RIPOTA PANORAMA
MWENENDO wa mambo katika Tarafa ya Igagala, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora umezigawa mamlaka za serikali ambazo sasa zinazungumza lugha ‘gongana’ huku baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wakipaza sauti kuhusu athari za mgogoro wa mipaka baina ya vijiji vyao na Hifadhi ya Pori la Akiba la Igombe na Hifadhi ya Jamii ya ISAWIMA.
Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), zinakiri kuwepo kwa mgogoro wa mipaka baina ya hifadhi na vijiji lakini Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dk. Rashid Chuachua na Kamanda wa Uhifadhi wa Pori la Akiba Igombe, Justine Dyanabo wanakanusha katu katu.
Tanzania PANORAMA Blog inazo taarifa kuwa mgogoro wa mipaka kati ya hifadhi na vijiji umesababisha mazao ya wakulima kufyekwa, mifugo kuuawa, utozaji faini mifugo inayokamatwa ndani ya eneo la hifadhi kinyume cha utaratibu na ukiukaji wa haki za binadamu.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wananchi waliozungumza na Tanzania PANORAMA Blog, zinadai kuwa walinzi wa Hifadhi ya Jumuiya ya ISAWIMA, sambamba na askari wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA), wanafyeka mazao ya wakulima, wanaua mifugo na kukiuka haki za binadamu.
Inadaiwa, wanapoyafanya vitendo hivyo wanadai wanalinda mipaka ya hifadhi na kupambana na wale wanaingia na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi hizo mbili kinyume cha utaratibu.
Vyanzo mbalimbali vya habari vilivyozungumza na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu mgogoro wa mipaka ya ardhi baina ya hifadhi na vijiji vimeeleza kuwa ISAWIMA ni jumuiya ya uhifadhi iliyoundwa na vijiji 11 vilivyopo Tarafa ya Igagala, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.
Hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 2007 ikiwa na ukubwa na kilometa za mraba 18,000 na kwamba vijiji wanachama vilikubaliana kutoa wajumbe watatu kila kijiji kuunda baraza la uongozi na hao; walitakiwa kuchagua viongozi wakuu watatu wa jumuiya.
Imeelezwa zaidi kuwa yalifikiwa makubaliano kila mwananchi kuheshimu mipaka kwa mujibu wa sheria ndogo za halmashauri za vijiji na ambaye angekiuka angetozwa faini kwa mujibu wa faini elekezi kama zilivyoainishwa kwenye sheria ndogo za halmashauri.
Afande Benedict Wakulyamba
Vyanzo vyetu vya habari vimeeleza zaidi kuwa makubaliano mengine yalikuwa mapato ya faini kugawanywa asilimia 20 kijijini na asilimia 20 kwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri huku asilimia 60 ikibaki kwenye jumuiya na kwamba; kutokana na ongezeko la watu, kuzaliana na au kuhamia, mipaka ya vijiji na hifadhi itabadilishwa kila baada ya miaka mitano.
Hata hivyo, taarifa kutoka serikalini zinaonyesha kuwa ilitwaa sehemu kubwa ya eneo la ISAWIMA na kulitangaza kuwa Pori ya Akiba Igombe, kutokana na umuhimu wake kiuhifadhi na pili kwa sababu za kiusalama, lakini uwekaji mipaka kati ya hifadhi na vijiji uliibua migogoro ambayo Wizara ya Maliasili na Utalii na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imepata kuitolea ufafanuzi na kuchukua hatua za kuitatua.
Taarifa zisizokuwa na chembe ya shaka, zinaonyesha kuwa Agosti 7, 2023 aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Afande Benedict Wakulyamba alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akifafanua kuhusu hadhi ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii ya ISAWIMA kuwa, ilisajiliwa kama Community Based Organisation (CBO) kwa ajili ya kusimamia eneo lililotengwa kuwa hifadhi ya wanyapori.
Vyanzo vya habari vya uhakika zinaeleza kuwa barua ya Afande Wakulyamba ilikuwa inajibu barua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Julai 13, 2023 iliyokuwa ikiomba ufafanuzi kuhusu hadhi ya hifadhi hiyo.
Imeelezwa, Afande Wakulyamba alieleza kuwa wizara yake kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua ilianzisha Hifadhi ya Wanyamapori ya ISAWIMA inayounganishwa na vijiji 11 wanachama, mwaka 2007.
Kwamba kwa mujibu wa kanuni za maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (Wildlife Management Areas Regulation za mwaka 2018, ilianzishwa asasi ya kijamii, CBO na kusajiliwa kwa ajili ya eneo lililotengwa la Hifadhi ya ISAWIMA.
Akiendelea, Afande Wakulyamba alifafanua kuwa eneo hilo halikufikia hatua ya kutangazwa kutokana na uwepo wa migogoro na kuvamiwa, ambayo inaendelea kutatuliwa katika ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.
Waziri wa Kilimo na Uvuvi, Abdallah Ulega
Ameandika zaidi Afande Wakulyamba akimfafanua katibu mkuu mwenzake kuwa, mwaka 2021 sehemu kubwa ya Hifadhi ya ISAWIMA ilipandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba Igombe na kutangazwa na rais kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama.
Kisha Afande Wakulyamba aliweka wazi kuwa kutokana na mchakato huo, mipaka ya iliyokuwa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ISAWIMA na mipaka mipya ya Pori la Akiba Igombe ilionekana kupishana na kusababisha malalamiko kwa wananchi kuwa maeneo yao yamemegwa.
Aidha, eneo muhimu la utalii wa picha lenye ukubwa wa kilometa 65 liliachwa nje ya mipaka ya Pori la Akiba Igombe likiendelea kusimamiwa na CBO ya ISAWIMA, hivyo serikali ilielekeza liingizwe ndani ya Pori la Akiba Igombe.
Akihitimisha, anaeleza ipo haja ya kuihusisha CBO ya ISAWIMA kwa sababu baadhi ya vijiji vinaweza kuwa havichangii tena ardhi kwa ajili ya hifadhi ya wanyamapori jamii na kwamba wizara na halmashauri vilitarajiwa kufanya tathmini ya eneo husika kujua uhalisia wake.
Mbali na Wizara ya Maliasili na Utalii kuthibitisha kuwepo kwa mgogoro wa mipaka baina ya hifadhi na vijiji. TAMISEMI nayo inatambua kuwepo kwa mgogoro huo na imekuwa ikichukua hatua za kuutatua.
Hilo linathibitishwa na barua ya TAMISEMI iliyosainiwa na naibu katibu mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila ambaye wakati akikaimu nafasi ya katibu mkuu, Agosti 25, 2023 aliandika barua yenye kumbukumbu namba GB.203/350/01/14 kwenda Ikulu, Jeshi la Wananchi (JWTZ), Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Kilimo, Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi, Wakala wa Misitu, Kamishna wa TAWA na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Mazingira na Ufugaji Wenye Tija Tanzania (CHAWAUTA), kuelekeza watoe wajumbe watakaounda timu ya kutatua mgogoro unaohusisha mipaka ya hifadhi na vijiji.
Katika barua hiyo ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona, Mhandisi Mativila ambaye amethibitisha kuiandika, anasema Ofisi ya Rais TAMISEMI ilipokea barua ya Julai 13, 2023 kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu malalamiko ya wananchi wa Tarafa ya Igagala, Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora.
Mhandisi Mativila ameandika kuwa wananchi walitoa malalamiko hayo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Mei 31, 2023 kuhusu mkanganyiko wa mipaka ya Hifadhi ya Jumuiya ya ISAWIMA na Hifadhi ya Pori la Akiba la Igombe kuingia kwenye maeneo ya vijiji vilivyo kwenye Tarafa yao.
Kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliagiza iundwe timu ya wataalamu kutoka ofisi hiyo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Malisili na Utalii, TAWA, TFS, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, CHAWAUTA na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kwa ajili ya kufanya mapitio ya mipaka husika na itoe mapendekezo ya suluhu ya mgogoro huo.
Mhandisi Mativila ametaja tarehe ya kuanza kazi kwa timu hiyo kuwa ni Agosti 28, 2023 na kuelekeza ofisi hizo kuteua maafisa watakaoiunda na alioelekeza waripoti kwa Afisa Msimamizi Nyanda za Malisho, Godfrey Mgasa.
Siku hiyo hiyo, Agosti 25, 2023 Mhandisi Mativila aliandika barua nyingine kwenda kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, akimwelekeza amjulishe Mkurugenzi wa Halmashauri wa Wilaya ya Kaliua juu ya ujio wa timu ya watalaamu ya kutatua mgogoro wa wananchi wa Tarafa ya Igagala kuhusu mipaka ya hifadhi na vijiji.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba GB.203/350/01/15 inataja tarehe ya kuwasili kwa timu hiyo ya watalaamu, ofisi ambazo wataalamu wanaounda timu hiyo wanatoka, muda wa kazi wa timu, bango kitita la wataalamu na inamwelekeza katibu tawala kufikisha mjumbe kwa mkurugenzi wa halmashauri kutoa ushirikiano wa kutosha kwa timu.
Wakati Wizara ya Maliasili na Utalii na TAMISEMI zikifafanua na kuchukua hatua za kushughulikia mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dk. Rashid Chuachua, kwa nyakati tofauti alizofanya mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog, amesema hakuna mgogoro wowote katika eneo lake la utawala, hakuna mifugo inayouawa wala mazao yanayofyekwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dk. Rashid Chuachua
Dk. Chuachua ameiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa hana taarifa za kuwepo mgogoro wa mipaka baina ya hifadhi na vijiji na hakuna taarifa iliyofikishwa kwake kuhusu mazao ya wakulima kufyekwa, mifugo kuuawa huku ulipishaji faini kinyume cha taratibu akieleza kuudhibiti tangu alipoingia ofisini, mapema mwaka jana.
“Nina miezi 10 katika Wilaya ya Kaliua sijapata taarifa yoyote ya kuuawa kwa ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku wala njiwa. Masuala ya uhifadhi ni nyeti, funga safari njoo Kaliua kwa sababu hayo yote unayoniambia ni uongo,” alisema Dk. Chuachua.
Afisa mwingine aliyetofautiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na TAMISEMI ni Kamanda wa Uhifadhi wa Pori la Akiba Igombe, Justine Dyanabo ambaye katika mahojiano marefu na Tanzania PANORAMA Blog, alisema hakuna eneo lolote la vijiji lililochukuliwa wakati wa kugawanya mipaka ya hifadhi na vijiji.
Dyanabo anasema hifadhi iliyopo Kaulia inaitwa Pori la Akiba Igombe ambalo lilipandishwa hadhi na Rais kwa tangazo la gazeti la serikali namba 455, Julai 25, 2021.
Dyanabo anatofautiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kueleza kuwa kwa mara ya kwanza ISAWIMA ilisajiliwa mwaka 2007 kama jumuiya ya hifadhi ya jamii (WMA) na baada ya eneo lake kupungua ilisajiliwa tena Desemba mwaka jana.
Anasema TAWA haina operesheni yoyote ndani ya hifadhi kwani operesheni huwa zinafanyika kwa amri maalumu ya kitaifa na amri ya kufanyika hutolewa na watu wenye madaraka ya kutoa amri hiyo.
Akizungumzia kuhusu mazao ya wakulima kufyekwa, mafugo kuuawa na uvunjifu wa haki za binadamu, anasema watu hawachinjani kwa sababu ya ISAWIMA bali ni vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na wahalifu kwa sababu zao.
Aidha, anasema ISAWIMA inaendesha doria za kawaida za kukamata mifugo inayoingia hifadhini na inatoza faini mifugo inayokamatwa, kuanzia Shilingi 200,000 hadi Shilingi milioni 10.
ENDELEA KUSOMA TANZANIA PANORAMA BLOG KUFAHAMU MENGI ZAIDI KUHUSU SAKATA HILI.