RIPOTA PANORAMA
SERIKALI imeibiwa mabilioni ya fedha za faini wanazotozwa wafugaji wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora.
Fedha za faini zilizoibiwa ni zile zinazokusanywa na ‘watu’ kutoka kwa wafugaji wanaoingiza mifugo yao katika Pori ya akiba la Igombe na eneo la Jumuiya ya Hifadhi za Jamii la ISAWIMA.
ISAWIMA imeweka watu wanaotoza faini wafugaji wanaokamatwa na mifugo ndani ya eneo la hifadhi na kuwaandikia risiti za mkono kwa kutumia vitabu vya kukusanya ushuru vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Rashid Chuachua amethibitisha serikali kuibiwa mabilioni ya fedha zilizokusanywa kama faini kutoka kwa wafugaji waliokamatiwa mifugo yao ndani ya hifadhi.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog jana, pamoja na mambo mengine, Chuachua alisema fedha za faini walizokuwa wakitozwa wafugaji kabla hajakalia kiti cha ukuu wa Wilaya ya Kaliua zilikuwa zinapokelewa mkononi kisha zinaandikiwa risiti za mkono badala ya utaratibu wa kawaida wa malipo hayo kufanyika benki, hivyo kupotelea mikononi mwa watu wachache.
Alisema wizi huo aliukomesha Machi, 2023 baada ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo na kuagiza faini zote wanazotozwa wafugaji zilipwe benki na wafugaji kuwasilisha risiti za malipo kisha kurejeshewa mifugo yao.
Kauli hiyo ya Chuachua imeungwa mkono na Kamanda wa Pori la Akiba Igombe, Justine Dyanabo ambaye katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog jana, alisema hivi sasa faini zote zinalipwa kwenye akaunti ya Benki ya ISAWIMA ambayo mmiliki wake ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.
Dyanabo alisema ISAWIMA imekuwa ikiendesha doria za kawaida za kukamata wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi na kuwatoza faini kati ya Shilingi 200,000 hadi milioni 10.
Alisema kabla ya kuanza kwa utaratibu wa sasa wa faini zote kulipwa benki, wafugaji walilipishwa na waliokamata mifugo yao na kuandikiwa risiti za mkono kwa kutumia vitabu vya kukusanya ushuru vya Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.
Alisema utaratibu huo ulipigwa marufuku baada ya Chama cha Wafugaji kuibua wizi mkubwa uliokuwa ukifanyika na kuwasilisha hoja kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kikitaka kusitishwa mfumo huo wa ulipaji faini; hoja ambayo ilifanyiwa kazi haraka.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya ISAWIMA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Usinge, Stanley Wilson yeye ameieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa wafugaji wanapokamatwa kwenye maeneo ya hifadhi hutozwa faini ya hadi Shilingi milioni 20 na kuandikiwa risiti za mkono.
Alisema kiwango hicho cha faini ni kikubwa na kinatozwa kimabavu na kinyume cha utaratibu hivyo kusababisha vurugu zinazotishia usalama wa watu na mauaji ya mifugo.
Awali, taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zilidai kuwa uongozi wa ISAWIMA unawatoza faini ya Shilingi milioni moja wananchi wanaoingia kwenye maeneo ya hifadhi bila kibali na ng’ombe anayekamatwa ndani ya hifadhi analipishwa Shilingi 106,000.
Baadhi ya wafugaji wanaolalamikia faini hizo walisema zinatozwa kienyeji na zinatumika kuwakomoa wafugaji wanaohoji au kupinga mfumo huo wa utozaji faini.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog umebaini kuwepo kwa mgogoro baina ya wakulima na wafugaji dhidi ya viongozi wa ISAWIMA, halmashauri na serikali ya wilaya.
Mgogoro huo ambao sasa umeanza kuibua viashiria vya uvunjifu wa amani, chanzo chake ni mipaka ya ardhi ya Hifadhi ya Pori la Igombe na vijiji vinavyopakana na pori hilo.
Uchunguzi umebaini kuwa, wenyeviti wa vijiji 11 vilivyopo Tarafa ya Igagala ambao mwaka 2007 waliunda Jumuiya ya Uhifadhi waliyoipa jina la Igombe and Sagala Wildlife Management Area (ISAWIMA) kwa lengo la kutunza maeneo yaliyokuwa wazi kwa ajili ya matumizi ya baadaye, hivi sasa hawaelewani.
Jumuiya hiyo ambayo ilikuwa na wajumbe watatu kutoka kila Kijiji ilikumbwa na migogoro ya uongozi baada ya wajumbe kutuhumiana kushindwa kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwake na kuweka mbele maslahi binafsi.
Baadhi ya mambo yaliyobainika kuipasua jumuiya hiyo ni usiri wa mapato na matumizi na uongozi wa jumuiya kushindwa kutoa gawio la asilimia 20 ya mapato yanakusanywa kwa vijiji wanachama wa jumuiya ambavyo ni wamiliki wa ardhi iliyotolewa kwa uhifadhi kama ilivyokubaliwa huku asilimia 20 ya mapato iliyoelekezwa kupelekwa ofisi ya mkurugenzi wa halmashari ikiwasilishwa kikamlifu.
Jambo jingine lililobainika kuigawa jumuiya hiyo ni kushindwa kubadilisha mipaka kila baada ya miaka mitano kutokana na ongezeko la watu kwa mujibu wa makubaliano ya kutunzwa kwa eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya baadaye na hivyo kusababisha uvunjifu wa sheria kabla serikali haijatwaa hekta 1300 ilizozitangaza kuwa Hifadhi ya Pori la Akiba la Igombe.
Uchunguzi umeonyesha kuwa serikali ilitwaa hekta 1300 na kuacha sehemu kidogo ya ardhi kwa wanakijiji kwa ajili ya shughuli za uhifadhi; sehemu hiyo ya ardhi ndiyo inayosababisha migogoro inayodaiwa kuwa chanzo cha mauaji ya mifugo, kutishia usalama wa watu na kufyekwa kwa mazao yaliyo shambani.