Monday, December 23, 2024
spot_img

EL NINO YATEPETESHA SERENGETI, WATAALAMU TANAPA WAKUNA VICHWA WAKIELEKEA UNESCO

MVUA za El Nino zinazoendelea kunyesha nchini; na ambazo hazijapata kunyesha kwenye Hifahi ya Taifa ya Serengeti kwa takriban miaka 64, zimeitepetesha na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja.

Tathmini ya wataalamu wa miundombinu ya barabara wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), zimeonyesha kuwepo kwa athari kubwa kwenye barabara kuu nne zinazopita ndani ya hifadhi na pia zinazounganisha hifadhi na maeneo mengine ya nchi na sasa wanakusudia kuliandikia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni kuomba kibali cha kuzifanyia matengenezo makubwa.

Kwa Mujibu wa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mhandisi Mshauri, Daktari Richard Matolo, barabara zilizoharibika kwa kiwango kikubwa zinatumiwa na watalii, wahifadhi na magari yanayosafirisha abiria na mizigo.

“Barabara za hifadhini zilizoharibika sana ni barabara kuu nne; ya kwanza inatoka Golini kupitia Nabi hadi Soronera yenye urefu wa kilomita 68, ya pili inatoka Soronera mpaka Dambaga, wilayani Magu yenye urefu wa kilomita 121, ya tatu inatoka Soronera mpaka Ikoma Gate, yenye urefu wa kilomita 30 na ya nne inatoka Banagi kupitia Robo hadi Cleans Gate, yenye urefu wa kilomita 72,” alisema Kamishna Matolo.

Alisema barabara hizo zimeharibika kwa sababu hazitumiki kwa shughuli za uhifadhi pekee bali zinaunganisha hifadhi na maeneo ya nje hivyo zinatumiwa pia na magari ya usafirishaji ya umma yakiwemo mabasi na maroli.

Kamishna Matolo alisema barabara hizo zinaunganisha hifadhi na maeneo muhimu ya kiuchumi yanayozunguka Hifadhi za Taifa.

Greda likitengeneza sehemu ya barabara inayotoka Soronera hadi Golini katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyoharibiwa na mvua kubwa za El Nino.

Sambamba na barabara na madaraja, sehemu nyingine za hifadhi ambazo Tanzania PANORAMA Blog imezifikia wakati wa ukaguzi uliofanywa na maafisa wa juu wa TANAPA ni eneo kubwa la hifadhi kujaa maji.

Kamishna Matolo amelizungumzia hilo akieleza kuwa ni kwa sababu udongo wa hifadhini ni tifutifu na haujapata mvua kubwa ya kiwango cha mwaka huu tangu mwaka 1959.

Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ina mpango wa kujenga barabara ‘bypass’ itakayopita kusini mwa Hifadhi ya Serengeti ambayo itatumiwa na magari makubwa ya kusafirisha mizigo na abiria na kwamba hilo litapunguza uharibifu wa barabara kuu za hifadhini.

Kamishna huyo alisema hivi sasa wataalamu wa TANAPA wanaendelea kutambua maeneo ya barabara yaliyoharibika na kuyafanyia ukarabati wa dharura ili magari yaendelee kupita.

“Lengo la TANAPA ni kutengeneza barabara kuu nne za ndani ya hifadhi ili ziweze kupitika wakati wote na hili litafanyika kwa kuziimarisha barabara hizo kwa kiwango cha kuweza kupitika wakati wote.

“Tunafikiria kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizo, wenzetu wa Ngorongoro wameishafanya maandiko ya kitaalamu wakawasilisha UNESCO nao wakawapa kibali cha kuimarisha barabara yao kuu yenye urefu wa kilomita 83 kutokea Lango la Rodwale hadi Golini,” alisema Kamishna Matolo.

Akiendelea, alisema uendelezaji mkubwa wa maeneo ya Hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro yanahitaji kibali cha UNESCO kwa sababu ni maeneo yanayotambulika na shirika hilo kama maeneo ya urithi wa dunia.

Akizungumzia daraja lililozua mjadala mitandaoni likidaiwa kuhatarisha maisha ya watalii, alisema daraja hilo halijaharibika bali lilijaa maji kutokana na wingi wa mvua ambazo Hifadhi ya Serengeti haijazipata tangu mwaka 1959.

.Alisema kalvati zilizowekwa kwenye daraja hilo zilizibwa na kinyesi cha viboko na uchafu uliosombwa na maji hivyo yakawa yanapita juu ya barabaraba.

“Hayo ni mambo ya mtandaoni, kama daraja lingekuwa limekatika au halipitiki mbona sisi na wewe mwandishi tumepita? Daraja limejaa maji kwa sababu ya mvua inayonyesha. Kilichotokea baada ya maji kujaa watu waliokuwa upande ule walishindwa kufika upande mwingine na hili tunalifanyia kazi,” alisema Kamishna Matolo.

Alisema mpango wa TANAPA ni kujenga daraja la juu ambalo litatumika wakati wa mvua na la lililopo sasa litakuwa limefungwa kwa sababu za kiusalama na kuongeza kuwa wakati wa kiangazi madaraja yote mawili yatatumika.

USIKOSE KUSOMA MAHOJIANO MAALUMU KESHO, KATI YA TANZANIA PANORAMA BLOG NA KAMISHNA MSAIDIZI, DK. MATOLO KUHUSU HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA TANAPA KUKABILIANA NA EL NINO KATIKA HIFADHI YA SERENGETI.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya