RIPOTA PANORAMA
WANANCHI wenyeji wa Kijiji cha Msomera, kilichopo Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga wamedai kutoridhishwa na uamuzi wa Serikali kuwaweka katika kundi la wavamizi kwenye kijiji hicho.
Wamekaririwa wakieleza kuwa walianza kuishi kwenye Kijiji cha Msomera muda mrefu wakiendesha maisha yao kwa kujishughulisha na kilimo na kwamba serikali ilikuwa ikiwapelekea huduma mbalimbali za kijamii kama shule, zahanati, barabara, mradi wa maji na mradi wa madume ya ng’ombe uliozinduliwa mwaka 2014 na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) pamoja na baadhi ya wanachama wake waliofanya ziara katika Kijiji cha Msomera, April 24 hadi 25, 2023, wananchi hao wanatambulika na serikali kama wenyeji halali wa kijiji hicho.
Ripoti inaeleza kuwa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania pamoja na baadhi ya wanachama wake walifanya ziara katika eneo hilo baada ya kuwepo taarifa kuwa wananchi wenyeji wa Msomera wamenyang’anywa ardhi yao na kugawiwa wageni waliohamishiwa kwenye kijiji hicho kutoka Tarafa ya Ngorongoro, mwaka 2022.
THRDC inaeleza katika ripoti yake kuwa wananchi wenyeji wa Kijiji cha Msomera wanailalamikia serikali kutwaa maeneo yao kwa nguvu bila kuwalipa fidia ya aina yoyote na pia kuwaita wavamizi huku waliohamia kutoka Tarafa ya Ngorongoro wakifanyiwa tathmini na kulipwa fidia kabla ya kuhamishwa.
“Namna ardhi yao ilivyotwaliwa ndio malalamiko yao makubwa zaidi kwamba, waliona tu vikosi vya askari vimezunguka maeneo yao na nyumba mpya kujengwa walizopewa wageni na wao kupewa taarifa tu kuwa eneo lao wamepewa watu kutoka Ngorongoro.
“Wananchi wenyeji walidai zaidi kuwa hawana maeneo ya kulima kwa sababu maeneo waliyokuwa wanalima wamepewa wageni ambao tayari wameshalima,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Ripoti inaeleza zaidi kuwa chimbuko la mgogoro katika Kijiji cha Msomera ni taarifa kuwa eneo la Msomera ni pori tengefu hivyo hakuna mtu yeyote anayekalia eneo hilo.
“Hata hivyo, baada ya wananchi kuhamia katika kijiji hicho, malalamiko kadhaa yalizagaa kwenye vyombo vya habari kuwa Serikali imetwaa ardhi ya wananchi wenyeji na kuwapa wageni waliotoka Ngorongoro bila fidia ya aina yoyote ile,” inasomeka sehemu nyingine ya ripoti.

Albert Msando
THRDC imemkariri Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando akikiri baadhi ya maeneo katika Kijiji cha Msomera kupewa wageni kutoka Tarafa ya Ngorongoro.
Kwamba DC Msando alieleza kuwa kila familia iliyopo Msomera imepewa ekari 2.5 za makazi na ekari 5 kwa ajili ya kilimo bila kujali kuwa ni mgeni au mwenyeji.
Ripoti imemkariri DC Msando kuwa uamuzi wa kugawanya ardhi sawia ulifikiwa kwa sababu Kijiji cha Msomera kilisajiliwa kimakosa mwaka 1992 kwani eneo lote hilo lilikuwa Pori Tengefu la Handeni tangu mwaka 1974.
“Siku ya kwanza ya ziara tulionana na kufanya majadiliano na uongozi wa Wilaya ya Handeni na baadae uongozi huo chini ya Mkuu wa Wilaya, Albert Msando tulitembelea miradi ya maendeleo inayojengwa na serikali katika Kijiji cha Msomera,” inasomeka zaidi ripoti.
Rekodi zilizokusanywa na THRDC na kuwekwa kwenye ripoti yake hiyo zinaonyesha kuwa Msomera ni Kijiji kilichopo Kata ya Misima, Tarafa ya Sindeni, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga.
Kijiji cha Msomera kilisajiliwa mwaka 1992 na kupewa hati ya usajili yenye namba TA/KIJ/576 na kabla hakijasajiliwa kilikuwa sehemu ya Kijiji cha Mbagwi, ambacho kilisajiliwa wakati wa oparesheni vijiji, miaka ya 1970.
Tangu kiliposajiliwa, Kijiji cha Msomera kiliendelea kupata huduma mbalimbali za kijamii kama vile shule, zahanati, mradi wa maji, ofisi za kijiji na huduma zingine muhimu za kijamii.
Mwaka 2014, Rais Mstaafu Kikwete alizindua mradi wa madume ya mbegu ya ng’ombe wa kisasa katika Kijiji cha Msomera na wakati akizindua mradi huo aliwahimiza wananchi kuongeza maeneo kwa ajili ya ufugaji na malisho.
Baada ya maagizo ya mstaafu Kikwete, mwaka 2016 wananchi waliandaa na kupitisha mpango wa matumizi bora ya ardhi wa mwaka 2016-2026.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa Ngorongoro
Kupitia mpango huo, halmashauri ya kijiji ilitenga maeneo ya makazi, kilimo, malisho na maeneo ya huduma za kijamii pamoja na kutunga sheria ndogo kwa ajili ya kusimamia mpango huo.
Januari 11, 2022 serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ilitangaza wito kwa wananchi kuhama kutoka katika Tarafa ya Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera.
Baada ya agizo hilo la Mkuu wa Mkoa, wananchi walifanya mikutano mbalimbali kujadili hatima ya maisha yao pamoja na ardhi yao katika Tarafa ya Ngorongoro.
Katika mikutano yao, wananchi walijadili na kujiuliza ni kwanini serikali haijawashirikisha kikamilifu kuhusu mpango wa watu kuhamishwa kwa hiari na kwamba huo uhiari ukoje ukizingatia kwamba wao kama wahusika hawakushirikishwa?
Maswali hayo hayakuwa na majibu hivyo waliendelea kufanya maombi ya kutaka kukutana na viongozi wa serikali kwa kuandaa mapendekezo ya namna bora ya kuhifadhi eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro huku wao wakiendelea kuishi katika eneo hilo.
Mapendekezo yao yaliwasilishwa rasmi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa lakini hayakufanyiwa kazi hivyo kuzua hofu kuwa hawasikilizwi na serikali.
Februari 17, 2022 Waziri Mkuu Majaliwa alifika Ngorongoro na kuongea na wananchi kufafanua kuhusu kinachoitwa ‘zoezi la kuhama kwa hiari.’
Juni 07, 2022 ikiwa takribani miezi minne baada ya Waziri Mkuu Majaliwa kufika Tarafa ya Ngorongoro, wananchi wa eneo hilo waliona vikosi vya askari wakiwa na silaha nyingi za moto wakizunguka maeneo yao ya makazi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwaaga wananchi wa Ngorongoro waliohamia Kijiji cha Msomera kwa hiari
Vikosi hivyo vilitapakaa katika maeneo mbalimbali kwenye Tarafa ya Ngorongoro na wakati huo huo viongozi wa serikali na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro walifika na kufanya tathmini na makadirio ya vitu ambavyo familia inamiliki na kisha kuondoka.
Ripoti hiyo inaeleza zaidi kuwa siku moja kabla ya wananchi kuhamishwa, walipigiwa simu wakitakiwa kufika Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, yaliyopo Karatu ambako walisainishwa kiasi cha fedha walichotakiwa kulipwa kama fidia.
Wakati wakielekea Karatu, maboma yao yalikuwa yanabomolewa na safari ya Karatu ndio ilikuwa mwanzo wa safari yao kuelekea Kijiji cha Msomera.