Wednesday, December 25, 2024
spot_img

TAARIFA ZAKINZANA NGORONGORO

RIPOTA PANORAMA

IMEELEZWA kuwa serikali ilifumbia macho jitihada za wananchi wakazi wa Ngorongoro, mkoani Arusha kutaka ushirikishwa kabla ya kuanza kutekelezwa kwa agizo la kuwahamisha kwenda Kijiji cha Msomera, kilichopo Handeni, Mkoa wa Tanga.

Hayo yamo kwenye taarifa ya hivi karibuni ya mtandao wa watetezi wa haki za binadamu na wanachama wake, uliyofanya ziara Ngorongoro na kuzungumza na wananchi walioeleza dosari za changamoto; kabla na baada ya kuhamishwa.

Taarifa hiyo ya mtandao wa haki za binadamu inaeleza kuwa ikishirikiana na wanachama wake; ilifanya ziara hiyo kati ya April hadi Septemba, 2023 na kuibuka na mambo ambayo hayajapata kusemwa kwa uhakika tangu serikali ilipoanza kuwahamisha wananchi hao.

Katika taarifa hiyo, mtandao wa watetezi wa haki za binadamu na wanachama wake, unachukua njia tofauti na tamko la serikali lililotolewa mapema mwezi huu na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi kuhusu mwenendo wa shughuli ya kuwahamisha wananchi wa Ngorongoro.

Kwa mujibu wa taarifa ya mtandao huo, Januari 11, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Arusha alitangaza wito kwa wananchi kuhama kwa hiari kutoka katika Tarafa ya Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga.

Taarifa inaeleza kuwa wananchi kwa kushirikiana na viongozi wao wa kimila na kisiasa walifanya mikutano na jitihada mbalimbali wakitaka ushirikishwaji katika uamuzi huo bila mafanikio.

Aidha, taarifa inaeleza kuwa wananachi walifanya vikao mbalimbali vya kujadili hatua za kuchukua ili kunusuru ardhi yao kuchukuliwa bila ridhaa yao pamoja na kujadili changamoto zilizokuwa zinawakabili watetezi wa ardhi Ngorongoro.

Inaeleza zaidi kuwa wananchi na makundi ya kijamii hayakupewa nafasi ya kushirikishwa katika uamuzi huo licha ya mashirika ya haki za binadamu kuratibu vikao vya wananchi, watetezi wa ardhi na haki za binadamu kujadili na kuandaa mapendekezo kabla ya kuanza kutekelezwa kwa amri ya mkuu wa mkoa ya watu kuhama kwa hiari.

Nyumba za Msomera

ā€œWananchi waliohamishwa kutoka Ngorongoro hawakupewa chaguo kama wanataka kwenda Msomera au sehemu nyingine ambayo wao wangependa kuhamia.

ā€œMchakato ulikuwa wa siri na wananchi hawakupewa mrejesho wa tathmini iliyofanyika na kiwango ambacho walistahili kulipwa,ā€ inasomeka sehemu ya taarifa.

Taarifa hiyo inawanukuu wananchi waliohamishwa kuwa fedha pekee iliyofahamika tangu awali kuwa watalipwa ni fedha taslimu za kitanzania Shilingi milioni 10, maarufu kama ā€œasante mamaā€ wanayosema ni fedha ya Rais Samia Suluhu Hassan.

ā€œLakini pia fidia haikuzingatia ukweli kwamba wananchi wa Ngorongoro walizuiwa kufanya shughuli za kimaendeleo kama vile kujenga nyumba za kisasa, kilimo na kumiliki vyombo vya usafiri. Wananchi wengi walipewa fidia ya kuanzia milioni moja hadi milioni tatu,ā€ inasomeka taarifa hiyo.

Kuhusu huduma za msingi za jamii kwa wananchi hao, taarifa inawanukuu tena wananchi kuwa walinyimwa huduma za kijamii ili kuwalazimisha kuhamia Kijiji cha Msomera.

Kwamba huduma mbabalimbali za jamii kama vile huduma za mabweni kwa shule za msingi na sekondari, vyoo mashuleni, afya, barabara, maji na vibali vya ujenzi hazikutolewa.

Mapema mwezi huu, Msemaji Mkuu wa Serikali, Matinyi katika mkutano wake na wana habari Jijini Dar es Salaam alisema serikali inafanya tathmini kwa kila mtu alichonacho kisha inamlipa na baada ya kulipwa kila kaya inapewa Shilingi milioni 10.

Matinyi alisema baada ya malipo hayo kufanyika, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inamuhamisha muhusika, familia na mali zake zote ikiwemo mifugo kutoka Ngorongoro mpaka Kijiji cha Msomera bila kulipishwa.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi

Alisema kazi ya kuwahamisha wananchi kutoka Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera sasa ipo katika awamu ya pili iliyoanza Julai, 2023 na inatarajiwa kukamilika Machi, 2924.

Msemaji Mkuu wa Serikali alisema lengo la serikali ni kujenga nyumba 5000 katika eneo linalojumuisha Vijiji vya Kitwai, Sauni na Msomera na kwamba nyumba hizo zinatarajiwa kuchukua kaya zilizopo Ngorongoro na aidha, serikali haimzuii mtu aliyepo Ngorongoro kwenda sehemu nyingine ya nchi kwa sababu kila mtanzania ana uhuru wa kwenda popote.

Akizungumzia jinsi maandalizi ya kuwahamisha wananchi hao yalivyofanyika, Matinyi alisema wizara 10 zilikwenda Ngorongoro na kuunda timu ya pamoja ili kufanikisha oparesheni ya kuwahamisha wananchi hao.

Alizitaja wizara hizo kuwa ni Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Maliasili na Utalii, Nishati, Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kilimo, Maji, Mifugo na Uvuvi, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mambo ya Ndani na Katiba na Sheria.

Alisema muunganiko huo wa wizara za kisekta ndiyo unaofanya kazi ya kubadilisha lililokuwa pori kugeuka kuwa makazi ya kisasa ya wananchi wanaotoka Ngorongoro kwenda Msomera.

ā€œKinachofanyika Msomera, mbali na tume inayoshughulika na masuala ya ardhi kufanya kazi ya kupima viwanja na viwanja hivyo kujengwa nyumba, kuna kazi ya kujenga barabara na mifumo ya umeme,ā€ alisema Matinyi na kuongeza kuwa:

ā€œKila mwananchi anayejengewa nyumba anapewa fursa ya kuunganishiwa umeme na Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) kwa gharama ile ile ya Shilingi 27,000 na wizara ya maji inachimba visima ambavyo vitakuwa na sehemu ya kusambaza.ā€

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya