Oktoba Mosi 2017, inayosomeka kwenye mkataba kuwa ndiyo tarehe, mwezi na mwaka alioajiriwa, navyo ni batili.
Mkataba unaodaiwa kuwa ni wa kughushi ambao Tanzania PANORAMA Blog imeuona umesainiwa na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile, Meneja Usambazaji Msaidizi, Leonce William, Mwandishi wa Habari Charles Jacob Ndagula, (Retained Reporter) na Manyilizu Magembe ambaye ni mtunza fedha (Cashier.)
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kuwepo kwa uchunguzi huo wakati wa mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog yaliyofanyika jana kupitia simu yake ya kiganjani.
Alisema, uchunguzi umeishakamilika lakini alikataa kuzungumza ni nini kilichobainika kwa kile alichosema hilo litaelezwa na wataalamu wa polisi baada ya kesi hiyo kufikishwa mahakamani.
Sambamba na uthibitisho wa RPC Maigwa, tayari Ofisi ya Kamanda wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Mkoa wa Kilimanjaro (RCO) imeeleza kuwa sanduku la barua lililotumika kwenye mkataba baina ya Jamhuri Media Limited na Ndagula, siyo la Ndagula na kwamba mwandishi huyo hajawahi kumiliki sanduku la barua.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa
Kwa mujibu wa barua ya polisi iliyoandikwa Oktoba 10, 2023 kwenda kwa Ndagula ikiwa na kumbukumbu namba KR.CID/B.1/7/VOL.XIX/130 na kusainiwa na SSP Cassin Kayombo, ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona, wataalamu wa maandishi wa Jeshi la Polisi wa Makao Makuu Ndogo ya Polisi Dar es Salaam wako mbioni kukamilisha sehemu muhimu ya uchunguzi wao kuhusu uhalali wa madai ya Ndagula kuwa saini na majina kwenye mkataba huo yameghushiwa.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni, Ndagula alisema Jamhuri Media Limited iliomba ruzuku TMF kwa ajili ya kuandika habari za uchunguzi na moja ya masharti ya kupata ruzuku hiyo ni kuwasilisha mikataba ya waandishi watakaohusika kuandika habari na makala zinazoombewa fedha.
Alisema Jamhuri Media Limited walighushi majina yake, saini na sanduku la barua na kuwasilisha mkataba walioghushi TMF na kwamba alibaini hilo baada ya kuingia kwenye mgogoro wa mapunjo ya mshahara wake na kampuni hiyo.
Tanzania PANORAMA Blog inafahamu kuwa April, 2020 Jamhuri Media ilipunguza asilimia 50 ya wafanyakazi wake na waliosalia kazini iliwapunguzia asilimia 80 ya mishahara yao kwa sababu ya kuyumba kiuchumi lakini iliendelea kuwalipia NSSF, WCF, PAYE na kodi nyingine na kwamba uamuzi huo iliufikia baada ya kufikia makubaliano na wafanyakazi hao kwenye kikao kilichoketi April 29, 2020.
Ndagula anasema hana taarifa na kikao hicho; hakushiriki kwenye maamuzi yaliyofikiwa hivyo alifungua shauri la mapunjo ya mshahara wake Tume ya Uamuzi na Usuluhishi (CMA) na wakati shauri hilo likisikilizwa, moja ya nyaraka iliyowasilishwa na Jamhuri Media Limited kuthibitisha utetezi wake ni mkataba wa ajira ya Ndagula ambao yeye baada ya kuuona aliutilia shaka.
“Baada ya kuwasilisha kielelezo hicho nilikitilia shaka, nikaomba Tume ikubali ombi langu nyaraka hiyo ichunguzwe na wataalamu wa maandishi wa Jeshi la Polisi na nilifungua Jalada la Uchunguzi Ofisi ya RCO Kilimanjaro, Novemba 2022, lenye nambari KR/CD/PE/72/2022,” alisema Ndagula.
Mwandishi wa Habari, Charles Ndagula
Balile alipoulizwa jana kuhusu hilo, alisema ni kweli Ndagula amefungua kesi hiyo lakini Jamhuri Media Limited imewasilisha ushahidi wote mahakamani tangu alipopewa mkataba wa mwaka mmoja chini ya mradi wa TMF, bank statement na jinsi fedha zilivyokuwa zinaingia kwenye akaunti yake tangu siku ya mkataba na pia alivyokaa bila kuandika habari hata moja kuanzia 2019 hadi 2022 huku akilipwa mshahara.
“Siyo hiyo tu, bima ya afya iliyokuwa inalipiwa miaka yote na Jamhuri imetumika muda wote. Anasema hajawahi kusaini mkataba na sisi tumeghushi saini yake na kulazimisha kuingiza hela kwenye akaunti yake ila hasemi kwanini Jamhuri ilikuwa inamlipa kila mwezi na sisi tuliipata wapi akaunti yake na ni kwa maslahi yapi tulazimishe kumlipa mtu katika nyakati hizi.
“Sehemu nyingine anasema tulikubaliana bila maandishi kumlipa Shilingi 600,000, akiulizwa mkataba anasema ulikuwa ni kwa kauli, aliuingia na nani, hasemi.
“Kwa maana hiyo sisi tunaheshimu uhuru wa mahakama, tunatunza kila risiti ya gharama tunazoingia kupeleka mashahidi Moshi na Wakili na kesho (leo) kuna kesi hiyo Moshi. Tumepeleka mashahidi na Wakili.
“Nilimwambia Mungu atasimama upande wa haki nasi tutadai haki yetu kesi ikiisha,” alisema Balile.