Monday, December 23, 2024
spot_img

BARABARA HIFADHI YA SERENGETI KUJENGWA KWA TABAKA GUMU

GEMBAGU NJAMITI, Serengeti

NIMEKUTANA na kufanya mahojiano ya ana kwa ana na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mhandisi Mshauri, Richard Matolo (Phd) kuhusu hofu ya kuathirika kwa sekta ya utalii nchini kwa sababu ya ubovu wa miundombinu ya barabara kuu za Hifadhi ya Serengeti, ambayo hupokea watalii wengi kutokana na umaarufu wake duniani.

Mhandisi Dk. Matolo aliniarika ofisini kwake mapema wiki hii ili kutoa ufafanuzi wa kitaalamu kuhusu changamoto ya miundombinu ya barabara kwenye Hifadhi ya Serengeti na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na changamoto hiyo.

Katika mahojiano haya, Mhandisi Dk. Matolo anazungumzia sababu ya kuharibika kwa barabara hizo na kuainisha mipango ya muda mfupi na muda mrefu wa matengenezo, pamoja na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kufanya matengenezo makubwa kwenye barabara za hifadhi hiyo.

Alinikaribisha ofisini kwake kwa kujitambulisha yeye kwanza; ‘Karibu sana mwandishi, mimi naitwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mhandisi Mshauri, Daktari, Richard Matolo. Ninazo taarifa zako kuwa una maswali ya kutuuliza TANAPA, nimeona uje ili nikupe majibu na ufafanuzi wa mambo unayotaka kujua. Nipo tayari kujibu maswali yako.’

Ninaanza kwa kumuuliza Mhandisi Dk. Matolo idadi ya barabara kuu zilizopo kwenye Hifadhi ya Serengeti, naye anajibu.

‘Hifadhi ya Serengeti ina barabara kuu nne; ya kwanza inatoka Golini inapita Nabi inakwenda hadi Seronera. Hii ina urefu wa kilomita 68. Ya pili inaanzia Seronera mpaka Ndambaka kwenye geti la kutokea Wilaya ya Magu, ina urefu wa kilomita 121.

‘Barabara ya tatu inaanzia Seronera mpaka Geti la Ikoma na urefu wake ni kilomita 30. Kisha kuna inayoanzia Banagi inapita Lobo inakwenda hadi Lango la Klein’s, ina urefu wa kilomita 72.’

Roli likimwaga kifusi kwenye barabara kuu ya Seronera hadi Golini iliyoharibiwa na mvua kubwa za El nino zinazoendelea kunyesha nchini.

Anaweka tuo, nami namuuliza swali la pili kuwa ni barabara zipi zilizoharibika kiasi cha kutopitika, naye anajibu.

‘Mvua kubwa inayonyesha imeharibu sehemu ya barabara zetu  kwenye hifadhi lakini zinapitika ndiyo maana watalii wapo hifadhini. Baadhi ya sehemu zimeharibika hivyo magari yanapita kwa shida.

‘Hizi mvua za El nino zimesababisha uharibifu wa miundombinu sehemu mbalimbali nchini, siyo kwenye Hifadhi ya Serengeti tu, bali sehemu nyingi za nchi kuna athari kubwa za mvua hizi.

‘Babaraba za hifadhini zinatumiwa na wasafiri wote kwa maana ya watalii na wananchi. Mabasi ya abiria na maroli ya mizigo yanazitumia. Hili ni muhimu sana watu kujua kuwa barabara kuu kwenye Hifadhi ya Serengeti zimeharibika zaidi kwa sababu hazitumiki kwa shughuli za hifadhi na utalii tu, bali zinaunganisha hifadhi na maeneo ya nje ambayo ni muhimu kiuchumi.

‘Kwa hiyo watumiaji wote wa barabara wanazitumia ikiwa ni pamoja na mabasi na maroli. Kiujumla barabara zote zimeguswa na athari za mvua kubwa inayoendelea kunyesha.’

Baada ya jibu hilo, ninamuuliza ni hatua gani zinazochukuliwa na TANAPA kukabiliana na changamoto hiyo, naye anajibu kwa kusema.

‘Sehemu zote korofi tunashughulika nazo. Tunazitambua na kuzifanyia matengenezo. Ila niseme kwamba serikali ikijenga ile ‘bypass’ (barabara ya pembeni) maana serikali inatarajia kujenga ‘bypass’ ambayo itapita kusini mwa Serengeti ambayo itatumiwa na magari makubwa, maroli na mabasi, hiyo  itapunguza mchango mkubwa wa magari haya kwenye uharibifu wa miundombinu ya barabara za Hifadhi ya Serengeti.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Juma Kuji (katikati) akiwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mhandisi Mshauri, Dk. Richard Matolo aliye kulia kwake, wakikagua barabara kuu ya Hifadhi ya Serengeti inayotoka Seronera hadi Golini iliyoharibiwa na mvua za El nino zinazoendelea kunyesha nchini.

‘Magari makubwa pamoja na mvua kubwa za Eli nino ambazo hazijawahi kunyesha kwenye Hifadhi ya Serengeti tangu mwaka 1959 zimekuwa na athari kubwa sana kwenye hifadhi. Na siyo tu barabara, bali ukiangalia hifadhi nzima kwa ujumla imejaa maji.

‘Sasa kama hifadhi nzima ipo kwenye maji hatuwezi kushikana uchawi kwa barabara kuharibika. Barabara ya Seronera hadi Golini ndiyo barabara inayotumika zaidi katika Hifadhi ya Serengeti na ndiyo iliyoharibika sehemu nyingi. Ni barabara muhimu sana kwa sababu hata ukiangalia takwimu, wageni wanaoingia Nabi ni wengi kuliko wanaoingia kupitia kwenye malango mengine. Kwa hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA tunaipa kipumbele. Tayari Kamishna Mkuu mwenyewe ametoka ofisini kwake kwenda kusimamia ukarabati wake na hivi tunavyoongea sehemu zote korofi zinatengenezwa.

‘Kikubwa ambacho tunafanya sasa ni uboreshaji. Kwanza tunakagua kutambua maeneo yote korofi, maeneo ambayo yameathirika zaidi kutokana na mvua hizi za El nino. Tunakagua kutambua maeneo korofi na kuyafanyia ukarabati wa haraka ili wageni na watumiaji wengine wa barabara wasikwame kuingia hifadhini.

‘Lengo la TANAPA baada ya mvua kupungua ni kuzifanyia ukaratabati wa kawaida barabara zote. Huo ni mpango wa muda mfupi.

‘Lakini mpango wa muda mrefu ni kuziimarisha barabara za hifadhini ambazo zina watumiaji wengi. Tunalazimika kuziimarisha kwa sababu tangu kuanzishwa kwa hifadhi hizi; kwa mfano ukichukua Hifadhi ya Serengeti ambayo ndiyo imeanzishwa zamani zaidi, mwaka 1959, matengenezo ya barabara zake yamekuwa yakifuata sera zinazolinda uendelezaji maeneo ya ndani ya hifadhi.

‘Sera hizo zinaweka mipaka ya matumizi ya nyenzo ndani ya hifadhi kwa sababu ya kuogopa kuleta spishi ya kigeni. Sasa chanzo cha kokoto zilizopitishwazamani na ambazo zinaendelea kutumika mpaka leo zimeonyesha kupungua kwa maana kwamba zile kokoto nzuri zimepungua kwa kiwango kikubwa na hilo limesababisha changamoto kubwa kwenye matengenezo ya barabara za hifadhini kwa kutumia utaratibu tuliokuwa nao.

‘Tunafikiria kuchukua kokoto nje ya hifadhi ingawa ni nje ya sera, lakini ukiangalia umbali wa usafirishaji ni mkubwa sana kiasi ambacho thamani ya fedha haitakuwepo.

‘Kwa sababu hiyo, shirika pamoja na wenzetu wa Hifadhi ya Ngorongoro imebidi kukaa tena mezani kufikiria njia nyingine. Majaribio mbalimbali yamewahi kufanyika, yote yakiwa na nia njema ya kunusuru barabara hizo kuu.

Simba akitembea taratibu kwenye eneo tepe katika Hifadhi ya Serengeti. Sehemu kubwa ya Hifadhi ya Serengeti ambayo ina udongo tifutifu imekuwa tepe kwa sababu ya mvua za El nino zinazoendelea kunyesha.

‘Lakini kwa sababu ya changamoto ya udongo kuwa mbaya kwenye maeneo mengi ya hifadhi. Tumeshuhudia wote kwamba ni udongo wa pamba nyeusi. Asili ya udongo iliyopo kwenye hifadhi haisaidii kunusuru barabara hizo.

‘Tumefanya utafiti mwingine Ngerengere kuangalia kama tunaweza kutumia njia nyingine. Kujenga lami ndani ya hifadhi hairuhusiwi na haijafikiriwa sana na wahifadhi na waikolojia wa kwetu.

‘Sasa, tunafikiria kutumia tabaka gumu jambo ambalo wenzetu wa Ngorongoro wameishafanya maandiko ya kitaalamu na kuwasilisha UNESCO nao wamewaruhusu kuimarisha barabara yao kuu yenye urefu wa kilometa 83 kutokea lango la Londware hadi Golini.

‘Kwa hiyo, utaona kwanza wenzetu wakiweza kuimarisha kile kipande itakuwa salama zaidi lakini kwa upande wa kwetu ndiyo mtu akija atakuwa kama anakuja jehenamu kwa sababu barabara hazina kiwango kinachotakiwa.

‘Lakini faida kubwa tuliyonayo, Serengeti na Ngorongoro ziko kwenye mfumo mmoja wa kiikolojia. Changamoto za barabara zilizopo Ngorongoro zinafanana kabisa na zilizopo Serengeti hivyo hatutarajii kuja na andiko tofauti na sababu tofauti za kuwashawishi UNESCO kwenye jitihada zetu za kutaka kuimarisha barabara za Hifadhi ya Serengeti kwa kutumia tabata gumu.

Nilimkata kauli Mhandisi Dk. Matolo kwa kumuuliza kwa nini lazima kupata kibali cha UNESCO ili kukarabati barabara za hifadhi zetu naye anajibu.

‘Ifamike kuwa maeneo haya mawili ya Ngorongoro na Serengeti yanaitwa urithi wa dunia kwa mujibu wa vigezo vya UNESCO, hivyo huwezi kufanya uendelezaji mkubwa wa aina yoyote pasipo kuwahusisha kwani inaweza kuonekana kuwa tunapingana na vigezo ambavyo walivitumia kutangaza maeneo hayo kama urithi wa dunia. Hivyo lazima tuwahusishe, wasome maandiko na wayapitishe.

‘Ngorongoro wamewahusisha na wamepata kibali chao cha kuitengeneza barabara yao kwa kutumia tabaka gumu na hivi sasa wapo kwenye hatua za manunuzi. Kwetu ni faida kwa sababu tutatumia uzoefu wao kujenga hoja ambayo itakubalika na UNESCO kufanyia matengenezo barabara zetu za hifadhini Serengeti.’

Greda likitengeneza sehemu korofi ya barabara kuu ya Seronera hadi Golini katika Hifadhi ya Serengeti iliyoharibiwa na mvua za El nino

Ninamuuliza pia kuhusu hali ilivyo sasa kwenye daraja lililoharibika na kuzua mjadala hasi kwenye mitandao ya kijamii naye anajibu.

‘Wala halijaharibika bali maji yamezidi. Kama nilivyosema Hifadhi ya Serengeti haijawahi kupata mvua kubwa kiasi hiki toka kuanzishwa kwake. Unajua ngoja nikwambie kitu, makalavati yaliyo chini ya daraja hilo yaliziba kwa sababu ya kujaa kinyesi cha viboko, uchafu uliosombwa na maji kwenye mto na miti inayokuja na mafuriko. Maji sasa yanapita juu ya barabara.

‘Menejimenti ya TANAPA kwa kutambua hilo na kwa kupitia uongozi wa wizara na uongozi imara wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tuna mpango wa kujenga daraja ambalo litakuwa linapita juu. Wakati wa mvua kubwa kama hizi za hivi sasa daraja la juu litatumika na la chini linafungwa. Wakati wa kiangazi yote mawili yanaweza kutumika.

‘Kwa hiyo daraja halijaharibika wala kukatika bali maji yamezidi. Mambo ya mtandaoni ni muhumu kuyathibitisha kwanza kabla ya kuyachukua. Halijaharibika wala kukatika maana yake ni kwamba watu walikosa njia ya kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

‘Afande Kamishna wa Uhifadhi anafanya jitihada kubwa sana akipata msaada wa wizara kuhakikisha kuwa daraja la juu linajengwa mapema iwezekanavyo.

‘Sasa hivi kinachofanywa na menejimenti kwa sababu gharama za ujenzi wa daraja zitafika kwenye Shilingi milioni 800, shirika linafikiria kuweka kalivati juu ya mkondo wa maji, kalvati zenye midomo ya kuanzia mita 1.2 mpaka mita 1.50 zikipangwa pale zitakuwa kama kalvati nane au kumi, kisha tunamwaga deki juu kunyanyua barabara juu hivyo tutaruhusu maji kupita kwenye kalvati ambayo tutaweka.’

Mara simu yake ya mezani inaita, anaipokea na baada ya kusikiliza kidogo anairudisha kwenye kishikio chake, ananigeukia akisema. ‘Ninaitwa kwa afande CC, tukutane wakati mwingine nimalizie kujibu maswali yako.’ Tunaagana tukikubaliana kukutana tena kuendelea na mahojiano.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya