MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ni Taasisi ya Serikali iliyokasimiwa wajibu wa kusimamia utendaji na uendeshaji wa shughuli za bandari za mwambao na za maziwa makuu nchini.
Katika kutelekeza wajibu huo, TPA inazingatia malengo ya serikali yaliyo kwenye bajeti yake ya kila mwaka ambayo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapunduzi (CCM), kilichopita kwa watanzania kikiahidi pamoja na mambo mengine; serikali yake kusimamia kwa ufanisi utendaji na uendeshaji wa TPA.
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025, inaelekeza serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati na maelekezo mahususi ya kuboresha na kuimarisha utendaji wa TPA yametolewa katika ukurasa wa 92 wa ilani hiyo.
CCM katika ilani yake kinaelekeza serikali kutekeleza miradi 11 ya uboreshaji Bandari ya Dar es Salaam, miradi mitano katika Bandari ya Tanga, sita katika Bandari ya Mtwara, Bandari za Ziwa Victoria miradi mitano, Ziwa Tanganyika miradi mitano na Ziwa Nyasa miradi minne.
Katika kutekeleza hilo, Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 iliyosomwa bungeni na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ilieleza shughuli zitakazozingatiwa na TPA kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kuwa ni pamoja na kuendeleza miundombinu na huduma za kibandari.
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025
Serikali ilieleza katika bajeti yake hiyo kuwa TPA imekasimiwa majukumu ya kusimamia na kudhibiti huduma za bandari, kulinda mazingira na usalama wa bandari kwa viwango vinavyokubalika pamoja na kuweka mazingira mazuri yatakayowavutia wawekezaji kuwekeza katika sekta ya bandari.
Kazi ya kutangaza bandari kimasoko pamoja na kushirikisha na kusimamia sekta binafsi katika uendeshaji wa shughuli za kibandari nayo imetajwa na serikali kuendelea kufanywa na TPA.
Katika bajeti hiyo, TPA ilitenga jumla Shilingi bilioni 100.11 ambazo ni fedha za nje kutoka Benki ya Dunia (WB) na Shilingi bilioni 650.00 kutoka vyanzo vya mapato vya ndani ya TPA kwa ajili ya kutekeleza kazi zake mbalimbali.
Makala haya maalumu, yamebeba majibu ya kazi zilizofanywa na TPA kutoka kwenye taarifa rasmi za mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, lakini zaidi ni taarifa rasmi kwa umma kuhusu utendaji na uendeshaji wa shughuli za mamlaka hiyo ambao umekuwa wa mafanikio.
Mafanikio iliyopata TPA kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yanaakisi utekelezaji wa bajeti ya serikali na ahadi za CCM kwa wananchi na yanachora taswira ya mafanikio makubwa zaidi kama yalivyoainishwa kwenye mipango mikakati ya uimarishaji shughuli za uendeshaji na utendaji wa TPA.
Waziri Makame Mbarawa
Kiujumla, taarifa za TPA zinaonyesha kuwa mwenendo wa shughuli za mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 zilikuwa za mafanikio makubwa ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2021/2022. Katika rekodi za sasa ambazo hazijawahi kufikiwa kwa muda wote wa uhai wa TPA, kiwango cha mizigo iliyohudumiwa kimepanda kwa wastani wa asilimia 19.8.
Wadau na wafuatiliaji wa mambo ya shughuli za uendeshaji bandari waliotoa maoni yao kuhusu mwenendo huo, wameeleza kuwa rekodi ya kuhudumia tani milioni 24.899 ni ya kujivunia na kwamba ni mafanikio yanayoielekeza mamlaka kwenye malengo iliyokusudiwa kuyafikia baada ya maboresho ya msingi kufanyika.
Taarifa zinaonyesha kuwa tayari hatua za msingi za kuimarisha utendaji na uendeshaji wa bandari zinazosimamiwa na TPA zimekwishaanza na zinaendelea kuchukuliwa kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo na pia maslahi ya taifa yakiwekwa mbele na hasa kwenye uwekezaji na ushirikishwaji wa sekta binafsi.
Ripoti ya TPA ya mwaka wa fedha 2022/2023 ya utendaji na uendeshaji ni ripoti yenye mafanikio ambayo umma una haki ya kijivunia na lengo la TPA ni kuyaendeleza mafanikio hayo.
Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, idadi ya makasha ya mizigo yaliyohudumiwa imepanda kwa kiwango cha asilimia 13.7 ikilinganishwa na idadi ya makasha ya mizigo yaliyohudumiwa mwaka 2021/2022. Kitakwimu, mwaka 2022/2023 makasha ya mizigo yaliyohudumiwa ni 936,286.
Bandari ya Tanga
Mchanganuo wa makasha ya mizigo yaliyohudumiwa kwenye bandari zinazosimamiwa na TPA unaonyesha katika Bandari ya Dar es Salaam, (Terminal 11) ilivuka lengo lililowekwa kwa kuhudumia makasha 784,909, sawa na asilimia 120.7 ya lengo la kuhudumia makasha 650,500 ambalo ni ongezeko la asilimia 22.
Rekodi nyingine katika utoaji huduma kwa makasha ya mizigo ilivukwa upande wa mizigo ya jumla (general cargo), ambapo lengo lilikuwa kuhudumia makasha ya mizigo 136,400 na badala yake yaliyohudumiwa ni makasha ya mizigo 138,054, sawa na ongezeko la asilimia 101.9 ya lengo lililowekwa.
Katika Bandari ya Mtwara, lengo lilikuwa kuhudumia makasha 2,700 na badala yake idadi hiyo iliongezeka zaidi ya marudufu kwa makasha ya mizigo 6,079 kuhudumiwa kwenye bandari hiyo.
Bandari ya Tanga ambayo iko kwenye mkakati maalumu wa TPA kuimarisha utendaji wake, ililenga kuhudumia makasha ya mizigo 9,200 lakini badala yake ilihudumia makasha ya mizigo 7,244.
Magari yaliyohudumiwa kwa mwaka 2022/2023 ni ‘uniti’ 187,814. Hata hivyo, kiwango hiki ni pungufu kwa asilimia 7.9 ikilinganishwa na kiwango cha mwaka 2021/2022.
Idadi ya meli zilizohudumiwa katika bandari za mwambao na maziwa makuu kwa mwaka 2022/23 ni 5,675 ambayo ni asilimia 118.1 ya lengo lililowekwa la kuhudumia meli 4,804.
Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara zilihudumia meli 2,253 na meli zilizohudumiwa kwenye maziwa makuu ni 3,422. Hili ni ongezeko la asilimia 21.1 la utoaji huduma ikilinganishwa na mwaka 2021/2022.
Meli zilizohudumiwa kulingana na vipimo vya uzito (GRT) ni milioni 40,534, sawa na asilimia 116.4 ya lengo lililowekwa la GRT 34,821. Utoaji huduma huu uko juu kwa wastani wa asilimia 18.4, ukilinganishwa na wa mwaka 2021/2022.
Kwa upande wa mapato, TPA imevuna Shilingi trilioni 1,394.585. Kiwango hiki cha mapato ni cha juu kwa asilimia 27.3 ikilinganishwa na mapato yaliyokusanywa mwaka 2021/2022.
Kwenye mapato hayo, matumizi yalikuwa Shilingi bilioni 843,110 ambayo ni asilimia 129.1 ya lengo lililowekwa la Shilingi bilioni 653,147 na zaidi ya matumizi ya mwaka 2021/2022 kwa asilimia 50.8.
Mwaka 2022/2023, ziada katika mapato ilikuwa Shilingi bilioni 551,474 ambayo ni sawa na asilimia 117.4 ya lengo lililowekwa la kuwa na ziada ya Shilingi bilioni 537,126.