RIPOTA PANORAMA
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) leo imefungua rasmi ofisi zake katika Jiji la Lilongwe, Malawi.
Kufunguliwa kwa ofisi hizo kunalenga kuboresha utoaji huduma kwa wateja wa Bandari ya Dar es Salaam walioko nchi jirani.
Taarifa ya kufunguliwa kwa ofisi hizo iliyotolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kwa Tanzania PANORAMA Blog, imeeleza kuwa kunadhihirisha dhamira ya Bandari ya Dar es Salaam kutoa huduma bora kwa wananchi wa Malawi.
Mbossa amesema Malawi ambayo imeunganishwa na ardhi ni miongoni mwa nchi saba zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam kama lango kuu la uagizaji na uuzaji bidhaa nje ya nchi hiyo.
Ametaja wateja wengine wa Bandari ya Dar es Salaam kuwa ni nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Rwanda, Burundi, Uganda na Zimbabwe.

“Jukumu kubwa la uuzaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, hususan Bandari ya Dar es Salaam sasa litakuwa kwenye ofisi iliyofunguliwa Malawi,” amesema Mbossa.
Alizitaja baadhi ya huduma ambazo zitatolewa na ofisi hiyo iliyofunguliwa Jijini Lilongwe, kuwa ni pamoja na kuwapa taarifa mpya ya miradi mipya na inayoendelea kutekelezwa nchini, mifumo na vifaa pamoja na kupokea malalamiko ya wateja, wamiliki wa mizigo wa nchini Malawi.
Mbossa amesema Malawi ni mteja namba nne kwa ukubwa wa Bandari ya Dar es Salaam ikitanguliwa na nchi za DRC, Zambia, Rwanda na Burundi na shehena ya mizigo ya nchi hiyo inayopitia Bandari ya Dar es Salaam iliongezeka kwa asilimia 18.3, mwaka 2022, ikiwa ni tani 557,826.