Saturday, September 6, 2025
spot_img

‘MBOWE KUMUOMBA HELA RAIS SAMIA NI ‘MCHEZO,’ UKOMAVU, NIA NJEMA’

RIPOTA PANORAMA

KITENDO cha Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan mchango wa hela kwa ajili ya ujenzi wa kanisa, kimeibua hisia na maoni tofauti miongoni mwa makundi mbalimbali katika jamii.

Wanasiasa, wanasheria, wanazuoni na wafuatiliaji wa mambo waliozungumza na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu ombi la hela lililotolewa na Mbowe kwa Rais Samia kwa ajili ya ujenzi wa kanisa na yeye akaitikia kwa kuchangia Shilingi milioni 150, wametoa maoni yao ambayo kimsingi yanaonyesha kuunga mkono kitendo hicho.

Jumapili, Disemba 31, 2023, Mbowe akiwa katika Kanisa la Kilutheri mkoani Kilimanjaro, alitaja waliochangia harambee ya ujenzi wa kanisa hilo kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Samia.

“Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameishaweka taslimu kwenye akaunti yetu Shilingi milioni 10, na wa mwisho ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan na familia yake wametupa tayari mchango, kwenye akaunti ya kanisa Shilingi milioni 150,” alisema Mbowe.

Kumekuwa na maoni mengi tofauti tangu Mbowe atangaze Rais Samia kutoa mchango wa hela kwa ajili ya ujenzi wa kanisa na miongoni mwa waliotoa maoni ni Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba huku wakili maarufu Profesa Rugemeleza Nshalla akikataa katakata kusema chochote.

Akitoa maoni yake, Jaji Warioba aliwashangaa wanaohusisha kitendo cha Rais Samia kuchangia kanisa na siasa na alionya kuwa rais wa nchi asihusishwe na makundi.

Jaji Joseph Warioba

Kwa maneno yake mwenyewe katika hilo na kwa kuzingatia uzito wa ujumbe wake, tunanukuu neno kwa neno: “Lina uhusiano gani na siasa hilo jambo, na je ametoa kwa Mbowe au ametoa kwa kanisa? Yeye ni rais na Mbowe haongozi kanisa, anaongoza chama cha siasa. Mimi sijui kama Mbowe ana kanisa.

“Huyu ni rais wa nchi, amechangia mara ngapi? Rais huwa anatoa michango, siyo mara ya kwanza rais kutoa mchango kwa kanisa au msikiti, sasa hili tofauti yake ni nini na michango mingine aliyotoa.

“Huyu ni rais wa kila mtanzania, anapotoa msaada ni rais ametoa msaada na ninavyoelewa ametoa msaada kwa kanisa, sasa Mbowe anaingiaje hapo.

“Rais mumtizame kama kiongozi wa nchi, msiwe mnaona vitendo vyake mnavihusisha na makundi, hilo ndilo limetugawanya. Naona rais ametoa mchango kama rais na imekuwa kawaida yake kutoa mchango kwa vikundi mbalimbali bila kuangalia kikundi hiki ni cha nani.

“Viongozi wengi sana wameongoza harambee ambalo ni jambo la kawaida. Nilikuwa sijasikia kwamba kiongozi ameongoza harambee ikaonekana kama ajabu, kwani kuna tatizo gani viongozi kuongoza harambee?

Rais Samia Suluhu Hassan

“Haya mambo yanayohusu jamii na mara nyingi nimesema hili kwamba shughuli za jamii kuziingiza katika siasa tunawagawa watu, akionekana wa chama hiki inakuwa siyo shughuli ya kijamii inakuwa ya kisiasa. Tukumbuke rais ni rais wa watanzania wote, tumsigawe rais kuwa ni wa hawa, wale hawahusiki. Tuache kuchukua mambno madogo madogo haya.”

Mhadhiri Mwandamizi  Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaveli Lwaitama yeye alisema Mbowe na Rais Samia wanajuana, ni wajanja na wanajua kucheza michezo ya kisiasa.

“Muktadha ni kwamba kuna Kanisa la Kilutheri walikuwa wanachanga hela za kukamilisha majengo yao. Wakaamua kumchangua Mbowe, (Freeman) ndiyo atamke waliochangia na yeye akajenga msingi kwamba katika kuchangia walialikwa watu wote, bila kujali chama wala nini,” alisema Dk. Lwaitama.

Alisema kwa jicho la uchambuzi wa mambo aliiona hatari iliyo mbele ya Mbowe kutokana na kauli yake hiyo lakini msingi alioujenga kabla ya kuitoa unagusa kila mmoja.

“Aliorodhesha watu wote waliochangia, waziri mkuu na wengine kisha rais, kuwa na yeye alimuomba achange na yeye ametuchangia na akasisitiza ameona hela imeingia kwenye akaunti ya kanisa. Kiuchambuzi nikasema huyu anajua juu ya hisia zitakazoibuliwa?

“Lakini alikuwa amejenga msingi tangu mwanzo kwamba alialikwa kila mtu bila kujali chama au jinsia yake. Rais naye kuchangia alikuwa anajua kwamba aliyempigia simu ni mshindani wake kisiasa na yuko kwenye ngome yake.

Dk. Azaveli Lwaitama

“Kwa hiyo rais alikuwa anamaanisha akichangia pale watampigia makofi nyumbani kwa mshindani wake lakini na mshindani wake alikuwa anasema si mimi ndiyo natangaza niliowafikia watuchangie kwa hiyo waumini watasema hata washindani wangu kisiasa nimewafikia,” alisema.

Dk. Lwaitama alieleza zaidi kuwa Mbowe na Rais Samia ni viongozi mahiri katika mchezo wa siasa na kwamba Mbowe alikuwa anatengeneza njia nzuri ya kisiasa nyumbani kwake na Rais Samia alikuwa anatafuta kujipenyeza mioyoni mwa wananchi wa eneo la mpinzani wake.

“Mbowe ana roho fulani kama ya Rais Samia ya kutokuwa na chuki ya kupitiliza. Hii inaonyesha wanasiasa hawa, Rais Samia na Mbowe wanaishi dhana ya uvumilivu, kutojenga chuki, na ni waumini wa wanachokizungumza,” alisema.

Akizungumzia mapokeo ya tukio hilo kwa jamii alisema Mbowe atakuwa amejitengenezea maadui na wapo watakampongeza, vivyo hivyo kwa Rais Samia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wapo ambao hawajafurahi lakini alisisitiza kuwa Mbowe na Rais Samia ni wanasiasa mahiri katika siasa za ushindani wa amani.

Wakili maarufu nchini, Profesa Rugemeleza Nshalla alipoombwa kutoa maoni yake kuhusu hilo, alikataa kusema chochote na kutaka aulizwe Rais Samia mwenyewe aliyetoa mchango.

Profesa Rugemeleza Nshalla

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema yeye alisema ni jambo zuri kwa Rais Samia ambaye siyo mkristo kuchangia nyumba ya ibada ya wakristo.

Akirejea historia, alisema hata Hayati Rais John Pombe Magufuli alipata kulifanya jambo hilo akiwa kanisani huko Dodoma alipochangisha hela kwa ajili ya ujenzi wa msikiti hivyo alichokifanya Rais Samia kinaunganisha taifa.

‘Ni jambo zuri kwa sababu linaunganisha taifa, lakini kwa upande wa pili linaonyesha mwenyekiti wa harambee ambaye ni Freman Mbowe ameonyesha jinsi alivyo na uwezo wa kushawishi hata watu ambao hawako upande wake.

John Mrema

“Mahasimu wake wa kisiasa kushiriki tukio ambalo anasimama yeye ni jambo linaloonyesha uwezo wake wa kushawishi hata viongozi ambao hawako upande wake,” alisema Mrema.

Wakili Mashuhuri, Jebra Kambole akitoa maoni yake, alisema anakiangalia kitendo cha Rais Samia kuchangia kanisa kama ishara ya kuondoa ubaguzi na kujenga ushirikiano na vyama vya siasa vya upinzani.

Hata hivyo, Wakili Kambole alisema  mtizamo wake mwingine katika hilo ni harambee za aina hiyo kuelekezwa zaidi kwenye mambo yanayohusu huduma za kijamii.

Wakili Jebra Kambole

“Lakini nafiriki watanzania wanahitaji zaidi huduma za kijamii kuliko huduma za kikanisa. Michango ingewekezwa kwenye vitu ambavyo vinahudumia watanzania wote kama hospitali, maji na shule.

“Sibezi umuhimu wa kanisa, lina nafasi yake lakini kuna vitu ambavyo vina umuhimu zaidi ikiwemo huduma za jamii. Nadhani mtizamo mkubwa wa harambee zielekee kwenye huduma za kijamii kwa sababu huu msaada ni kutafuta umaarufu wa kisiasa kwa pande zote mbili, upinzani na chama tawala.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya